ANDREW MSECHU -DAR ES SALAAM
KITABU cha Rais mstaafu Benjamin Mkapa, ‘My Life, My Purpose’ (Maisha Yangu, Kusudio Langu), ambacho juzi kilizinduliwa na Rais Dk. John Magufuli, kimeeleza siri za kiongozi huyo wa awamu ya tatu, ikiwa ni pamoja na Mwalimu Julius Nyerere alivyomlimisha kwa saa tatu mara baada ya kumteua kuwa katibu wake.
Kitabu hicho ambacho ni cha kwanza cha aina yake kuandikwa na kiongozi mstaafu wa Tanzania, pia kimeeleza jinsi alivyoandika kimemo kwenda kwa Mwalimu Nyerere kumweleza nia yake ya kuwania urais.
KULIMA KILA SIKU ASUBUHI
Katika kitabu hicho, Mkapa anasema alianza safari yake ya siasa mwaka 1974, ambapo bila kutarajia, aliteuliwa kuwa Mwandishi Maalumu wa Mwalimu Nyerere, Ikulu.
Anasema muda mfupi baada ya uteuzi huo, Mwalimu aliondoka kwenda Butiama, hivyo Mkapa alitekeleza majukumu yake kwa kukabidhi madaraka ya Mhariri Mtendaji wa gazeti la Daily News kwa Ferdinand Ruhinda, lakini akiwa na mshangao.
Mshangao wake ulitokana na hatua ya Mwalimu Nyerere kuondoka kwenda Butiama, akiwa hajui atarejea lini, hivyo aliamua kumfuata.
“Nilimkuta Mwalimu akiwa shambani, alishangaa, akaniuliza ‘Ben, umekuja kunipa taarifa? Ni vyema, Karibu’. Nilichukua jembe na kuungana naye kwa muda wa saa tatu, suala ambalo lilikuwa gumu kwa mtu aliyezoea kazi za ofisini,” anasema.
Kutokana na hali hiyo, anasema kazi yake ya kwanza baada ya kuteuliwa kuwa Mwandishi wa Rais ilikuwa ni kulima kila asubuhi, kisha mchana kurejea nyumbani, ambapo Mwalimu alikuwa akipumzika na kupokea simu, kama sehemu ya mawasiliano na watendaji wake.
“Nilikuwa mwajiriwa wa Ikulu, kwa hiyo nilikuwa makini kujenga uhusiano mzuri na wale niliowakuta pale, akiwemo msaidizi wake, Joseph Butiku. Pia nilimfahamu vyema msaidizi wake, Joan Wicken kutokana na majukumu yangu,” anasema Mkapa.
Anasema kwa miaka miwili aliyotumikia nafasi hiyo, alisafiri na Mwalimu na kujumuika naye katika vikao vya nchi zilizokuwa mstari wa mbele, ikiwemo Zaire (sasa DR Congo), Zambia na Botswana.
Mkapa anasema pia alihudhuria vikao vya Baraza la Mawaziri la Mwalimu, ambako alijifunza mengi kutoka kwake na kwa mawaziri waliokuwa na asili ya India, akiwemo Amir Jamal na Alnoor Kassum.
“Walikuwa wakiuliza maswali mengi sana, walikuwa ni watu wanaofikiri sana, wenye mitazamo ya kimaendeleo. Waziri Mkuu Msuya (Cleopa David) alinivutia, alikuwa mchapakazi haswa na hakuwa anatuingilia kwa kuwa kulikuwa na Wizara ya Habari,” anasema Mkapa.
Anasema Wizara ya Habari wakati huo ilikuwa inahitaji kuunda Wakala wa Habari ambao hatimaye ulithibitishwa na Baraza la Mawaziri, kwa hiyo Mwalimu Nyerere alimwagiza kuanzisha wakala wa hiyo iliyoitwa Shirika la Habari la Taifa (Shihata).
Mkapa anasema baada ya ya hapo, Mwalimu alimtuma kwenda Nigeria ili kurejesha mahusiano mema, kwa kuwa hakukuwa na balozi nchini humo tangu kumalizika vita ya wenyewe kwa wenyewe.
“Uhusiano haukuwa vyema kwa wakati huo kwa kuwa tuliunga mkono wapambanaji wa Biafra waliokuwa wakitaka kujitenga, Mwalimu alisema anahitaji mtu anayeweza kuzungumza vyema Kiingereza, ambaye anajua diplomasia, aliyeaminika na anayeweza kushindana na wahusika.
“Niliwasili Nigeria nikiwa balozi mwishoni mwa Oktoba 1976 na kuwasilisha nyaraka zangu kwa Jenerali Olusegun Obasanjo ambaye wakati huo alikuwa mtawala kupitia Serikali ya kijeshi,” anasema.
KUTOROKA UBALOZINI
Mkapa anasema baada ya kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, mwaka 1976 Mwalimu alifanya ziara ya kiserikali ya siku sita ambayo iilikwenda vizuri, ambapo pia alitoa muhadhara katika Chuo Kikuu cha Ibadan.
Anasema alipoondoka nchini hakuwa amefanya mawasiliano na Wizara ya Mambo ya Nje ili kujua ni mamnbo gani ambayo alipaswa kuyasimamia akiwa nchini Nigeria.
Mkapa anasema wakati huo, alilazimika kutoroka baada ya Wizara ya Mambo ya Nje kumkatalia ruhusa ya kuhudhuria uzinduzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kiliundwa Februari 5, 1977.
“Unajua, nilikuwa mhariri wa gazeti la Chama cha Tanu kwa miaka sita, kwa hiyo hatua ya kuungana kwa Tanu na Afro Shirazi Party na kuunda chama kipya, ilikuwa muhimu sana kwangu. Halafu mtu ananiambia siwezi kuwepo kushuhudia kwa macho yangu. Hilo niliona siwezi kulivumilia,” anaeleza.
Mkapa anasema alimweleza msaidizi wake kwamba aseme taarifa iliyotumwa kwa njia ya telegram ikimzuia kurudi nchini, ilifika wakati yeye akiwa ameshaondoka.
Anasema baada ya kuzinduliwa kwa CCM, alizungumza na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Ibrahim Kaduma, na wakati huo mtu mmoja aliingia ofisini kwake na kumwambia kuwa Mwalimu anamuhitaji nyumbani kwake Msasani.
Mkapa anasema alikwenda Msasani, ambako walikuwa wakipaita kliniki na alipofika, Mwalimu alimwambia ameamua kumteua kuwa Waziri wa Mambo ya Nje.
Anasema hatua hiyo ilimshtua na Mwalimu alisema anafikiria namna ya kumweleza Obasanjo na hajui atalipokea vipi suala hilo.
Mkapa anasema alimweleza Mwalimu kwamba; “Rais wangu, huna haja ya kuhofu kuhusu Obasanjo, alikupokea vyema wakati wa ziara yako ya kiserikali. Atajua kuwa kuna sababu maalumu ya wewe kuniteua mimi kwa nafasi hii ya juu, kwa namna yoyote. Kwa hiyo iwapo utaandika barua nitaiwasilisha mwenyewe na kuitolea maelezo.”
Anasema aliwasilisha barua hiyo kwa Obasanjo na kuwaaga wafanyakazi wenzake, kisha kurudi Tanzania kuanza kutekeleza majukumu yake mapya.
KUTENGENEZA FEDHA SI DHAMBI
Mkapa anasema wakati wa utawala wake, miongoni mwa maamuzi magumu aliyochukua ni suala la ubinafsishaji, hasa wa viwanda vilivyokuwa vikimilikiwa na Serikali, mabadiliko katika utumishi wa umma na kuuza nyumba za Serikali.
Anasema kwa sehemu, ubinafsishaji huo ulianza kutekelezwa na mtangulizi wake, Ali Hassan Mwinyi na viwanda muhimu vilivyokuwa vikimilikiwa na Serikali ambavyo yeye alisimamia ubinafsishaji wake ni Tanzania Breweries na Benki ya CRDB.
Mkapa anasema hatua hiyo ilikuwa muhimu kwa wakati huo kwa kuwa aliamini katika kujitegemea kwa kuwa uchumi wa nchi haukuwa mzuri.
“Elimu ya ujamaa ilikuwa imekolea nchini, kuanzia madarasani hadi kwenye Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), mashirika ya umma ilimaanisha kuwa yanamilikiwa na umma, hili lilikuwa limetukaa sana vichwani.
“Hii ilijenga picha kuwa kutengeneza au kumiliki fedha ilikuwa kosa, haikuwa sahihi. Taasisi ya kiuchumi lazima itengeneze fedha, lakini kwa wale walioamini katika ujamaa hii ilikuwa kosa.
“Hata sasa unaweza kuona makala za kijamaa katika magazeti au mkufunzi katika chuo kikuu akipinga ubepari na kuituhumu Tanzania kuwa wakala wa ubepari wa nchi za magharibi,” anasema.
UKOMO WA UONGOZI
Mkapa anasema suala la kubadilisha madaraka haliepukiki, japokuwa anashangaa baadhi ya nchi za Afrika hazina rekodi nzuri katika suala hili.
Anasema suala hilo limekuwa likivipa vyombo vya habari vya kimataifa hasa vya mataifa ya magharibi faida ya bure, kuliko hatua za kubadilishana uongozi kwa njia ya kidemokrasia.
“Ukomo wa urais kwa Tanzania ni vipindi viwili vya miaka mitano mitano na nakumbuka niliwahi kujadiliana hili na aliyekuwa Rais wa Msumbiji, Joaquim Chissano akasema vipindi viwili havitoshi.
“Anasema katika miaka mitano ya kwanza unaweka miundombinu na kuelewa mifumo inavyofanya kazi, kisha unasimamia mipango uliyoiweka kwa manufaa ya taifa, na kwa miaka mitano mingine, inasaidia kusimamia utekelezaji na kuiweka sawa mikakati,” anasema.
Mkapa anasema anadhani awali Chisano alikuwa na mtazamo wa vipindi vitatu na huenda alikuwa sahihi, lakini kwa Afrika, watu wana uchu wa madaraka na hadhani kama wataruhusu mtu mmoja kukaa madarakani kwa miaka 15.
“Binafsi, sina tabu na utaratibu wa mihula miwili ya urais, ndiyo maana vipindi vyangu viwili vilipomalizika niliondoka, kuongoza nchi masikini kama hii si jambo jepesi,” anasema.
UDHAIFU WA MWINYI
Mkapa anabainisha kuwa wakati wa utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi, Mwalimu Nyerere alionyesha kutoridhishwa na utendaji wake, ikiwemo namna alivyosimamia Muungano na kuibuka kwa suala la Serikali tatu.
Anasema katika moja ya kikao walichokaa walijadili suala hilo na yeye akawashauri ni vyema kwanza wakamjuza Nyerere ili kujua maoni yake na alitumwa yeye kwenda kupeleka ujumbe kwa mwalimu.
Mkapa anasema alitoka kwenye kikao hicho cha Kamati Kuu kilichofanyika Dodoma kumpelekea Nyerere ujumbe huo ambaye alisema; “waambie nimeshatoa maoni yangu kuhusu hilo, suala la muhimu hapa ni kwamba uwaeleze kuwa maoni yangu siwezi kukaa nayo, nitaitisha mkutano wa wanahabari kueleza msimamo wangu.”
Anasema alilazimika kumpigia simu Rais Mwinyi na kumwelekza msimamo wa Nyerere kuwa haungi mkono suala hilo na amepanga kuitisha mkutano na wanahabari kutoa maoni yake.
Mkapa anasema baada ya kuzungumza naye, Mwinyi aliamua kumkaribisha Nyerere Dodoma kuzungumza na Kamati Kuu na aliongozana naye.
“Na alipotoka tu kwenye ndege, niliona baadhi ya watu waliokuwepo wakimwangalia na kusema kuwa yeye (Nyerere) ndiye chanzo cha tatizo.
“Mwalimu alizungumza na Kamati Kuu, ambayo baadaye iliamua kuwa na kamati maalumu iliyojumuisha wabunge, wawakilishi kutoka Baraza la Mapinduzi la Zanzibar na Kamati ya Uongozi ya chama, ambapo alizungumza nao kuhusu suala hilo la Serikali tatu,” anasema.
NJIA YAKE KUWANIA URAIS, DK SALIM KUTAJWA NA NYERERE
Katika kitabu chake hicho, Mkapa anaeleza chimbuko la njia yake ya kuwania urais na jinsi alivyomshirikisha Nyerere na kuibuka jina la Dk. Salim Ahmed Salim.
