Na Pendo Fundisha, Mbeya
MBUNGE wa Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (Chadema) na Meya wa Jiji la Mbeya, David Mwashilindi, wamekatwa wakidaiwa kuingilia utendaji kazi wa Jeshi la Polisi.
Viongozi hao walikamatwa jana mchana wakishutumiwa kuwazuia polisi ambao walikuwa doria wakiongozwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mbeya (OCD), James Chacha.
Polisi hao waliwakamata vibaka waliokuwa wanalalamikiwa kwa ukwapuaji jijini Mbeya.
Viongozi hao walitiwa mbaroni walipokuwa wakiendelea na mkutano wa maendeleo katika eneo la Kabwe jijini hapa.
Polisi walipofika eneo hilo wananchi walitaharuki kwa hofu ya kukamatwa ndipo Sugu aliposimama na kuwataka kutokimbia akisema mkutano huo haukuwa wa siasa.
Mkutano huo ulikuwa unaratibiwa na Mbunge huyo, meya, Mkurugenzi wa Jiji na baadhi ya madiwani na ulikuwa na lengo la kuwaeleza wananchi kuhusu mkakati wa halmashauri hiyo wa kuboresha mazingira ya wafanyabiashara wadogo ‘Machinga’.
Wakati mkutano huo ukiendelea, ghafla walitokea polisi ambao baadhi yao walikuwa wakionekana kubeba mabomu ya machozi, silaha na gari la maji ya washawasha.
Walikuwa wakikamata watu ambao kwa mujibu wa jeshi hilo, walikuwa ni vibaka.
Kitendo hicho cha kukamata watu ovyo, kinadaiwa kuwa kiliwashangaza viongozi hao wa siasa pamoja na watendaji wa halmashauri.
Hali hiyo ilisababisha Mbunge huyo kuingilia kati na kuwataka wananchi wasikimbie, jambo lililozua taharuki kwa baadhi ya wananchi waliokuwa kwenye mkutano huo.
“Tunawaomba sana ndugu zetu askari msituingilie katika mkutano huu kwa sababu ni wa utendaji haupo kisiasa hivyo tunahitaji mtupe nafasi ili wananchi ambao ni wafanyabiashara wa eneo hili wafahamu nini halmashauri yao imewaandalia kabla ya kuwahamisha.
“… na hapa tunatekeleza agizo la Rais wa nchi ambaye ameaagiza kutosumbuliwa kwa wamachinga mpaka watakapotafutiwa maeneo ya kuwaweka,”alisema Sugu.
Baada ya kauli hiyo, baadhi ya askari walieleza kwamba walikuwa wametumwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashali, kwamba Meya na Mbunge Sugu wanahitajika katika ofisi yake.
Mbunge huyo akiwa ameongozana na Meya wa jiji na baadhi ya madiwani walitii agizo hilo na kwenda moja kwa moja katika ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya ambako walikuwa na mahojiano maalum yaliyochukua nusu saa na kabla ya kutakiwa kufika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.
Akizungumzia tukio hilo, Meya Mwashilindi, alisema walikuwa katika majukumu yao ya kazi lakini walishaangaa kuona askari wakiwahitaji yeye na mbunge Sugu kwa maelezo kwamba walikuwa wakihitajika katika ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya.
“Tulitii sheria lakini kwa masharti ya kutobughudhiwa wananchi, hivyo tulienda ofisini kwa kamanda na kumweleza lengo la mkutano huo ambako Kamanda alitutaka kwenda katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,” alisema.
Alisema wakiwa katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa, walieleza kilichokuwa kikiendelea na kuonekana kwamba tatizo lilikuwa ni kushindwa kuelewana kwa pande mbili hizo na baada ya muda waliachiwa.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda Kidavashali alisema jeshi hilo lilikuwa limejipanga kwa muda mrefu kudhibiti uhalifu katika eneo hilo ambalo limekuwa na matukio mengi ya uhalifu.