NA WAANDISHI WETU, DAR/MIKOANI
BEI ya sukari hivi sasa haikamatiki, imezidi kupaa kila kona ya nchi, huku maeneo mengine ikiwa adimu na kusababisha taharuki kwa wananchi.
Kuadimika na kupanda bei kwa sukari kumetokana na hatua ya Serikali kupiga marufuku uagizaji wa bidhaa nje ya nchi kwa nia ya kulinda viwanda vya ndani. Uchunguzi wa MTANZANIA katika baadhi ya mikoa na wilaya nchini, umebaini uhaba mkubwa wa sukari ambao umesababisha wafanyabiashara wa jumla na rejareja kupandisha bei na kuzusha malalamiko kutoka kwa wananchi.
MOROGORO
Baadhi ya wananchi katika Manispaa ya Morogoro, wamelalamikia kupanda kwa bei ya sukari kutoka Sh 2,000 za awali hadi 3,000 kwa kilo moja, huku wafanyabiashara wa maduka ya rejareja nao wakilia kuuziwa bei ya juu katika maduka ya jumla.
Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wauzaji wa sukari ya rejareja, walisema kuwa katika siku za karibuni wamelazimika kununua mfuko mmoja wa kilo 25 kwa Sh 60,000 badala ya 35,000 hadi 40,000 za awali na ule wa kilo 50 hivi sasa unauzwa Sh 120,000 badala ya 48,000 na 50,000.
TANGA
Bei ya sukari katika Mkoa wa Tanga imepanda kutoka Sh 1,800 kwa kilo moja ambayo ilikuwa ikiuzwa mwanzoni hadi kufikia kati ya Sh 2,300 na 2,800.
Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA jana ulibaini kuwa kupanda huko kwa sukari kumetokana na Serikali kupiga marufuku sukari ya magendo iliyokuwa inaingizwa jijini humo kwa njia za panya.
Akizungumzia hali hiyo, mmoja wa wafanyabiashara wa rejareja, Julius Makundi alisema kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo muhimu hakuendani na kipato halisi cha maisha ya Watanzania walio wengi.
KITETO
Katika Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, kilo moja ya sukari hadi jana ilikuwa ikiuzwa kwa Sh 2,600 kutoka Sh 1,700 ya awali huku wafanyabishara wakidai upatikanaji wake ni mgumu kwa sasa.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Kanali Samweli Nzoka, alikiri kuwepo kwa uhaba wa sukari wilayani humo na kuahidi kuwasiliana na mamlaka husika kupata ufumbuzi wa suala hilo.
Bakari Maunganya mkazi wa Kiteto, alisema uwezekano wa mwananchi wa kawaida kunywa chai kwa sasa uko shakani kwani wengi wana vipato vidogo.
Mmoja wa wafanyabiashara wa duka la rejareja aliyefahamika kwa jina la Ijumaa Bakari, alisema kwa sasa hakuna duka linalouza sukari ya jumla wilayani Kiteto hivyo kufanya bidhaa hiyo kuadimika.
MWANZA
Jijini Mwanza, hivi sasa kilo moja imepanda kutoka Sh 2,500 hadi Sh 3,000 licha ya Serikali kutoa bei elekezi ya Sh 1,800.
Katika maduka mbalimbali ya Jiji la Mwanza juzi bei ya sukari ya rejareja ilikuwa Sh 3,000 kwa kilo moja na wachache waliuza Sh 2,900 kama mteja akinunua kuanzia kilo tano.
Hali hiyo imesababisha mamalishe nao kupandisha bei ya chai ya rangi kutoka Sh 100 hadi 200 huku ya maziwa ikifikia Sh 500 kwa kikombe kimoja.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya familia zimeamua kuachana na chai na kujikita kwenye uji.
Joshua Mang’ombe, mfanyabiashara wa Kishiri jijini Mwanza, alisema bidhaa hiyo imeadimika katika maduka ya jumla na amekuwa akielezwa kwamba imeagizwa nje Mwanza.
“Nahisi ni njama za kuihujumu Serikali ya Dk. John Magufuli,” alisema Mang’ombe.
Mamalishe anayefanya biashara zake katika eneo la Makoroboi kwa wauza nguo, Sabina Juma alisema amelazimika kuuza chai ya rangi Sh 200 kwa kikombe kutokana na kuadimika kwa sukari.
Akizungumza uhaba huo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, alisema tayari ameagiza maofisa wake kuchunguza hali hiyo kabla ya kuanza utekelezaji wa kuwafuatilia wafanyabiashara walioficha sukari.
KILIMANJARO
Katika mkoa wa Kilimanjaro, sukari inauzwa Sh 2,800 kwa kilo badala ya 1,800 ya awali pamoja na kuwapo kiwanda cha TPC kinachozalisha bidhaa hiyo mjini Moshi.
Akizungumza na MTANZANIA, Ofisa Utawala wa TPC, Jaffari Ally aliitupia lawama Serikali kupitia Kamati ya Ulinzi na Usalama chini ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla kwamba waliwalazimisha kusambaza katika mimkoa mingine tani 20,000 za akiba yao ambayo inatosheleza mahitaji ya Kanda ya Kaskazini.
“Hivi sasa hatuna sukari kabisa kwenye maghala baada ya kulazimishwa na Serikali kuisambza katika mikoa mingine tofauti na utaratibu wetu wa kuuza sukari katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Singida, Manyara na Tanga,” alisema.