Mkapa anasema mwishoni mwa mwaka 1994 alijadiliana na mke wake, Anna kuona kama kuna umuhimu kuendelea na siasa.
Anasema baada ya utumishi wa umma uliotukuka kati ya mwaka 1962 hadi 1995, alidhani ulikuwa wakati mwafaka kustaafu shughuli nyingine.
Lakini wakati huo huo, hali ya kisiasa ilivyokuwa nchini ilimfanya akose amani nafsini mwake kutokana na masuala kadhaa kutokwenda vizuri.
Miongoni mwa masuala ambayo yalikuwa yakimsumbua ni hali ya mishahara ya watumishi wa umma, makusanyo ya kodi yalikuwa chini, kulikuwa na sintofahamu kwenye mashirikisho ya wafanyakazi, hasa walimu na washirika wa maendeleo hawakuwa wakifurahia mambo yalivyokuwa yakifanyika nchini.
Mkapa anasema baada ya mashauriano na rafiki zake na mke wake, aliona anaweza kusaidia kuweka mambo katika nchi yetu.
“Hatua yangu ya pili ilikuwa kumtaarifu Mwalimu. Nikaandika ujumbe kwenda nyumbani kwake Butiama alipokuwa nikisema; Ndugu Rais, natumaini ni mzima, nimeamua kutafuta kuteuliwa, na nakutumia ujumbe huu kwa sababu sitaki usikie kwa mtu mwingine asije akapotosha juu ya sababu za uamuzi wangu.”
Mkapa anasema alimpa ujumbe huo Joseph Warioba ambaye ni mwenyeji wa mji wa Bunda, mji ambao ni jirani na Butiama, ingawaje hakumwambia lolote kuhusu kilichomo kwenye ujumbe, na Mwalimu hakujadili lolote na Warioba kuhusu ujumbe huo.
Mkapa anasema kuwa alikuja kukutana na Mwalimu Nyerere Dodoma, ambako alikwenda kuhudhuria kikao cha Halmashauri Kuu ya chama, na alitumia fursa hiyo kumweleza sababu za kutaka kuteuliwa.
Baada ya kumaliza kumweleza Mwalimu nia yake, alimshukuru kwa kumsikiliza, na kwamba alikuwa msikivu kwa kiwango cha juu, na alimsikiliza bila kutamka neno.
Mkapa anasema baada ya kumaliza, Mwalimu alimwangalia machoni na kumwambia; “Ahsante sana kwa kuwa mkweli na muwazi kwangu. Nami nitakuwa mkweli kwako.
“Sikuwahi kudhani siku moja utatafuta urais, wazo hilo halijawahi kuja mawazoni mwangu, na si tu kwamba sikutegemea utataka urais, lakini nilikuwa nikifikiria mtu mwingine ambaye angekuwa rais bora.
“Lakini juhudi zangu kumshawishi hazikufanikiwa, anasita, anadhani anaweza pata uteuzi kwenye sahani, hiyo si siasa, ni lazima upambane. Nilituma mjumbe kwake, lakini hakuonekana kuwa tayari.
“Ben nachoweza kukwambia, sitokuzuia, sitakupinga. Kama umeamua, endelea kama dhamira yako inavyokutuma.”
BARAZA LA MAWAZIRI
Mkapa anasema baada ya kuteuliwa na kushinda urais, aliwasiliana na Nyerere ambaye alimpongeza kwa ushindi na alimwomba amsaidie kujua ni nani anastahili kuwepo na kwenye Baraza la Mawaziri.
Anasema Nyerere alimwambia; “Ben, hili ni baraza lako, siyo langu. Ni Serikali yako, siyo yangu. Kwa hiyo kaa uunde baraza. Ushauri pekee ninaokupa ni kwamba kwanza, tuna makabila mengi, hilo hutakiwi kulipuuza hilo.
Jitahidi kuweka usawa, na pili tuna dini nyingi, ila tuna dini kubwa mbili, hili pia hutakiwi kulipuuza. Zaidi ya hapo, hii ni Serikali yako, ni baraza lako, nenda kaliunde.”
Anasema katika uteuzi wake wa Baraza la Mawaziri, aliamua kuwa wazi na alidhamiria kuwaacha waliowahi kuwa mawaziri wakuu, Cleopa Msuya na John Malecela, uamuzi mgumu uliowashangaza wengi.
“Nilikuja kusikia kuwa Mwalimu aliposikia taarifa hizo kuwa wawili waliowahi kuwa mawaziri wakuu si miongoni mwa mawaziri niliowateua, alisema hakuwahi kujua kuwa nina maamuzi magumu namna hiyo,” anasema.
WAZAZI WAKE
Mkapa anasema wazazi wake, mmoja alifariki dunia wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na mwingine alifariki wakati akiwa Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, na kwamba kazi yake aliyokuwa akiifanya haikuwa chaguo la baba yake, ambaye alitaka awe kasisi, daktari au mwalimu.
CHIMBUKO LA VUGUVUGU
Mkapa anasema alianza kushiriki katika midahalo na maigizo, akiwa mwanafunzi aliyependa zaidi Hesabu na Kiingereza, ambaye aliwahi kuigiza kama Lady Macbeth katika mashairi ya Shakespear.
Anasema katika midahalo na maigizo alijifunza mambo mengi ambayo baadaye yalimsaidia katika maisha yake ya kazi, hasa katika kuhutubia umma na alipokuwa bungeni.
Mkapa anasema alikuwa mwanafunzi mdogo, lakini machachari katika midahalo hatua iliyomfanya mlezi wao, Father Mc Tiernan kujikuta akilazimika kumwambia anyamaze.
“Sikuwahi kuwa na mambo ya kutamani wasichana hadi nilipofika Chuo Kikuu cha Makerere, hata wakati huo ilikuwa kwa mbali sana. Nilikuwa mtu tofauti, mwenye aibu sana kwa wasichana, labda ndiyo maana Father Tiernan alinichagua kuigiza nafasi ya Lady Macbeth,” anasema.
MWAMKO WA KISIASA
Mkapa anasema wakati wa vuguvugu la kudai uhuru, ambapo Chama cha TAA kilibadilishwa jina kuwa Tanu mwaka 1954, alijifunza mambo kadhaa kutoka kwa Mwalimu Nyerere, ambaye aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho mwaka 1955.
Anasema hatua ya Mwalimu kujiuzulu na kuacha kazi ya ualimu Pugu kisha kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa Tanu mwaka 1955 iliibua mijadala na mitizamo tofauti baina ya vijana, ambao waliona kuwa ameamua kuwa kama nabii, aliyeamua kuacha ualimu na kuanza safari mpya ya kutumikia taifa lake.
Mkapa anasema darasa la juu wakati huo, mwaka 1955 ambalo lilikuwa mbele yao, lilikuwa na mwamko wa juu wa kisiasa na lilianzisha umajumui wa kisiasa uliopewa jina la ‘Pukka’, naye alikuwa miongoni mwa washiriki waliokuwa na mwamko sana katika jumuiya hiyo.
“Nilikuwa na mwamko sana katika jumuiya hiyo, japokuwa rafiki yangu, Oscar Kambona alikuwa akiibeza. Muamko uliokuwepo haukuwafurahisha walimu wetu na hata matokeo ya GCE yalikuwa si mazuri. Kwahiyo mwaka uliofuata walitusisitiza kusoma kwa bidii kwa ajili ya mitihani na kuachana na mambo ya siasa,” anasema Mkapa.
Anasema wakati huo alibaini kuwa Waafrika hawana fursa za kutosha ikilinganishwa na zile walizokuwa wakizipata watu wa jamii ya waasia na ndipo alipoanza kujitambua, baada ya kuona ofisi nyingi za umma zikiwa zimejazwa waasia na wazungu.
Mkapa anaeleza hapo ndipo alipoanza kupata hisia za kukandamizwa na alianza kuandika barua kwa siri kwenye gazeti la Tanganyika Standard akisisitiza umuhimu wa kujitambua na kudai uhuru, akiwa na miaka 17.
Anasema maendeleo yake shuleni yalikuwa mazuri kwa kuwa alikuwa akishika nafasi za juu, ya kwanza hadi ya tatu kati ya wanafunzi 51 na baba yake alikuwa akitamani awe daktari.