KOCHA Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, amesema amefurahishwa na kiwango cha timu hiyo kilichoonyeshwa wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City uliofanyika katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Katika mchezo huo, Azam walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya wenyeji wao Mbeya City, ambapo kocha huyo alidai kuwa pambano hilo ni sehemu ya maandalizi yao kabla ya kuivaa Tanzania Prisons keshokutwa.
Akizungumza baada ya mchezo wa juzi, Hall alisema wachezaji wake walionyesha kiwango safi baada ya kufanyia kazi udhaifu uliojitokeza katika mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union kwa kushindwa kuutendea haki mfumo wa 3-5-2 wanaoutumia.
“Tulijitahidi kufanya mazoezi ili kurudi katika kiwango chetu cha kawaida na jitihada zetu zilionekana kuanzia dakika ya 15 na kuendelea kwani wachezaji walianza kujiamini na kusahau matokeo ya mchezo uliopita.
“Tulifanya mabadiliko ya kipindi cha pili ili kuongeza mbinu zaidi, tulimpeleka Messi (Ramadhan Singano) katikati na kumchezesha Farid (Mussa) upande wa kushoto aliyeingia kuchukua nafasi ya Mudathir Yahya,” alisema.
Mwingereza huyo alisema siku zote huwa hawaamini waamuzi jambo linalomfanya ampumzishe dakika 25 za mwisho, Himid Mao na kumwingiza Frank Domayo kutokana na kiungo huyo mkabaji kuonyeshwa kadi ya njano kipindi cha kwanza.
Hall alisema wamepania kuendeleza wimbi la ushindi katika mchezo ujao dhidi ya maafande wa Prisons licha ya kukiri kuwa pambano hilo litakuwa la ushindani mkubwa.
“Itakuwa ni mechi ngumu na siku zote mechi za nje ni ngumu, hivyo tunatakiwa kuendeleza ushindi, tumefarijika kwani kushinda mabao 3-0 ugenini ni matokeo mazuri ndiyo maana tunatakiwa kuendelea katika hali hiyo ya kujiamini,” alisema.