NYUMBA za kutolea ushauri nasaha (sober houses) jijini Dar es Salaam zimefurika waathirika wa dawa za kulevya baada ya kile kinachodaiwa kupotea kwa dawa hizo mtaani.
MTANZANIA limefanya utafiti katika baadhi ya vituo hivyo na kukuta idadi kubwa ya watu ambapo wasimamizi wake wamesema kabla ya msako wa watumiaji na wauzaji wa dawa hizo walikuwa wakipokea mtu mmoja au wawili kwa mwezi lakini baada ya vita hii kuwa kali sasa wanapokea watu tisa hadi 10 kwa siku.
“Kwa kweli hali sasa ni mbaya na ndiyo tumegundua kuwa nchi yetu imejaa mateja wengi kuliko kawaida, kwani hatukuzoea kupata waathirika wengi kiasi hiki kwani wote wamekuwa wakitaka kusaidiwa kwa sababu wamekosa ‘unga’ na wanapata maumivu makali ,” alisema Munishi.
Aidha, vituo hivyo vingi vimekuwa vikipokea watu wa jinsia moja au kuwatenganisha wasionane kwa sababu ya kuwaepusha tamaa za kimwili kwani wanapopata nafuu na mwili kurudi katika hali yake hali ya matamanio huwa kali zaidi hasa wakiwa pamoja watu wa jinsia tofauti hivyo wamiliki wengi wanaamua kuweka watu wa jinsia moja ili kuepukana na tatizo hili.
Aidha kuhusu dawa ya methadone alisema sober house nyingi hawazikubali kwa sababu haitibu bali ni njia salama ya kutumia dawa za kulevya kwani ina heroin hivyo mtu akikosa basi maumivu anayapata kama alivyokosa unga kwa hiyo mtumiaji hatakiwi kuikosa hata siku moja, kwa kifupi haitibu.