26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

SINTOFAHAMU ZATAWALA VIWANDA VYA SARUJI NCHINI

Na SHERMARX NGAHEMERA,

BIASHARA ya saruji ni kama maji ya mto uliokomaa na wa kina kirefu, ukitazama kwa juu utayakuta maji yametulia tulii, lakini ukienda chini hadi kwenye sakafu ya mto kuna mkondo mkubwa wa maji ambao una nguvu ya kukokota vizuizi vyake.

Kuna matatizo mengi yanayokabili viwanda vya saruji hapa nchini na hadi vingine kukata tamaa kwa kuona hakuna  usawa wa kushughulikia matatizo yao na serikali na kila kukicha ushindani unaongezeka, kwani viwanda vingine vinaanzishwa kuendana na azma ya serikali ya kufanya nchi hii kuwa ya uchumi wa viwanda.

Tanzania imepiga hatua kubwa katika mwongo mmoja uliopita katika kujenga mitandao ya barabara na miundombinu yake ya mawasiliano na hivyo kufanya biashara ya saruji kufaidika na kuongezeka kulikopitiliza kwa mahitaji ya bidhaa hiyo, licha ya kuwa na matatizo mengi ya upatikanaji nishati na mifumo ya usambazaji bidhaa usioridhisha.

Mengi ya matatizo ya viwanda vya saruji yameainishwa na Mkurugenzi Mtendaji  wa Tanga Cement (Simba Cement), Reinhardt Swart, alipokutana na wanachama  wa  Jukwaa la Wahariri  (TEF), ambapo  aliwa eleza kuwa  Serikali inatakiwa kufanya zaidi kurekebisha hali na mwenendo wa biashara, kwani inaonekana viwanda kufanya kazi katika sakafu  iliyo tenge.

Swart anaona ngumu kumeza  na anasema kuwa, licha ya dhamira nzuri ya serikali ya awamu ya tano ya kuja na sera ya viwanda, lakini kama changamoto za kisera na kimiundombinu hazitaweza kufanyiwa kazi, sera hiyo  inaweza  kushindwa kutekelezeka.

Anasema serikali imejikita zaidi katika uanzishwaji wa viwanda vipya badala ya kuboresha mazingira ya viwanda vilivyopo viweze kuimarika.

Tunaposema viwanda siyo lazima viwe vipya, bali ni shughuli za uzalishaji mali kiviwanda.

“Sera ya uchumi wa viwanda ni nzuri, lakini naona serikali imejikita katika uanzishwaji wa viwanda vipya, hivyo naona kutakuwa na anguko kubwa la viwanda vya zamani,” anasema Mkurugenzi Swart.

Hivyo anaishauri serikali kuwa ni vema kwanza ingetatua changamoto zinazoikabili sekta ya viwanda vya saruji kwa sasa, ili vilivyoko viendelee  kuwepo kwa muda mrefu badala ya kunyong’onyeshwa na mwishowe kufa.

Anaongeza kwa kusema, kwa vile Tanzania inataka uchumi wa viwanda, ni lazima ihakikishe inatoa kipaumbele kwa wawekezaji wazawa kuwekeza zaidi katika sekta binafsi kwa kununua hisa  zake na wao kuwa wabia wa wawekezaji kutoka nje.

Alibainisha kuwa, baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta hiyo kuwa ni uhaba  wa nishati ya umeme, ambayo wakati mwingine inawalazimu kutumia nishati mbadala ili kuendelea na uzalishaji. Kwa Kiwanda cha Saruji Tanga, kimeshindwa kutumia majiko yake yote ya kutengeneza ‘klinker’ kwa kukosa umeme wa kutosha wakati kiwanda kimewekeza hela nyingi katika kuboresha uzalishaji kiwandani hapo na hivyo kubakia katika uzalishaji uleule.

“Tunatumia umeme katika mitambo yote, lakini uliokuwepo ni mdogo, hali iliyolazimu wakati mwingine kusitisha uzalishaji ili kufidia gharama ya ziada za uzalishaji umeme kiwandani hapo,” amebainisha Swart.

“Serikali ione umuhimu wa kutumia nishati mbadala kama gesi na mafuta  katika kusaidia kuzalisha umeme wa uhakika maalumu ambao utaweza kutumika kwa ajili ya viwanda pekee,” ameshauri Mkurugenzi huyo.

