MANCHESTER, England
MTANDAO wa Sun umefichua kuwa Manchester City wanaangalia uwezekano wa kumpa mkataba mpya winga, Raheem Sterling ambao utamfanya awe anavuna kitita cha pauni 300,000 (zaidi ya Sh milioni 650) kwa wiki.
Hayo ni maelekezo ya Pep Guardiola ambaye anataka kuona mchezaji huyo akibaki kwenye kikosi hicho, hata kwa kiasi hicho cha fedha ambacho kitamfanya kuwa mchezaji anayelipwa mshahara mnono zaidi Ligi Kuu England.
Kama mambo yatakwenda vizuri katika mazungumzo ya mkataba huo, basi Sterling mwenye umri wa miaka 22 atampiku hata staa wa Manchester United, Paul Pogba ambaye anakinga pauni 290,000 (Sh milioni 638) kwa wiki.
Man City wanataka kumpa mkataba mpya licha ya kwamba nyota huyo wa kimataifa wa England amebakisha miaka miwili katika ule aliosaini wakati anatua klabuni hapo akitokea Liverpool.
Inasemekana kuwa kutokana na mkataba wake wa kwanza wa miaka mitano aliosaini mwaka 2015, nyota huyo anapokea si zaidi ya pauni 180,000.
Sterling amekuwa kwenye kiwango kizuri msimu huu kwani bao lake katika mchezo dhidi ya Southampton lilikuwa la 13.
“Alicheza vizuri, ndiyo maana Man City walitoa fedha nyingi kumsajili. Sifa zote ziende kwake,” alisema Guardiola baada ya mchezo huo.
Wakati wa dirisha la usajili la majira ya kiangazi, nyota huyo alikaribia kuondoka Etihad, hasa baada ya Man City kuipelekea Arsenal ofa ya pauni milioni 60 kwa ajili ya Alexis Sanchez.
Kwa upande wake, Kocha wa Gunners, Arsene Wenger, aliitaka Man City kutoa kiasi hicho cha fedha pamoja na kumruhusu Sterling aelekee Emirates, kitu ambacho hakikumwingia akilini Guardiola.