NEW YORK, Marekani
STAA wa vipindi vya televisheni vya Keeping up with the Kardashian, Kim Kardashian (35), ameelezwa kuwa na hofu kubwa ya vitu vyake vya siri vilivyopo katika moja ya simu yake kati ya simu zake mbili zilizoibiwa alipovamiwa akiwa hotelini Paris nchini Ufaransa.
Hofu hiyo inakuja baada ya kugundulika kwamba simu hizo mbili zilizoibwa pamoja na vito vya thamani imeongeza thamani ya vitu vilivyoibwa na wavamizi hao watano wanaoendelea kusakwa na polisi wa Ufaransa kutoka zaidi ya dola za Marekani milioni 10 hadi zaidi ya dola za Marekani milioni 11.
Wadadisi wa mambo waliokaribu na Kim, wanadai kwa sasa hofu yake si kama fikra zake alipovamiwa akiwa amevalia nguo za kulalia kwamba watekaji wangembaka au kumuua bali ni juu ya simu yake kuja kutumika vibaya na watekaji hao kwa kumtaka awape kiasi kikubwa cha fedha ama wasambaze vitu vyake vya siri mitandaoni.
Wadadisi hao wanaeleza kwamba, imani yao kubwa ni kwamba watekaji hao bado hawajafuta vitu vya siri vilivyopo katika simu hizo kwa kuwa uwezo wao wa utekaji waliotumia ni wa kisasa na hali ya juu hivyo watatumia vitu hivyo vya siri kujinufaisha zaidi.
Hata hivyo, mume wa Kim, Kanye West (39), amemfukuza kazi na kutomlipa mshahara mlinzi wa Kim, Pascal Duvier, baada ya kudai kwamba ripoti inaonyesha kuna uzembe wa mlinzi huyo kumuacha mkewe peke yake na kwenda kwenye muziki na wadogo wa Kim.
Mtandao wa Hollywood Life umeripoti kwamba, Kanye alimtupia lawama Pascal alipomfuata na kumhoji kwa hasira huku akimtazama usoni na muda mwingi alikuwa akimuuliza kwanini hakuwa karibu na Kim wakati alikuwa akihitaji msaada wake.
“Alisikika akimfokea Pascal kwamba Kim angeuawa je? Kanye alikasirika kiasi kwamba aligoma kumlipa Pascal kitendo ambacho kilimfanya Kim amtulize na kumpeleka chumba kingine,” ulieleza mtandao wa Hollywood Fife.
Awali baada ya Kim kuvamiwa, polisi walieleza kwamba watekaji hao watano waliiba boksi lenye vito vya thamani ya euro milioni 6 sawa na dola milioni 6.7 na pete yenye thamani ya euro milioni 4.