Na FRANCIS GODWIN– IRINGA
MBUNGE wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), amesema ataendelea kusimamia ukweli na hataogopa kufungiwa bungeni.
Alisema ataliambia Bunge na wananchi kwamba hali ya maisha mtaani ni ngumu hata kama ukweli huo utasababisha yeye kufukuzwa bungeni.
Alisema kazi ya wabunge kwa ujumla wake ni kuihoji na kuikosoa Serikali hivyo hataacha kuikosoa inapofanya tofauti lakini pia haogopi kuchukuliwa hatua na kupewa na Spika wa Bunge ambaye hapendi kuona wabunge wa upinzani wakiikosoa Serikali iliyopo madarakani.
Akiwahutubia wananchi wa Iringa Mjini, katika Uwanja wa Mwembetogwa, Mchungaji Msigwa, alisema mtaani kuna uhaba mkubwa wa fedha ambao umesababisha watu kukosa fedha mifukoni ambayo imewakumba wabunge pia.
“Kazi yangu kama mbunge si kupongeza kila jambo ila pale Serikali inapokwenda ndivyo sivyo kazi ya Kambi ya upinzani bungeni ni kuikosoa yasiyokwenda sawa.
“Ninaongea haya huku nikijua nitafungiwa ama kupewa adhabu kwa kuyasema haya ila siogopi hata kama nitapewa adhabu ya kufungiwa hata mwaka mmoja poa tu, ila nitasimamia ukweli.
Mchungaji Msigwa alisema anashangazwa na kauli ya Serikali kwamba uchumi wa Tanzania upo juu kuliko nchi yoyote Afrika, lakini ni wakati wa kila Mtanzania kujiuliza kama mfukoni mwake kuna pesa.