Manchester, England
KOCHA wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer, ameweka wazi kuwa, anahofia kufukuzwa kasi baada ya uongozi wa timu hiyo kushindwa kutimiza matakwa yake wakati wa dirisha dogo la usajili wa Januari.
Solskjaer amedai kabla ya kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili, aliutaka uongozi huo kuweka mezani kitita cha fedha ambacho kitaweza kusajili wachezaji wanne ambao wangeweza kuboresha kikosi.
Manchester United ikatenga kitita cha kusajili wachezaji wawili ambao ni kiungo kutoka Sporting, Bruno Fernandes, aliyejiunga kwa kitita cha pauni milioni 48, pamoja na kumsajili mshambuliaji Odion Ighalo kwa mkopo wa miezi sita.
Kocha huyo raia wa Norwey, amedai alikaa chini na makamu mwenyeki Ed Woodward na kumtajia wachezaji ambao anawataka, lakini ameshangaa kuona anawapata wawili jambo ambalo anaamini badi ni mtihani kwake kuweza kufanya vizuri msimu huu.
“Kumekuwa na uwekezaji mdogo wa kusajili wachezaji kwa kipindi cha miaka kadhaa iliyopita, zaidi ya pauni milioni 200 zimetumika kusajili wachezaji tangu nimekuja hapa, lengo la klabu ni kuwa na wachezaji wenye ubora mkubwa ili kuweza kuleta mataji kwenye kikosi.
“Lakini kwa uwekezaji huo bado tutakuwa na wakati mgumu, wakati wa uhamisho wa Januari nilitaka wachezaji wanne, lakini wamepatikana wawili, hii inaweza kuwa ngumu kutimiza malengo, hivyo timu ikishindwa kufanya vizuri anayeangaliwa ni kocha, hivyo chochote kinaweza kutokea,” alisema kocha huyo.
Leo Manchester United itashuka dimbani kwenye Uwanja wa Stamford Bridge kupambana na wapinzani wao Chelsea kwenye mchezo wa Ligi Kuu England. Manchester United wao wanashika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 35 baada ya kucheza michezo 25, wakati huo Chelsea ikiwa nafasi ya nne kwa pointi 41.