NA ABRAHAM GWANDU, ARUSHA,
SPIKA wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Margreth Zziwa, jana ameng’olewa kushika wadhifa huo baada ya wabunge 36 kati ya 49 kupiga kura za ndiyo kutokuwa na imani naye kutokana na kile kilichoelezwa ameshindwa kuongoza Bunge hilo.
Kabla ya kufikia uamuzi wa kupiga kura, Kamati ya Bunge ya Sheria, Hadhi na Madaraka ya Bunge hilo ilipewa jukumu la kuchunguza tuhuma kadhaa zilizokuwa zikimkabili ikiwamo kuwapendelea baadhi ya wabunge, kushindwa kufuata kanuni zinazoongoza Bunge na kutumia madaraka yake vibaya.
Kamati hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Mwenyekiti wake Frederick Ngenzebuhoro kutoka nchini Rwanda, iliundwa kutokana na hoja iliyowasilishwa awali na Mbunge Peter Mathuki wa Kenya ya kulitaka Bunge hilo kukubali ombi la kumfukuza Spika Zziwa kwa kile alichodaiwa amekuwa akiwagawa wabunge hali inayotishia kuivunja Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Akiwasilisha taarifa ya uchunguzi wa kamati yake, Ngezebuhoro alisema hatua aliyofikia Zziwa alikuwa hastahili tena kuwa kiongozi wa chombo hicho muhimu kwa wanajumuiya ya Afrika ya Mashariki.
“Ilifika hatua mbaya sana kwa wajumbe hata chai tulishindwa kunywa pamoja, alipendelea wabunge, alitugawa wabunge na aliwapa fursa wanafamilia wake kutumia rasilimali za jumuiya kinyume na makubaliano ya kuundwa kwa EAC.
“Kupitia ushahidi wa picha za video, nakala za magazeti na vyombo mbalimbali vya habari, hatuna shaka kwamba alipitiliza kutumia madaraka yake vibaya hivyo hafai kuwa kiongozi,” alisema Ngezebuhoro.
Wakichangia hoja hiyo, wabunge Twaha Taslima wa Tanzania, Nyiramiro Odete kutoka Rwanda na Hafsa Mosi wa Burundi waliunga mkono hoja hiyo kwa kile walichosema kuwa spika huyo alikuwa dhaifu na hakuwa na uwezo wa kulisukuma mbele gurudumu la wanajumuiya ya Afrika Mashariki.
Wabunge waliohudhuria kikao kilichotoa uamuzi huo walikuwa 39 ambao kati yao Watanzania walikuwa watano, Kenya (8), Uganda (8), Rwanda (9) na Burundi walikuwa 9.
Idadi ya wabunge waliopiga kura ya ndiyo kumng’oa Spika Zziwa ilikuwa 36, kura za hapana mbili na kura moja iliharibika na hivyo kupitishwa kwa azimio la kumwondoa Spika huyo katika wadhifa wake na kuruhusu Uganda kupeleka jina la mtu mwingine kujaza nafasi hiyo katika kipindi kifupi kijacho.
Wabunge Shyrose Bhanji, Mariam Ussi, Makongoro Nyerere na Adamu Kimbisa kutoka Tanzania hawakuhudhuria kikao hicho.
Awali asubuhi ya jana Zziwa kupitia Mwanasheria wake, Jet John Tumwebaze wa Kampala Associated Advocates, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa kikao kinachofanyika ni kinyume cha sheria na uamuzi wowote utakaofikiwa ataupinga katika Mahakama ya Afrika ya Mashariki.
Juzi mahakama hiyo ilitupilia mbali zuio la shughuli za EALA kwa madai kuwa mahakama haina mamlaka ya kuingilia muhimili mwingine wa jumuiya.