Alisema hivi sasa wamesimamisha uzalishaji wa sukari katika utaratibu wao wa kawaida ambapo hufunga kiwanda mwezi Machi kila mwaka ili kupisha matengenezo.
ARUSHA
Mkoani Arusha sukari inauzwa kati ya Sh 2,500 na 2,800 kwa kilo moja katika maduka ya jumla, huku ikiuzwa kati ya Sh 3,000 na 3,500 katika maduka ya rejareja kutokana na bidhaa hiyo muhimu kuadimika.
Baadhi ya wasambazaji wanadai kubughudhiwa kila mara na maghala yao kupekuliwa na maofisa wa Serikali na vyombo vya dola wakidhaniwa kuwa huenda wanaficha bidhaa hiyo ili waiuze kwa bei kubwa.
KAGERA
Wananchi katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, wamelalamikia kupanda kwa bei ya sukari kutoka Sh 2,000 za awali na kufikia Sh 2,500 kwa kilo moja wakati sukari inatengenezwa mkoani humo.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na MTANZANIA jana, waliitaka Serikali ilinde kauli yake iliyotoa kwa wafanyabiashara kwamba sukari isiuzwe zaidi ya bei elekezi ya Sh 1,800 kwa kilo.
“Jamani Serikali iwatazame wafanyabiashara wanaojipangia bei maana tunaibiwa wanyonge, watoto wetu wamezoea kunywa chai au uji, sasa bei zikiwa juu tutaishia wapi?” alisema mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina moja la Hassan.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mstaafu Salim Kijuu, alizungumzia uhaba huo wa sukari, alisema unatokana na kusitishwa kwa uzalishaji ili kufanya marekebisho ya majengo ya Kiwanda cha Kagera.
DAR ES SALAAM
Mkoani Dar es Salaam sukari inauzwa kati ya Sh Sh 2,300 na 2,800 katika baadhi ya maeneo, huku bei elekezi ya Sh 1,800 iliyotangazwa na Serikali ikiwa haijawahi kutumika.
WAFANYABIASHARA
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Johnson Minja, alisema kuadimika kwa sukari nchini kunatokana na taarifa zisizokuwa sahihi kuhusu mahitaji halisi ya bidhaa hiyo kwa sasa.
“Mahitaji ya sukari kwa sasa ni tani 600,000 huku viwanda vya hapa nchini vikiwa na uwezo wa kuzalisha tani 300,000 tu.
“Si kweli kwamba upungufu ya sukari nchini ni tani 100,000, mahitaji halisi ya nchi ni tani 600,000 hivyo kunahitajika ongezeko la viwanda kama 10 ili tuweze kuzalisha tani zinazohitajika,” alisema Minja.
Aidha alisema kuadimika kwa bidhaa hiyo pamoja na sababu nyingine, pia kunatokana na kushindwa kuviendeleza viwanda vya ndani.
BODI YA SUKARI
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari nchini, Henry Simwanza, alipotakiwa kutolea ufafanuzi bei ya sukari kuongezeka, alisema kwa sasa yuko Dodoma bungeni na kuahidi kulizungumzia suala hilo wiki ijayo.
WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Adelhem Meru, alisema Bodi ya Sukari ndiyo inapaswa kuzungumzia uhaba huo wa sukari.
SUKARI BUNGENI
Sakata la kuadimika kwa sukari nchini limeibuka pia bungeni baada ya Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) kuomba mwongozo kwa Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson akilitaka Bunge lisitishe mjadala wa bajeti ya Wizara ya Kilimo na kujadili suala hilo kama dharura.
Bashe aliomba mwongozo huo jana bungeni baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu.
“Mheshimiwa Naibu Spika, bei ya sukari nchini inazidi kupanda juu na hali hii inawaumiza wananchi. Kutokana na hilo natumia kanuni ya 47 (1,2,3 na 4) ya kutaka kiti chako tusitishe mjadala wa bajeti ili tujadili hali ya sukari nchini kama suala la dharura,” alisema Bashe.
Akijibu hoja hiyo, Naibu Spika alisema: “Tayari suala hili limeshatolewa majibu na Waziri Mkuu wiki iliyopita, kilichobaki sasa Serikali ituambie suala hili limefikia wapi.”
KAULI YA WAZIRI MKUU
Jumatano iliyopita, Waziri Mkuu KassimMajaliwa wakati akifanya majumuisho ya bajeti ya ofisi yake ya makadirio ya fedha kwa mwaka 2016/17, aliwaagiza maofisa biashara nchini kuhakikisha wanafanya msako dhidi ya wafanyabiashara walioficha sukari na kusababisha bidhaa hiyo kuwa adimu.
Alisema kutokana na hilo, Serikali imeagiza sukari nje ya nchi kufidia iliyopungua nchini lengo likiwa ni kuzuia kuingiza sukari nyingi ambayo inadhoofisha viwanda vya ndani.
Habari hii imeandaliwa na Benjamini Masese (Mwanza), Ramadhan Libenanga (Morogoro), Oscar Assenga (Tanga), Renatha Kipaka, Elizabeth Hombo (Dodoma), Safina Sarwat, Mohamed Hamad, FLORIAN MASINDE (Dar) na Abraham Gwandu CArusha)