Na Mwandishi Wetu, Nigeria
Mnenguaji nyota wa muziki wa dansi Mtanzania, Hassan Mussa ‘Super Nyamwela’ na bendi yake Ubuntu Traditional juzi alifanikiwa kuwachengua maelfu ya watu waliofurika katika shamra shamra za tamasha la kimataifa Calabar Carvinal Festival, linalofanyika mjini Calabar nje kidogo ya jiji la Abuja nchini Nigeria.
Nyamwela na bendi yake walitumia fursa ya dakika tatu walizopewa na waandaji wa tamasha hilo Serikali ya Nigeria kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ili wasalimie tu na kuangusha shoo ya nguvu iliyofanya washangiliwe kwa nguvu.
Maelfu ya watu waliojipanga pembezoni mwa barabara za mji wa Calabar waliwashangilia wasanii hao kwa namna walivyoamsha dude na kusababisha gumzo.
Ubuntu ilitumia nafasi hiyo kuonyesha watanzania wamekuja Calabar kwa ajili ya kutangaza utamaduni wa Tanzania na si kutalii hivyo kipande cha shoo hiyo ni sehemu ndogo ya makubwa waliyojiandaa kuyafanya siku ya kupanda jukwaani rasmi ambayo ni leo usiku wa Jumamosi Desemba 29.
Hii ni mara ya pili kwa Nyamwela na bendi yake ya Ubuntu kushiriki tamasha hilo ambalo linashirikisha nchi zaidi ya 60 duniani.
Kwa Tanzania ni Ubuntu pekee ndiyo imepata nafasi ya kutumbuiza katika tamasha hilo ambalo hufanyika kila mwaka kwa udhamini wa serikali ya Nigeria ambayo imekuwa ikilitumia kutangaza utalii wa nchi yake.
Tamasha hilo lilianza rasmi Desemba 4 mwaka huu na linatarajia kufikia tamati Januari 4 mwaka 2019.