JESHI la Polisi wilayani kiteto mkoani Manyara limefanikiwa kuipata silaha aina ya SMG ikiwa na risasi 14 kati ya 30 zilizokuwamo baada ya kuporwa askari H 3068 PC Ginwe wakati akitekeleza majukumu yake ya ulinzi katika mnada wa Dosidosi wilayani humo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, ACP Camilius Wambura, amethibitisha kupatikana silaha hiyo ikiwa imefukiwa chini ardhi, baada ya jitihada kubwa zilizofanywa na Jeshi la Polisi wilayani hapa kwa kushirikisha viongozi wa kimila wa jamii ya kifugaji ya Kimasai.
“Kwa mara ya kwanza kufika hapa Kiteto pamoja na mambo mengine nimekuja kujitambulisha na kupongeza vijana wangu wa polisi kwa kazi nzuri waliyofanya ya kuokoa silaha aina ya SMG iliyokuwa imeporwa na wahalifu ikiwa na risasi 14 kati ya 30 zilizokuwamo,” alisema Kamanda Wambura.
Alisema awali askari H 3068 PC Ginwe wa Kituo cha Polisi Kibaya akiwa mnada wa Dosidosi Januari 14, mwaka huu akitekeleza jukumu lake, alishambuliwa na kundi la watu waliotaka kumuua mmoja wa watuhumiwa wa wizi wa fedha aliyekuwa mikononi mwa polisi.
Kamanda Wambura alisema Jeshi la Polisi Kiteto lilifanya kazi kubwa kufanikisha kupatikana kwa silaha hiyo ambayo ilihofiwa kuwa ingeweza kuleta madhara kwa jamii.
Askari huyo alijeruhiwa kwa kupigwa na silaha za jadi, sime na rungu akiwa hapo mnadani baada ya kuachwa na gari alipompakia mtuhumiwa wa wizi aliyemwokoa wakati akipigwa na wananchi wenye hasira.
Kutokana na tukio hilo, Kamanda Wambura alisema Jeshi la Polisi linawashikilia watuhumiwa sita kwa uchunguzi zaidi ambao wanadaiwa kumpora silaha askari huyo.