Na FERDINANDA MBAMILA,
ASASI isiyo ya kiserikali ya Children’s Village (SOS) ni ya kimataifa ambayo hujishughulisha na masuala ya malezi ya watoto. Walengwa wakuu ni watoto waishio katika mazingira magumu au yatima.
Asasi hii duniani ilianzishwa mwaka 1949 ikiwa chini ya mwanzilishi wake Helmanhn Gmeiner, ambaye alianzisha taasisi hii baada ya kuona hali ya watoto duniani ilivyokuwa mara baada ya kumalizika kwa Vita Kuu ya pili ya Dunia.
Kwa Tanzania asasi hii inaitwa SOS Children’s Village – Tanzania; ambapo ilianza rasmi mwaka 1991, baada ya Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi kuona kwamba kuna umuhimu wa kuwa na huduma ya aina hii nchini. Kwa mara ya kwanza, SOS Children’s Village Tanzania ilianza shuguli zake kwa kujenga kituo cha watoto Zanzibar ambapo vinapatikana katika visiwa vya Pemba na Unguja. Ikifuatiwa na Dar es Salaam, Arusha na Mwanza wilayani Nyamagana, ambapo hivi vinaitwa vijiji vya watoto. Mkoani Iringa vipo Iringa Mjini na katika Wilaya ya Mufindi.
Mratibu wa Masuala ya Ushawishi SOS, Grace Matui anataja miongoni mwa kazi wanazofanya kuwa ni pamoja na kutoa na kusimamia malezi bora ya watoto, kusimamia ulinzi na usalama wa mtoto kwa ujumla.
Anasema kuwa kazi hizo hufanywa katika programu tofauti wakianzia katika vijiji vya watoto Unguja. Ikifuatiwa na Dar es Salaam, Arusha na Mwanza.
Pia wana mradi wa kuelimisha familia unaofanywa katika jamii moja kwa moja nje ya vijiji. Anatoa mfano wa mradi unaoendelea katika Kata ya Chanika, Manispaa ya Ilala jijini hapa.
“Kupitia programu hizi tumekuwa na miradi inayohusu elimu, afya, masuala ya jinsi na jinsia kwa watoto, pia miradi ya kujenga uwezo wa kipato kwa familia.
“Mbali na vijiji, SOS Children’s Village inaendesha huduma za shule kuanzia awali mpaka sekondari na huduma za afya kwa watoto na jamii,” anasema Matui.
Anasema kuwa mpaka sasa hapa nchini wanahudumia watoto 5,000 wakiwamo watoto waliopo katika vijiji vya watoto kama kile cha Ubungo Mawasiliano jijini Dar es Salaam.
Anasema kwa watoto walio vituoni, SOS huwa inatoa mafunzo maalumu kwa kina mama, ambao huajiriwa rasmi na asasi kama walezi wa kuduma wa watoto walio vituoni.
Anasema kwa kuwa lengo ni kuwatunza vema watoto hao, SOS huhakikisha kuwa walezi wanaowaajiri ni wale wenye roho ya huruma na kujitolea, ili wasione tofauti ya kuishi bila wazazi.
Anabainisha kuwa kila kituo kina watoto wasiopungua 150 isipokuwa kituo kipya cha Mwanza ambapo watoto hao hupatikana kupitia idara husika za Serikali, hasa ya Ustawi wa Jamii.
“Lengo letu ni kufikia watoto wengi zaidi waishio katika mazingira magumu ambao takwimu zinaonyesha kuwa wapo zaidi ya milioni nne kwa nchi nzima. Hii ni kupitia miradi ya ushawishi na utetezi, inayolenga masuala ya uboreshwaji wa Sera na Sheria za Kitaifa zinazomuhusu mtoto.
“Agenda yetu kuu ni kuwa na ongezeko la bajeti inayomuhusu mtoto hasa anayeishi katika mazingira magumu. Bajeti hii pamoja na mambo mengine iangalie watekelezaji wa mikakati ya mtoto hasa katika ngazi za chini, wakiwamo maafisa wa ustawi wa jamii –wasaidizi ili kuona kamati zinazohusu ulinzi na usalama wa mtoto zikifanya kazi kama ilivyokusudiwa,” anasema Matui.
Anaongeza kuwa uwapo wa asaisi hii umesaidia watoto wengi kutorandaranda mitaani na hivyo kuepuka kufanyiwa vitendo vya kikatili kama kubakwa na mambo mengine.