27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

‘VISIMA PEKEE NDIO VITAMALIZA SHIDA YA MAJI TEMEKE’

Na MWANDISHI WETU,

MOJA ya changamoto kubwa zinazoukabili Mkoa wa Dar es Salaam ni pamoja na ukosefu wa maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, viwandani na sehemu nyingine zinazotoa huduma mbalimbali kwa wananchi.

Kulingana na sensa ya mwaka 2012, Jiji la Dar es Salaam linakadiriwa kuwa na wakazi wapatao milioni 4.3 ambao hupata huduma ya maji kutoka katika vyanzo vya Mto Ruvu, Kizinga pamoja na maji chini ya ardhi.

Takwimu zinaonesha kuwa, mahitaji ya maji kwa wakazi wa mkoa huo na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Pwani ni wastani wa lita milioni 450 kwa siku ambapo uwezo wa uzalishaji ni lita milioni 388 kwa siku.

Kwa upande wa uzalishaji wa maji, takwimu zinaonesha kuwa maji yanayozalishwa yanakidhi mahitaji kwa asilimia 56.5 kwa wastani wa saa nane kwa siku.

Eneo kubwa linalopata maji linahudumiwa na Shirika la Maji safi na Maji taka Dar es Salaam (Dawasco) ambayo imepewa mkataba na Mamlaka ya Maji Safi na Maji taka Dar es Salaam, (DAWASA).  Maeneo yasiyo na mtandao wa DAWASA hupata maji kutoka visima vinavyoendeshwa na vyombo vya watumia maji, taasisi na watu binafsi.

Hadi kufikia Septemba mwaka jana, visima virefu 676 vya jamii vilijengwa katika Mkoa wa Dar es Salaam, ambapo Ilala ni visima 316, Temeke 231 na Kinondoni 129.

Kadhalika kuna visima vya taasisi na watu binafsi visivyopungua 600 katika maeneo mbalimbali ya mkoa. Maji yanayozalishwa na visima vya taasisi na watu binafsi yanafikia lita za ujazo milioni 53 kwa siku ambapo yanakidhi mahitaji kwa asilimia 16.2 tu ya wakazi wote wa jiji hilo.

Takribani asilimia 40 ya eneo la Dar es Salaam, hakuna mtandao wa mabomba kutokana na uwekezaji mdogo, hivyo kulazimika kutumia visima kama vyanzo vikuu vya huduma ya maji.

Wilaya ya Temeke ndiyo yenye kiwango cha chini (asilimia 10) cha upatikanaji wa mtandao wa bomba kutokana na kuwa mbali na mtandao wa maji kutoka Ruvu, pia maeneo mengi ni mapya yakiwa ni makazi holela yasiyopimwa na yaliyo pembezoni.

Hata hivyo, matarajio ya mkoa huo ni kutoa huduma ya majisafi na salama kwa asilimia 95 kwa wakazi wa jiji na asilimia 30 kwa uondoshaji wa majitaka hadi ifikapo Desemba 2019/20.

Juhudi za uongozi wa mkoa huo ili kuhakikisha kuwa tatizo la maji linapatiwa ufumbuzi, limekuwa likiungwa mkono na Kampuni ya Bia ya Serengeti Breweries Limited (SBL) ya jijini Dar es Salaam.

Hospitali ya Temeke iliyopo jijini Dar es Salaam, ni kati ya hospitali zinazopokea wagonjwa kwa kiasi kikubwa, kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo. Kuna kila sababu ya sekta husika kuweka mazingira mazuri yenye kulenga huduma bora kwa wagonjwa ikiwamo upatikanaji wa maji safi na salama.

Kampuni ya SBL, kati ya mambo iliyoyafanya katika manispaa hiyo, ni pamoja na kujenga visima vyenye ujazo mkubwa kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la maji katika hospitali hiyo. Visima hivyo kwa sasa vyenye uwezo wa kubeba lita 38,000 za maji vimekuwa msaada mkubwa kwa wagonjwa wanaopata huduma hospitalini hapo, tangu vilipojengwa miaka minne iliyopita.

“Huu ni msaada ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa kwa sababu kati ya wilaya za Dar es Salaam, Temeke tunapata shida ya maji ikilinganishwa na nyingine kutokana na sababu za kijiografia. Kwa upande wa hapa hospitali, Serengeti wamefanya la maana mno,” anasema Mwajuma Issa, mkazi wa Temeke aambaye mwanawe amelazwa hospitalini hapo.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa SBL, John Wanyancha anasema kampuni hiyo itaendelea kusaidia jamii na hasa katika mahitaji muhimu, kama sehemu ya majukumu yao.

“Tunafurahi kuona kuwa wananchi wanafurahia kile tunachokifanya, lakini pia huu ni mwendelezo wa mpango wetu wa kusaidia jamii katika mahitaji muhimu,” anasema Wanyancha.

Wanyancha anafafanua kuwa kupitia programu yake inayofahamika kama Maji kwa Uhai, SBL imechimba visima vya kisasa 16 katika mikoa nane na kuwezesha jamii katika maeneo hayo kupata maji safi na salama, lakini yenye uhakika.

“SBL imewapatia Watanzania zaidi ya milioni mbili kote nchini maji safi na salama bure katika kipindi cha miaka sita iliyopita kupitia programu ya hisani ya kusaidia jamii inayoendeshwa na kampuni hiyo inayolenga kuboresha maisha,” anasema Wanyancha.

Kwa mujibu wa Wanyancha, mpango uliopo kwa sasa kwa mwaka 2017 kupitia programu hiyo ya Maji Kwa Uhai ni kuanzisha miradi zaidi katika maeneo ya Ngare Nairobi, (Wilaya ya Siha), Chang’ombe B (Temeke), Karatu na Likamba mkoani Arusha ambapo miradi yote itawanufaisha wakazi zaidi ya 300,000.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles