Na CHRISTOPHER MSEKENA
JARIDA la Forbes Africa lililojipatia umaarufu kwa kutoa orodha ya watu wenye mafanikio kutoka kwenye sekta mbalimbali barani Afrika mapema wiki hii lilitoa orodha ya vijana wenye umri chini ya miaka 30 ambao wamepata mafanikio katika sekta mbalimbali mwaka 2017 huku Tanzania ikiwa imeingiza vijana wanne ambao ni Harun Elias, Godfrey Magila, Upendo Shuma na Jokate Mwegelo.
Hapa kwenye Gumzo la Town leo tunamwangalia zaidi Jokate Mwegelo ambaye ni mdau wa burudani akiwa kama msanii wa muziki, filamu na Miss Tanzania 02, mwaka 2006.
Jokate amekuwa akiutumia umaarufu wake kwenye sanaa na urembo kutengeneza ajira kwa vijana na kipato hali iliyomfanya atazamwe kama kijana mwenye mafanikio.
Katika orodha hiyo ambayo Jokate alikuwa namba tatu, Forbes Africa liliandika makala fupi ya kimombo iliyosomeka kwa lugha ya Kiswahili;
Miaka mitano iliyopita, Mwegelo alitumia fedha zake na mkopo kutoka kwa bilionea kijana barani Afrika, Mohammed Dewji ‘MO’ kuanzisha Kampuni ya Kidoti inayojishughulisha na urembo.
Kampuni hiyo inasanifu na kutengeneza nywele, viatu aina ya ‘sendozi’ na mikoba.
“Mpaka sasa tumefanikiwa kuwa na takribani nywele 60,000 sokoni, tukiwa na imani ya kufanya vizuri zaidi tutakapokuwa na kiwanda chetu wenyewe hapa nchini,” alisema Mwegelo.
Jarida hilo liliendelea kufafanua kuwa mwanasiasa, mhitimu wa masomo ya falsafa na mtangazaji huyo (Jokate Mwegelo), aliongeza kuwa anataka kutumia umaarufu wake kwa kufanya mambo mazuri.
“Nimetumia muda mwingi katika programu za biashara na ICT (Teknolojia ya Mawasiliano na Habari). Hapo ndipo tamaa yangu ya kuwa na kampuni na bidhaa ilipokuja.
“Nilihisi kuwa tunahitaji bilionea wa kike, mpaka sasa viwanda vingi hapa nchini vinamilikiwa na wanaume, kama zilivyo bidhaa nyingi za urembo sokoni, ingawa watumiaji ni wanawake.”
Mwegelo alimfuata Dewji kwa ajili ya kumpa msaada, bilionea huyo alijitolea kumpa baadhi ya bidhaa zake ili aziuze kwa ajili ya kupata fedha.
Kwa upande mwingine, Mwegelo anatambua umuhimu wa kurudisha sehemu ya alichonacho kwa jamii.
Katika hilo, mrembo huyo ameanzisha kampeni ya ‘Be Kidotified’ ambayo inalenga kuwawezesha wasichana kwa kujenga miundominu ya michezo katika shule za Serikali, kuwahimiza katika elimu na ujasiriamali.
Pia, Mwegelo ameanzisha shindano la ‘Msusi Wao’, ambalo huwaunganisha wasusi, wawezeshaji kiuchumi na wateja. Hivyo ndivyo lilivyoandika jarida la Forbes Africa, likitoa siri ya Jokate kuchomoza kwenye orodha hiyo iliyojaa vijana wa mataifa mbalimbali ya Afrika wenye mafanikio.
Nafasi aliyoipata Jokate imewashtua mastaa wengi hasa wa kike ambao licha ya umaarufu wao wameshindwa kutengeneza mkwanja kwenye ujasiriamali.
Jokate amewaamsha warembo mastaa wa Kibongo waliolala huku wakiridhika na mafanikio kiduchu waliyoyapata kwenye sanaa zao na pia ameonyesha kuwa inawezekana mrembo kuwa na mipango ya kuwa bilionea siku za usoni.
Nilichogundua kwenye orodha ile nchi za Nigeria na Afrika Kusini zimetoa vijana wengi zaidi wenye mafanikio, naiona nafasi ya mastaa wengine wa kike ikiwa wazi kwenye mafanikio na endapo tu watakubali kutumia ustaa wao kustawisha shughuli za kijasiriamali nje za sanaa.
Vijana hao ni wengine ni Sandra Mwiihangele wa Namibia, Nasir Yammama, Iyinoluwa Aboyeji, Edikan Udiong, Muktar Onifade, Shakeela Williams wa Nigeria, Sibusiso Ngwenya, Corbyn Munnik, Rupert Weterings, Thato Kgatlhanye, Lulo Rubushe, Khethi Ngwenya, Jennifer Glodik na Rushil Vallabh, Allegro Dinkwanyane wa Afrika Kusini.
Wengine ni Sean Drake, Alloysius Attah wa Ghana, Eugene Mbugua, Zameer Verjee wa Kenya, Jean Bosco Nzeyimana wa Rwanda, Knight Ganje, Shaleen Manhire wa Zimbabwe, Jishan Ahmed (Zambia), Mike Chilewe Jnr, Mwayi Kampesi (Malawi), Elijah Lubala (Kongo).