Na BRIGHITER MASAKI-DAR ES SALAAMÂ
MKUU wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro, amewaagiza makamanda wa jeshi hilo kuwachukulia hatua watu wote watakaobainika kuhusika kwa namna yoyote kuchoma ofisi za vyama vya siasa nchini.
Alisema Jeshi la Polisi limejipanga kikamilifu kuhakikisha wanalinda amani na utulivu wa nchi katika kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba.
Sirro ametoa kauli hiyo wakati ofisi mbili za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) zikiwa zimechomwa moto ndani ya wiki mbili na watu ambao hawajajulikana.
Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa kikao cha viongozi wa Kamati ya Amani, Sirro alisema wanaochoma ofisi za vyama vya siasa ni kama wanalidhalilisha Jeshi la Polisi.
“Nitahakikisha nawashughulikia wote waliohusika kwa namna moja ama nyingine katika kuchoma moto ofisi, hali ya watu kujitokeza na kuchoma ofisi ni hali mbaya.
“Haiwezekani unacheza na Jeshi la Polisi, wanaosema wamechoma wenyewe, lakini tunawahakikishia wanaofanya uhalifu huo watapatikana,” alisema Sirro.
Aidha Sirro aliitaka kamati hiyo ya amani kukemea vitendo vya uvunjifu wa amani pindi vitakapojitokeza, ikiwezekana kwa kuita mikutano na wanahabari.
“Sisi tunashughulika na kupambana kimwili, jambo la kiroho tunawaachia viongozi wa dini, kubwa ni kutenda kwa kuongea na waumini makanisani na misikitini kuombea taifa katika kuelekea uchaguzi,” alisema Sirro.
Mwenyekiti wa Kamati ya Amani, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alisema katika kuelekea Uchaguzi Mkuu hawataridhia kuona mtu au chama kinahamasisha vitendo vya uvunjifu wa amani.
“Viongozi wa dini hatutaruhusu wala kuona mtu anapotosha na anaharibu amani ya taifa letu tukamwangalia.
“Tunataka kampeni za kistaarabu, hatutaki kusikia lugha chafu za matusi zikitolewa na wanasiasa wakati wa kampeni wakati watoto wakiwepo wanasikiliza,” alisema Sheikh Mussa.
Mwenyekiti msaidizi wa kamati hiyo, Zachary Kakobe, aliwaomba watu wote kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu wakiwa wamoja.
Alisema amani ni tunu na ni rahisi kuipoteza, lakini ni ngumu sana, kuna nchi nyingi zinatamani kuwa na amani, lakini hawaipati.
“Watanzania msipowachokoza polisi mkatulia, tutakuwa raia wema na wenye amani kwa kuanza vizuri uchaguzi na tutafanikiwa kumaliza salama, tukae tukijua msitu mkubwa unateketea kwa njiti ndogo sana, hivyo tuwe tayari kuzima njiti mapema kabla haijaunguza msitu,” alisema Askofu Kakobe.