29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

SUGU, MASONGA KUANDIKA KERO GEREZA LA RUANDA

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM


KATIBU wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga, amesema anaandika kero zilizopo katika Gereza la Ruanda mkoani Mbeya na baadaye Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, atawasilisha bungeni kama hoja binafsi.

Mei 10 mwaka huu, Masonga na Sugu waliachiwa huru kutoka katika gereza hilo walikokuwa wakitumikia kifungo cha miezi mitano, baada ya kukutwa na kosa la kutumia lugha chafu dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.

Walitolewa kwa msamaha wa Rais alioutoa Aprili 26, mwaka huu baada ya kukidhi vigezo vya msamaha huo sawa na wafungwa wengine zaidi ya 3,000 waliopunguziwa robo ya vifungo vyao.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na MTANZANIA juzi, Masonga, aliyepata kugombea ubunge katika Jimbo la Njombe Mjini kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, alisema mambo waliyoyakuta katika gereza hilo si ya kawaida na kwamba watayapigia kelele.

“Hivi sasa tunaandika kero zilizopo katika Gereza la Ruanda kwa sababu nyingi tulizishuhudia nyingine tuliwahoji wafungwa. Sasa tukishakamilisha Sugu atawasilisha kama andiko rasmi bungeni ili dunia ijue kwamba haya ndiyo yanayotendeka gerezani,” alisema.

Miongoni mwa kero alizozitaja Masonga ni pamoja na kuvuliwa nguo wakati wa kukaguliwa jambo ambalo alisema ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

“Unapoingia gerezani kuna utamaduni wa ukaguzi, lakini sisi tulienda kuona utamaduni mpya wa namna ya kukagua mfungwa anapofika gerezani.

“Kitendo cha kumkagua mfungwa akabaki uchi hatukuona kama ni jambo la haki na tuliweza kumwambia mkuu wa gereza kwamba sisi ni viongozi na wala si wabakaji, hatujaua kwanini tufanyiwe hivi.

“Inapofika hatua unashindwa kunikagua kwa vifaa maalumu lakini ukanivua nguo, sisi kwetu tuliona ni udhalilishaji mkubwa na tukasema tutalizungumza hili ili utaratibu ubadilishwe kwa sababu ni kinyume na haki za binadamu.

“Teknolojia imekua ya watu kukaguliwa, ziko mashine maalumu ambazo zikipelekwa gerezani watazitumia kuwakagua wafungwa, lakini suala la kuanza kuvuana nguo hatukuona kama ni la kiungwana na ni kinyume kabisa na haki za binadamu, kwa hiyo suala hili tulilipinga na tutaendelea kulipinga kokote.

“Sisi hatukusimuliwa bali tumeshuhudia tena bora wanakuvua nguo lakini wanakwambia uiname, tulifanyiwa tena sehemu ambayo si faragha, unabaki kama ulivyotoka kwa mama yako.

“Kama sisi viongozi tunafanyiwa hivi je, hawa wafungwa wa kawaida inakuwaje. Serikali na magereza waliangalie hili, wengine wako pale amefungwa yeye na mtoto wake, anavuliwa nguo mbele ya mtoto wake, ni jambo ambalo si sawa,” alisema Masonga.

Pia alisema chakula imekuwa ni tatizo katika gereza hilo, kwani wanakula mlo mmoja kwa siku huku wakipimiwa kipimo kidogo sana.

Alisema huwa chakula ni ugali maharage, lakini siku walipofungwa wao alichinjwa ng’ombe jambo ambalo liliwashangaza hata wafungwa waliopo katika gereza hilo.

“Wanapata chakula kidogo gerezani hawashibi muda wa chakula inakuwa ni kama vita, manyapara wao ndio wanaopata mpaka watoto wanachanganywa mle ndiyo maana vitendo vya ulawiti gerezani haviishi kwa sababu mtu anaona bora alawitiwe ili apate chakula.

“Ndiyo maana wakati fulani Lema (Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema), alisema ni bora Serikali ikagawa condoms magerezani kwa sababu vitendo hivyo vipo.

“Siku sisi tulipoingia mle walichinja ng’ombe na wakawa wanapika wali. Sasa wale wafungwa wakawa wanatusimulia kuwa kwao ni maajabu kula nyama wakati haijapata kutokea kwa sababu kila siku wanakula ugali maharage,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles