25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mapinduzi yamkimbiza kwenye siasa kinara wa upinzani

BAMAKO, MALI

SIKU mbili baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyoulazimisha utawala wa Rais Ibrahim Keita kujiuzulu nchini Mali, kinara wa upinzani nchini humo ametangaza uamuzi wake wa kuachana na siasa baada ya kukutana na wanajeshi walioendesha mapinduzi hayo.

Kinara huyo wa upinzani, Mahmoud Dicko, amekuwa kiongozi wa upinzani nchini Mali aliyeongoza maandamanamo na malalamiko ya wananchi dhidi ya Rais Keita aliyelazimika kujizulu.

Dicko ambaye anaonekana kuwa na ushawishi mkubwa nchini Mali, alitangaza uamuzi huo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na wanajeshi walioongoza mapinduzi yaliyomlazimisha Rais Keita ajiuzulu.

Msemaji wa Dicko alisema kuwa kiongozi huyo ambaye alikuwa kinara wa kuchochea maandamano ya wananchi aliamua kutangaza kuachana na siasa. 

Hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa kuhusiana na uamuzi huu ikiwa ni siku moja tu baada ya wanajeshi walioongoza mapinduzi kutangaza kuwa wako tayari kuitisha uchaguzi baada ya kipindi cha mpito.

Hatua hiyo inaacha kitendawili kwa kuwa kile alichokizungumza Dicko na aina ya maelekezo aliyoyapata au makubaliano aliyofikia katika mazungumzo yake na wanajeshi hao bado inabaki kuwa siri.

Hayo yanajiri katika hali ambayo jumuiya, taasisi na nchi mbalimbali zimeendelea kulaani mapinduzi ya kijeshi nchini Mali yaliyohitimisha utawala wa miaka saba wa Rais Keita.

Umoja wa Afrika (AU) sambamba na kulaani mapinduzi hayo ya kijeshi, umetangaza kusimamisha uanachama wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres pia amelaani mapinduzi hayo ya kijeshi nchini Mali. 

Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (Ecowas), nayo imelaani mapinduzi hayo na kusema itafunga mipaka yote ya anga na nchi kavu ya Mali sambamba na kuwawekea vikwazo wale wote waliohusika na mapinduzi hayo.

Mali imekuwa ikikabiliwa na machafuko ya kisiasa na maandamano  kwa kipindi cha miezi miwili sasa. 

Maelfu ya wafuasi wa kambi ya upinzani walishiriki kwenye maandamano nchini humo kushinikiza Rais Keita na Waziri Mkuu wake, Boubou Cisse wajiuzulu.

AFP

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles