30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Straika Mghana anukia Jangwani

NA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

KLABU ya soka ya Yanga imeanza mipango ya chini kwa chini ya kumwinda mshambuliaji kinda raia wa Ghana, Awudu Zakari, ambaye amemaliza mkataba wake wa kuichezea timu ya Nogoon El- Mstakbal, inayoshiriki Ligi Kuu nchini Misri.

Straika huyo mwenye umri wa miaka 20, alijiunga na Nogoon El- Mstakbal Januari mwaka jana, kwa mkataba wa mwaka mmoja na nusu akitokea timu ya Union Doula ya Cameroon, aliyoanza kuichezea tangu mwaka 2013 kama mchezaji wa kulipwa kwa mara ya kwanza.

Ili kuhakikisha inampata nyota wa kimataifa mwenye vigezo na sifa zinazokubalika, mabingwa hao watetezi wameanza kuchunguza baadhi ya video za mshambuliaji huyo ili kujiridhisha zaidi na uwezo wake.

Akizungumza na MTANZANIA jana kwa njia ya mtandao, Zakari alithibitisha kuwepo kwa mawasiliano kati yake na baadhi ya viongozi wa Yanga na kudai yupo tayari kujiunga na mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita katika dirisha la usajili msimu ujao.

“Namuomba Mungu mambo yaende vizuri ili niweze kutimiza ndoto za kuichezea Yanga, kwani sina mpango wa kuongeza mkataba na timu niliyokuwa nikiichezea kutokana na migogoro ya kisiasa ya mara kwa mara nchini Misri,” alisema Zakari.

Akizungumzia ushindani wa namba uliopo katika kikosi cha Yanga, Zakari alisema kama dili lake litafanikiwa yupo tayari kupambana ili aweze kucheza kikosi cha kwanza na kuisaidia timu hiyo kwa kuwa ana uwezo na kipaji cha kufanya hivyo.

“Siku zote mimi ni mpambanaji, ndiyo maana siogopi kupigana kuhakikisha napata namba ya kucheza, ingawa siwajui wachezaji wote wanaoichezea timu hiyo.

“Mchezaji ambaye ninamfahamu vizuri kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara ni mshambualiaji Hamis Kiiza, raia wa Uganda niliyewahi kupata bahati ya kucheza naye katika timu ya Nogoon El Mstakbal,” alisema.

Straika huyo alieleza kuwa bado hajaanza rasmi mazungumzo na uongozi wa Yanga, licha ya kuwepo kwa mawasiliano ya karibu na baadhi viongozi.

Ikiwa dili ya mchezaji huyo itafanikiwa kwa msimu ujao, atakuwa ameongeza ushindani katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ambayo kwa sasa inaongozwa na Amissi Tambwe, Donald Ngoma na Simon Msuva.

Tambwe anaongoza katika kinyang’anyiro cha kuwania kiatu cha dhahabu msimu huu ambapo tayari amepachika wavuni mabao 13, huku Ngoma akifunga tisa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles