NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
UBUTU wa safu ya ushambuliaji ya Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, umempa somo kocha Mkuu wa Yanga, Mbrazil Marcio Maximo, kuiondoa hali hiyo kwenye kikosi chake msimu ujao wa ligi kuu Tanzania Bara.
Stars katika mechi yake dhidi ya Msumbiji juzi, ilishindwa kutumia nafasi nyingi za kufunga mabao walizozipata na hatimaye kuishia kutoka sare ya 2-2, hali iliyowapa unyonge mashabiki kwa kiasi kikubwa.
Maximo alijumuika na mashabiki wengine kuishangilia timu hiyo, aliingia uwanjani huku akionyesha vidole viwili ikiwa ni ishara ya mabao mawili, ambayo Stars pia waliweza kuyafunga licha ya kurudishwa na wapinzani na kutoka sare.
Katika mazoezi ya jana ya Yanga Uwanja wa Shule ya Loyola, Maximo alianza kwa kuwapigisha jaramba wachezaji wake kwa dakika 38, aliwakimbiza kuzunguka uwanja kwa kasi sana na polepole na baadaye kuwaingiza uwanjani.
Baada ya hapo, Maximo alianza kwa kuwapanga wachezaji kupiga mpira haraka golini bila kupiga chenga, pindi anapopewa pasi na wenzake ambapo ni mapungufu yaliyoonekana jana kwa timu ya Taifa na kusababisha kukosa kutumia ipasavyo nafasi hizo.
Wachezaji walionekana kuwa wepesi kuyamudu mazoezi hayo ya Maximo, huku wachezaji Said Bahanuzi na Andrey Coutinho wakifunga mabao ya kiufundi, mbele ya kipa namba moja wa timu hiyo Juma Kaseja.
Baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo, Maximo aliwapa mazoezi ya viungo na kumaliza programu yake ya jana.