25.5 C
Dar es Salaam
Monday, December 16, 2024

Contact us: [email protected]

Siri ya ‘Watoto wa Kamwene’ kuwabwaga mastaa SZIFF

CHRISTOPHER MSEKENA

GUMZO kubwa kwenye ulimwengu wa filamu za Kibongo ni waigizaji wapya Flora Kihombo na Rashid Msigala maarufu kama ‘Watoto wa Kamwene’ kushinda tuzo za Sinema Zetu International Film Festival (SZIFF 2019) katika vipengele vilivyo wakutanisha na mastaa wakubwa.

Mtoto Flora Kihombo, aliyeigiza katika filamu ya Kesho aliibuka kidedea katika kipengele cha Mwigizaji Bora wa Kike mbele ya mastaa Wema Sepetu, Monalisa na Johari.

Hali kadharika Rashid Msigala, aliwabwaga mastaa wakubwa kama vile Gabo, Madebe Lidai na Hemed Suleiman katika kipengele cha Miwgizaji Bora wa Kiume kupitia filamu yake ya Kesho.

Baada ya matokeo hayo kutangazwa, gumzo likawa uhalali wa watoto hao kutoka Iringa kushinda tuzo hizo mbele ya waigizaji wakubwa wenye uwezo, majina makubwa na filamu nyingi.

Wengi wakahoji, hivi kweli Rashid  mwenye filamu moja tu anaweza kuwa bora zaidi ya Gabo ambaye amecheza sinema nyingi na mwaka jana alishinda tuzo hizo kama Mwigizaji Bora wa Kiume.

Au mtoto Rashid ni bora kuliko ‘role model’ wake Hemed Suleiman na Madebe Lidai ambao wapo kwenye tasnia kitambo na Afrika Mashariki inawatambua kwa kazi zao.

Pia hivi inawezekana vipi mtoto Flora Kihombo akawa bora zaidi kuliko Monalisa aliyetwaa tuzo kibao za Kimataifa au Wema Sepetu aliyeshinda tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kike mwaka jana  na amefanya kazi na mastaa wakubwa Afrika akiwamo Van Vicker wa Ghana.

Ni ngumu kuamini kuwa Flora ana ubora mkubwa zaidi ya Johari ambaye anaelewa uchungu wa tasnia hii toka kipindi kile cha Kaole akiwa na kina Ray Kigosi na Steven Kanumba.

Hoja hizo ndiyo zimefanya watoto hao wanaolelewa katika moja ya kituo cha kulele watoto wanaoishi katika mazingira magumu huko Isimani, Iringa wawe maarufu zaidi.

Akizungumza na Swaggaz juzi, Jaji Mkuu wa tuzo za Sinema Zetu, Profesa Martin Mhando, anasema kitu ambacho watu hawakifahamu ni kwamba watu walikuwa hawategemei kama watoto wanaweza kushinda.

Ndani ya ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam kila mmoja aliyeingia kwenye tuzo zile alikuja na mshindi wake huku wale watoto wakipewa nafasi ndogo ya ushindi.

Ndiyo maana kumekuwa na malalamiko juu ya kuwashindanisha watoto na watu wazima jambo ambalo ni kawaida kufanyika kwenye tuzo nyingi zikiwamo zile kubwa kabisa duniani za Oscars.

“Watu wengi walikuwa wanategemea mshindi ni yule atakayekuwa amepigiwa kura nyingi na watazamaji na ili tuzo ziwe za kitasnia kwa vyovyote lazima majaji wawe wenye uzoefu katika tasnia na wanaojua namna ya kujaji filamu,

“Kwahiyo asilimia 40  ya alama zote zinatoka kwenye kura za watazamaji lakini asilimia 60 zinatoka kwa majaji wao ndiyo wanajua kiwango gani cha Kimataifa au kiwango cha tasnia, ukimpa mtu wa nje ndiyo akuchagulie mshindi basi utakuwa huwezi kujua kama kile kiwango ni kiwango cha Kimataifa au kiwango cha tasnia,

“Ndiyo maana tukaamua kwamba watu wapige kura na zile filamu zitakazofikisha asilimia 40 zinaingia katika kinyang’anyiro cha pili ambapo majaji wanazijadili, kwa hiyo wale watoto walitoka kwenye hiyo 40 wakaingia kwenye hii asilimia 60 na wakaonekana ni washindi,” anasema jaji mkuu Mhando.

Kwa hiyo unaweza kuona ni namna gani ‘watoto wa kamwene’ walivyoweza kuwapiga bao mastaa baada ya jopo la majaji kuona filamu ya Kesho ina sifa za kutoa Mwigizaji Bora wa Kiume na Mwigizaji Bora wa Kike.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles