22.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Spika wa Bunge Marekani amtetea Hillary Clinton

Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Democrat, Hillay Clinton
Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Democrat, Hillay Clinton

NA JUSTIN DAMIAN, NORTH CAROLINA

SPIKA wa Bunge la Wawakilishi la Marekani, Paul Ryan, amemtetea mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Democrat, Hillay Clinton, dhidi ya kashfa mpya ya matumizi ya barua pepe binafsi kwa shughuli za kiserikali.

Mwishoni mwa wiki, Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI), lilinasa mawasiliano mapya ya barua pepe binafsi ambayo Clinton aliyafanya wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Nje.

Mkurugenzi wa FBI, James Comey, aliliandikia Bunge la  Wawakilishi na kulieleza kuwa, shirika lake linafanyia uchunguzi wa mawasiliano hayo mapya.

Kashfa hii ni ya pili baada ya ile ya  Julai mwaka huu, ambayo haikuwa na ushahidi wa kutosha kumweka mgombea huyo hatiani. Hata hivyo, Comey alisema hawezi kusema ni  lini uchunguzi wa suala hilo utakamilika.

Uchunguzi huu mpya unafuatia kukamatwa vifaa vya mawasiliano vya mjumbe wa bunge hilo, Anthony Weiner pamoja na mke wake, Huma Abedin, ambaye ni msaidizi wa karibu wa kampeni za Clinton wakati FBI  wakimchunguza mume wa Abedin kwa tuhuma za kuwa na uhusiano wa kimapenzi na binti wa miaka 15.

Abedin na mumewe waliachana Agosti mwaka huu, baada ya gazeti la The New York Post kuchapisha habari kuwa Weiner alikuwa akimtumia picha na ujumbe wa kimapenzi binti huyo kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Mamia ya ujumbe kupitia barua pepe ambazo Clinton alikuwa akimtumia msaidizi wake huyo kipindi akiwa waziri, zimenaswa na FBI katika chombo cha kuhifadhia kumbukumbu (server) ambacho msaidizi huyo alikuwa akikitumia pamoja na mume wake.

Lakini katika hali isiyo ya kawaida, Ryan amenukuliwa na vyombo vya habari vya hapa Marekani akimtaka Mkurugenzi  wa FBI kuacha kutoa taarifa kwa umma juu ya suala hilo kwa kuwa ni nyeti na zinatakiwa kufanyiwa kazi kwa siri.

Tamko la Ryan linachukuliwa kama utetezi kwa Clinton, ikiwa imebaki wiki moja Wamarekani kupiga kura, huku chama cha spika huyo kikiwa kimegawanyika kutokana na mgombea wao, Donald Trump, kutoa kauli zenye utata.

Akizungumza katika moja ya mikutano yake ya kampeni, Hillary hakusema chochote kuhusu tuhuma hizo mpya ambazo zinaweza kubadilisha upepo.

Lakini mwenyekiti wa timu ya kampeni ya Hillary, John Podesta, alimtaka Mkurugenzi wa FBI kutoa ufafanuzi kwa umma juu ya suala hilo

“Ni jambo la kushangaza kuona jambo kama hili linatokea siku 11 tu kabla ya uchaguzi. Mkurugenzi wa FBI awaambie Wamarekani haraka anachunguza nini. Tunaamini suala hili litakuwa na mwisho mzuri kama lile la Julai,” alisema.

Akihutubia katika moja ya mikutano yake, mpinzani wa Hillary, Donald Trump , alisema suala hilo haliwezi kumwacha salama.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa hapa Marekani, wameitupia shutuma FBI kwa namna ambavyo imekuwa ikilishughulikia suala hilo na wameonyesha wasiwasi wao juu ya siasa kuingia ndani yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles