24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa: Imarisheni doria kuzuia uvuvi haramu

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa.
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa.

Na Mwandishi Wetu, Mafia

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewaagiza Mkuu wa Wilaya ya Mafia mkoani Pwani, Shaib Nnunduma  na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Eric Mapunda kuimarisha doria kwenye eneo la Bahari ya Hindi ili kuzuia uvuvi haramu.

Alisema vitendo vya uvuvi haramu vinavyoendelea katika wilaya hiyo,vinapaswa kudhibitiwa haraka kwa sababu vinasababisha halmashauri kukosa mapato na kushindwa kuboresha maendeleo ya wananchi.

Waziri mkuu ametoa agizo hilo kwa nyakati tofauti juzi, wakati alipotembelea kiwanda cha samaki cha Tanpesca na kuhutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Kirongwea.

Alisema uvuvi ndiyo shughuli kuu ya uchumi na chanzo muhimu cha mapato kwa wilaya ya Mafia na suala la uvuvi haramu linaathiri sana mapato ya halmashauri hivyo ni vema wakaimarisha doria ili kukomesha vitendo hivyo.

“Lazima jambo hili lidhibitiwe. Uvuvi wa kutumia mabomu unaharibu mazingira ya chini ya bahari hivyo samaki wanashindwa kuzaliana kwa wingi. Hakikisheni watu hao wanakamatwa na kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kuteketeza zana wanazotumia,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Alphakrust inayomiliki Kiwanda cha Tanpesca, Ganeshen Vedagiri alisema kampuni hiyo imeajiri watumishi 855 kati yake 445 ni wakazi wa  Mafia, huku wanawake wakiwa 250.

Alisema wana mabwawa 76 ya kufugia samaki aina ya kamba na kwa sasa yanayotumika ni 30, kila moja lina uwezo wa kuzalisha kilo 5,000 katika siku siku 150 na kufanikiwa kuvuna tani 300 kwa mwaka.

Alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2016/17, wanatarajia kupata wastani wa Sh bilioni 120 katika mauzo ya nje na Sh bilioni 62 kutoka katika mauzo ya ndani. Wanatarajia kulipa kodi ya zaidi ya Sh bilioni 15 kwa mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles