27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

SOPHIA SIMBA AFUNGUKA

Na Bakari Kimwanga-DAR ES SALAAM


ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Sophia Simba, amevunja ukimya na kusema amepokea adhabu aliyopewa na chama chake kwa moyo mkunjufu.

Kutokana na hali hiyo, amesema hana mpango wa kujiunga na chama chochote cha siasa, kwani ataendelea kubaki kuwa mkereketwa wa chama hicho tawala.

Sophia alitoa kauli hiyo jana katika mahojiano maalumu na MTANZANIA yaliyofanyika  nyumbani kwake jijini Dar es Salaam.

Alisema kwa takribani miaka 46 amekuwa mwanachama mwaminifu wa CCM, hivyo haoni sababu ya kukiacha chama hicho.

Akizungumza kwa kujiamini, Sofia alisema alijiunga na Chama cha TANU mwaka 1971, wakati huo akiwa Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) na Katibu wa UWT Tawi la NDC nafasi ambayo alidumu nayo hadi mwaka 1979.

Baadaye mwaka 1977 alijiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kuzaliwa kwake.

Adhabu dhidi yake

MTANZANIA ilipotaka kujua namna alivyopokea adhabu hiyo na majaliwa yake ya baadaye, Sophia alisema amepokea uamuzi huo kwa mikono miwili kwani adhabu aliyopewa ni halali kwake, ingawa katika maisha yake ya kisiasa hakuwahi kukisaliti chama chake.

“Kwanza una bahati msimamo wangu ni kutozungumza na waandishi wa habari ila kwa kuwa ni wewe haya… Kuhusu adhabu ya chama binafsi nimeipokea kwa mikono miwili na sina kinyongo na uamuzi wa chama changu hata kidogo.

“Ninajua wapo waliozusha, eti  baada ya uamuzi wa Dodoma  nimekwenda kukutana na mwanasiasa mmoja wa upinzani, taarifa hizi  si za kweli na sitofanya hivyo. Nimetoka Dodoma na kurejea hapa nyumbani kwangu Dar es Salaam nimepokewa na watoto wangu, ndugu na marafiki zangu.

“Napenda kuwaeleza Watanzania wote, wafahamu sina mpango wa kujiunga na chama chochote cha upinzani. Na unajua CCM ina makundi mawili, la kwanza ni wanachama wenye kadi na la pili wakereketwa ambao ni wengi nami nitaingia katika kundi hilo na si kuhama,” alisema Sophia.

Alisema kwa miaka yake ya sasa, ikiwamo uzee hana muda wa kuhangaika katika vyama kwa sababu ujana wake wote ameumalizia ndani ya CCM.

Kwenda mahakamani

MTANZANIA ilipomuuliza kama ana mpango wowote wa kwenda mahakamani kupigania uanachama wake kupinga adhabu aliyopewa, Sophia  alisema hana mpango wa kwenda mahakamani kwa sababu kila taasisi huwa na utaratibu wake na si vinginevyo.

“Moyo wangu, maisha yangu yote ya ujana nimetokana na CCM, suala la kwenda mahakamani kupinga uamuzi wa chama kwangu halipo na sina nia hiyo hata kidogo, chama kupitia mwenyekiti wetu, Rais Dk. John Magufuli kimechukua hatua kwa wema na fadhila zote nilizopewa bado niende mahakamani?

“… nasema tena hili kwangu hapana sitofanya hivyo unaweza kwenda mahakamani halafu iwe nini, maisha yangu yote yametokana na CCM na leo kwenda mahakamani ni kukosa fadhila nilizozipata ndani ya chama.

“Kama suala ni ubunge wa viti maalumu kinachopanga nani awe mbunge ni chama ambacho pia kinaweza kusema hapana …msimamo wangu naheshimu uamuzi  halali ya chama,” alisema Sophia.

Alisema pamoja na mtihani uliomkuta bado ataendelea kuenzi na kutambua mchango mkubwa wa chama hicho  katika maisha yake yote ya ujana hadi utu uzima kwa sasa.

Ajivunia marais watatu

Alisema kutokana na uwezo aliopewa na Mwenyezi mungu, amepata bahati ya kufanyakazi na marais watatu kwa nyakati tofauti ambapo kila mmoja amefanya kazi nzuri ya kukijenga CCM.

“Usipoweza kumshukuru Mwenyezimungu huwezi kumshukuru  yeyote, mwanangu mimi nina bahati ya pekee nimejaaliwa kufanyakazi kwa karibu na marais watatu, Rais mstaafu Benjamin Mkapa kama mbunge.

“… na si hivyo tu kufikia mwaka 2005 hadi 2015 nimefanyakazi na Rais mstaafu Jakaya Kikwete na mwaka 2015 hadi sasa 2017, nimefanyakazi na mwenyekiti wetu wa chama, Rais Magufuli ambao wote kwa nyakati tofauti, wamekuwa viongozi wangu,” alisema.

Sophia, alisema wakati wote anamshukuru Mungu kwa kumjalia neema hiyo ya kufanyakazi na viongozi hao ambao wakati wote walikuwa msaada kwake.

Usaliti

Alisema pamoja na kupewa adhabu ikiwamo kufanya usaliti kwa chama, hivi sasa hawezi zungumzia suala hilo ila nafsi yake imekuwa ikijua ukweli namna alivyo mwaminifu.

“Sitaki kuzungumzia kwa undani suala la usaliti ila kwa kifupi, Mungu anaishuhudia nafsi yake jamani hivi kweli nikisaliti chama changu ambacho kimenilea katika maisha yangu yote.

“Sitaki kusema hili ila kikubwa ninaomba umma na wana CCM wote watambue nimepokea adhabu kwa mikono miwili na sina kinyongo chochote,” alisema.

Mitandao ya kijamii

Aliwaomba Watanzania kuitumia mitandao ya kijamii kwa faida hasi na si vinginevyo, ikiwamo kumwekea maneno mdomoni.

“Ninawaomba Watanzania wenzangu tuitumia mitandao ya kijamii kwa faida maana hivi sasa kila jambo limekuwa likizushwa ikiwemo kuwekewa maneno kinywani si jambo zuri ndugu zangu,” alisema.

Nafasi alizoshika

Sophia Simba, amekuwa Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto sambamba na kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ambapo kwa nafasi yake pia, alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) na Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC).

Waliofukuzwa

Machi 11, mwaka huu, CCM ilitangaza kuwafukuza wanachama wake 12, akiwamo Sophia ambaye wiki iliyopita alitangaza kutogombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi wa ndani ya chama hicho unaofanyika mwaka huu.

Wengine ni wenyeviti wa mikoa ambao ni Jesca Msambatavangu (Iringa), Erasto Kwilasa (Shinyanga), Ramadhan Madabiba (Dar es Salaam) na Christopher Sanya (Mara).

Wengine ni Willfred ole Mollel ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha Mjini, mjumbe wa NEC wa Wilaya ya Babati Mjini, Ally Sumaye na Mathias Manga wa Wilaya ya Arumeru.

Katika orodha hiyo, pia wamo wenyeviti wa wilaya ambao ni Omari Awadhi (Gairo), Ally Msuya (Babati Mjini), Makolo Laizer (Longido) na Salumu Madenge (Kinondoni-Dar es Salaam).

Wanachama wengine waliochukuliwa hatua baada ya kufanya makosa kama hayo ni Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi ambaye amepewa onyo kali na anatakiwa kuomba radhi.

Wakati Nchimbi akipewa onyo hilo, Adam Kimbisa ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma na Mbunge wa Afrika Mashariki alisamehewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles