NA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM
KIKOSI cha timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kimeondoka nchini jana alfajiri kuelekea jijini Algiers huku kikiwa na matumaini ya kufanya vizuri na kuwatoa wapinzani wao Algeria ‘The Desert Foxes’ ugenini.
Stars iliyolazimishwa sare ya mabao 2-2 nyumbani, itarudiana na Algeria kwenye Uwanja wa Stade Mustapha Tchaker jijini Algiers kesho katika mchezo wa raundi ya pili kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi.
Kocha Mkuu wa Stars, Charles Mkwasa, amesema kuwa wachezaji wake watakwenda kucheza mchezo ugenini kama walivyocheza mchezo wa kwanza na anaamini wanaweza kupata mabao ugenini.
“Tuna matarajio mazuri kuelekea mchezo wa ugenini, naamini wachezaji wangu watacheza mchezo mzuri kama waliouonyesha hapa leo (juzi) naamini Mungu akipenda tutapata matokeo mazuri ugenini, tumewaona wanavyocheza hawatishi sana,” alisema.
Akizungumzia mchezo uliopita, Mkwasa alisema mabadiliko aliyofanya kipindi cha pili ya kuwaingiza Mrisho Ngassa, Said Ndemla na kuwatoa Elias Maguli na Mudathir Yahya ndiyo yaliharibu mchezo huo na kuwapa nafasi wapinzani wao kurudisha mabao.
“Leo (juzi) ilikuwa ni mechi yetu 100% ya kushinda, tumetengeneza nafasi nyingi hasa kipindi cha kwanza, lakini tumeshindwa kuzitumia tumepata mabao mawili na kuna muda tulikosa umakini baada ya mabadiliko na wakaweza kurudisha mabao yote. Vijana wamepambana wamehangaika kutafuta mabao kutokana na nafasi zilizopatikana na Algeria wana bahati sana,” alisema.
Naye nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, alisema matokeo waliyopata si mazuri sana na kudai kuwa wana nafasi nzuri ya kurekebisha makosa yao ugenini.
“Matokeo si mazuri ni magumu kwa upande wetu, ni kama tunapanda mlima mrefu ambao ni mkubwa sana, ila kwenye mpira lolote linaweza kutokea, tumejipanga kufanya vizuri na bado tuna nafasi kwani tukipata ushindi wa bao moja tunaweza kusonga mbele, matatizo tuliyoyapata madogo madogo kocha atayatatua kabla ya mchezo huo na sisi kufanya vizuri,” alisema.
Zitto Kabwe anena
Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, ni mmoja wa Watanzania waliohuzunishwa na matokeo hayo, ambaye amesema kuwa Stars ni timu nzuri na makosa madogo madogo ndiyo yamechangia matokeo hayo.
“Cha msingi ni kujipanga kwa ajili ya mchezo ujao, timu ni nzuri kama mlivyoiona, imejitahidi sana na mabao tuliyofungwa ni ya bahati mbaya sana, kama wao wamedraw (sare) kwetu na sisi tunaweza kushinda kwao, naamini kulikuwa na matatizo kwenye mabadiliko na makocha watafanyia kazi kwenye hilo,” alisema.
Kabwe alisema timu inaweza kufanya vizuri ugenini hasa ikijua kama nchi bado ipo nyuma yao, hivyo akawaomba Watanzania watakaoweza kwenda nchini Algeria wafanye hivyo ili kuishangilia timu hiyo.
Taifa Stars ili isonge mbele kwa kuitoa Algeria, inatakiwa kupata ushindi wowote au sare ya kuanzia mabao matatu na mshindi wa jumla atafuzu kwa hatua ya makundi itakayohusisha timu 20 na bingwa wa kila kundi atafuzu kwa fainali za michuano hiyo.