26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, June 1, 2023

Contact us: [email protected]

Waandishi wa habari watakiwa kuwa makini wanapoandika habari za corona

Na Janeth Mushi, Arusha
 
Waandishi wa Habari nchini wametakiwa kuwa makini wanapoandika habari za ugonjwa wa corona kwa kuhakikisha wanatumia takwimu, wataalamu na vyanzo sahihi ili kuepuka kutoa taarifa zisizo sahihi na kusababisha hofu katika jamii.

Aidha, kwa kufanya hivyo kumetajwa kusaidia kupunguza hofu iliyojengeka katika jamii juu ya ugonjwa huo,inayochangiwa na taarifa zisizo sahihi hasa kutoka kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.

Hayo yamesemwa na Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Uuguzi cha Rheumatology (University of the West of England, Bristol), Dk. Mwidini Ndosi, alipokuwa akizungumza katika mkutano wa siku moja ulioshirikisha waandishi wa habari, wadau na wataalamu wa afya.

Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Shirika la Internews Tanzania kwa waandishi wa habari yalifanyika jana kwa njia ya mtandao “Zoom”.

Dk. Ndosi amesema umakini unahitajika kwa kiasi kikubwa hasa wakati wa matumizi ya takwimu ikiwemo za kitafiti.

Amesema wananchi wanawaamini waandishi wa habari kupitia taarifa mbalimbali wanazotoa katika vyombo vyao,hivyo wanapaswa kuhakikisha wanatoa taarifa zenye ukweli ikiwemo za chanjo ya corona ili wananchi waweze kufanya maamuzi.

“Wananchi wa Tanzania wanaamini taarifa zinazotolewa katika vyombo vya habari hivyo mhakikishe mnapotoa taarifa mbalimbali ikiwemo za chanjo ya corona mpate wataalamu wanaohusika,”ameongeza.

Amesema siku za hivi karibuni kumekuwa na taarifa mbalimbali zisizo sahihi hasa za chanjo ya Covid-19 hasa kwenye mitandao hivyo wanahabari wana jukumu la kuhakikisha wanatumia vyanzo vilivyo sahihi.

Amesema kupitia mkutano huo waandishi wameweza kupata fursa ya kuongeza uelewa juu ya janaga hilo la corona hivyo wanaweza kutafuta wataalamu na kuwatumia katika vipindi na habari zao mbalimbali ili kuendelea kuelimisha jamii.

Akiwasilisha mada juu ya jukumu la wanahabari, Wwakilishi kutoka Taasisi ya Nukta Afrika, Daniel Mwingira, amesema wanahabari wana wajibu wa kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi kwa jamii.

Amesema katika kipindi hiki dunia inakumbana na janga la Covid-19, wanahabari wanapaswa kutoa taarifa sahihi kwa jamii ikiwemo kuelimisha masuala ya namna ya kujikinga na chanjo.

Amesema kwa kuandika habari za ukweli na usahihi hasa kuhusiana na suala la chanjo kutasaidia kuondoa hofu iliyojengeka katika jamii kubwa juu ya chanjo ya Covid-19.

“Katika kipindi hiki cha janga la Corona wanahabari mna wajibu wa kuhakikisha mnatoa taarifa sahihi ikiwemo ya masuala ya chanjo na umuhimu wake.

“Habari zisizo sahihi ni nyingi katika jamii ambazo zinachangia jamii kuwa na hofu hasa juu ya chanjo,hivyo mhakikishe taarifa zenu na takwimu ziko sawa na zimetolewa na mamlaka husika/vyanzo sahihi.

“Niwapongeze wadau ikiwemo Internews kwani mkutano huu ni muhimu na utasaidia hata waandishi wa habari wenyewe kwani baadhi yao walikuwa hawaelewi kuhusu chanjo,”amesema Mwingila kutoka Nukta Afrika.

Kwa upande wake Mratibu wa Programu kutoka Internews, Shaaban Maganga, amesema wanahabari wanayo nafasi kubwa ya kuisaidia jamii kwa kuandika habari zenye usahihi.

Amesema kupitia mkutano huo ambao pia ulishirikisha wadau wengine ikiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali na wataalamu mbalimbali, elimu waliyoipata itawasaidia kuongeza weledi katika majukumu yao.

Amesema  Internews kwa kushirikiana na wadau wake wengine, wamewakutanisha waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali, ili kujifunza masuala mbalimbali ya Covid -19.

Kwa upande wao baadhi ya waandishi walioshiriki mafunzo hayo akiwemo Mwandishi wa Mtanzania Dingital Winfrida Mtoi, amesema kuwa elimu waliyoipata kutoka kwa wataalamu mbalimbali itawasaidia kuandika kwa usahihi kuhusu ugonjwa huo hasa chanjo.

Winfrida amesema elimu bado inahitajika katika jamii ili kusaidia kubadili mtazamo hasi walionao wananchi wengi kuhusu ugonjwa huo hasa chanjo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,225FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles