Na Upendo Mosha,Dodoma
Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda, amesema hawezi kutumia mgambo kuzuia wakulima wa kahawa kung’oa miche ya kahawa mashambani na badala yake watafiti wafanye tafiti zenye tija katika kuongeza uzalishaji wa kahawa sambamba na kutoa elimu.
Prof. Mkenda ameyasema hayo jana Alhamisi Juni 18, 2021 katika mkutano wa 11 wa wadau wa kahawa uliofanyika Jijini Dodoma ambao uliowakutanisha wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya wakurugenzi , taasisi za fedha pamoja na viongozi mbalimbali wa vyama vya msingi.
Amesema sekta ya zao la kahawa inakabiliwa na ukosefu wa tija kwa wakulima jambo ambalo baadhi yao wamekuwa wakipuuza kilimo hicho na kung’oa miche na kuamua kulima mazao mengine na kwamba wajibu wataalamu ni kuhakikisha wanatoa elimu na kufanya tafiti zinazoweza kuongeza uzalishaji wa kahawa zaidi.
“Kupambana na tija kwenye mazao yetu ni kufanya tafiti ili kuongeza uzalishaji naagiza taasisi ya ufatiti wa kahawa TaCRI muendelee kufanya jitihada za utafiti ili kudhibiti tija ndogo ili tupate mbegu bora na pia naomba mtushauri.
“Bila tija kupatikana kwenye kilimo haswa kahawa watu wataanza kung’oa miche na kuotesha vitu vingine na hilo ni suala la uchumi kiuhalisia (pure Economic) sitaweza kugombana nao na kutumia migambo kuwadhibiti wasifanye hivyo..ni wajibu wenu sasa kutoa elimu na kuwahelimisha umuhimu wa kulima kahawa,” amesema Prof. Mkenda.
Amesema mche mmoja wa kahawa una upaswa kuzalisha kilo moja na sio gramu 375 kama ilivyo na kwamba kuna changamoto ya upatikanaji wa mbegu bora za kutosha kwa ajili ya kilimo hicho.
“Hatuna mbegu za kutosha za mazao yetu tunahitaji kuzalisha mbegu zaidi hilo liende sambamba na kuongeza huduma za ugani kwa wataalamu wetu wapate mafunzo ya kutosha…kwani tatizo la ugani ni kubwa nchini kwetu,” amesema Prof. Mkenda.
Akizungumza katika mkutano huo, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya kahawa nchi, Primus Kimaryo, alisema bodi hiyo inahakikisha unywaji wa kahawa unaongezeka nchi na kwamba suala hilo halisabishwi na kuyumba kwa soko la kahawa duniani.