CALFORNIOA, MAREKANI
MABADILIKO kwenye mtandao maarufu wa simu, WhatsApp, yataanza rasmi leo wakati kipindi cha siku 30 cha kukubali masharti mapya kitakapomalizika.
Mabadiliko hayo yanawataka watumiaji kusambaza taarifa zao kutoka Whatsapp hadi Facebook, mtandao ulioinunua Whatsapp kwa S. trilioni 22 mwaka 2014.
Hata hivyo, unapokubali masharti hayo haimaanishi kuwa Facebook itadukua taarifa za mtumiaji kutoka Whatsapp kwa vile kwa siku 30, ana hiari ya kuchagua kusambaza au kutosambaza taarifa zake kwa Facebook.
Watakaokataa kusambaza taarifa zao, wataendelea kutumia Facebook kama kawaida ila watakaokubali, kufikia leo hawataweza tena kuubatilisha uamuzi huo.
Facebook ilisema Ijumaa kuwa hii ni mara ya kwanza kwao kufanya mabadiliko makubwa kwa Whatsapp tangu ianze kuimiliki.
“Hili ni jambo la kawaida kwa kampuni zilizonunuliwa lakini tunajitahidi kuwapa watumiaji hiari ya kuchagua iwapo Facebook itatumia taarifa zao za Whatsapp kuwaletea matangazo na bidhaa zinazolingana na matakwa yao,” Facebook ilisema.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa mitandao hiyo miwili itazidi kushirikiana ili kuboresha huduma zao mbalimbali.
Baadhi ya watumiaji wanahofia kuwa kukubali kusambaza taarifa zao kutaifanya Facebook kudukua undani wao huku wengine wakikubali bila wasiwasi.
Hata hivyo, wataalamu wanaamini hakuna haja ya kuhofia kwani Whatsapp ina mbinu maalumu ya kukinga ujumbe kutosomwa na yeyote asiyekusudiwa yaani ‘encryption’.
Facebook ina zaidi ya watumiaji bilioni moja kote duniani.