Ethiopia imeanzisha mfumo wa umeme ambao unakwenda viwandani tu na hautumiki kwa shughuli nyingine, ila uzalishaji na inaendelea vizuri katika kiwanda cha Dangote Cement kule Ethiopia.

Kuhusu miundombinu ya kusafirishia saruji au malighafi zake, ni tatizo mojawapo kubwa nchini, kwani gharama ni kubwa sana kwa kutumia usafiri wa barabara badala ya ule wa reli ambao ni nafuu na wa uhakika. Kwa hali hiyo bei ya saruji ya Tanzania ni ghali bila sababu ya msingi kutokana na changamoto za miundombinu ya usafiri.

“Saruji inayozalishwa nchini ilipaswa iuzwe kwa bei sawa na bure, lakini gharama za usafirishaji zimekuwa ni kubwa kutokana na kuwapo kwa miundombinu ambayo si rafiki,” amebainisha Swart.

Mkurugenzi wa Kiwanda cha Saruji Tanga, anasema licha ya saruji yao kupangwa kusafirishwa kwa njia ya reli kwa ajili ya kusafirisha shehena ya mizigo, lakini bado huduma hiyo haipo katika maeneo mengi nchini, hivyo shehena nyingine hulazimika kutumia barabara ambayo ni ghali sana.

Anaongeza kuwa, kama Serikali itaboresha huduma ya reli na kuwa ya uhakika, wanaweza kuachana na usafiri wa barabara, kwani ni ghali sana.

Mkurugenzi Swart anasema changamoto nyingine ni kuwapo kwa saruji kutoka nje ya nchi, hali inayosababisha wazalishaji wa ndani kukosa soko la bidhaa zao kutokana na ukweli kuwa, saruji inayotoka nje huuzwa kwa bei ndogo, tofauti na inayozalishwa nchini, kwani wao hawalipi kodi kwao. Anasema kimsingi hakuna sababu ya kuagiza saruji ya kawaida kutoka nje, kwani uzalishaji hapa unatosheleza.

“Licha ya serikali kuongeza kodi kwa saruji kutoka nje, bado tatizo ni kubwa, kwani viwanda vya humu nchini vina uwezo wa kuzalisha tani milioni 4.8, huku soko likihitaji tani milioni 3 pekee, hivyo kuna kiasi kikubwa cha saruji  kinadharia kinabaki bila ya soko,” amebainisha Swart.

Ameupokea ujaji wa viwanda vipya kwa hali iliyojaa sintofahamu, kwani hadi sasa viwanda vilivyopo havijatumia  uwezo wake wa uzalishaji hadi mwisho kutokana na matatizo mengi ya uzalishaji, kama alivyoainisha, lakini  anakaribisha ushindani, kwani ndiyo njia pekee ya kuboresha utoaji huduma  na wenye tija ndio mhimili soko na kusonga mbele.

“Hatuogopi kushindana, ila mambo yawe sawa kwa wote badala ya wengine  kupendelewa vitalu na masharti mengine ya kuwawezesha kufanya bora kwenye soko,” alishauri.

Mwekezaji mkuu wa Saruji Afrika Dangote Cement ni Aliko Dangote.

Makaa ya mawe ni kero

Swart anasema kuwa, licha ya serikali kutoa agizo la usitishaji wa ununuzi wa makaa ya mawe kutoka nje, lakini bado kumekuwa na changamoto nyingi katika muundo wa ununuzi wa bidhaa hiyo nchini.

Anasema kumekuwa na madalali wengi katika biashara ya makaa ya mawe, hali inayosababisha wakati mwingine kuuziwa bidhaa ambayo haina ubora, hivyo huathiri hata saruji wanayozalisha.

Wachunguzi wa mambo wanashindwa kuelewa athari hiyo ya makaa ya mawe inatoka wapi, kwani haitumiki kama malighafi, ila kwa kupasha moto mawe ya kusagwa au wakati wa kusaga.

Kumaliza ubishi wa masuala ya ubora, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) mwezi uliopita limepitisha viwango 18 mbalimbali vya makaa ya mawe na hivyo kufanya biashara hiyo iwe na uwajibikaji zaidi kwa pande zote, yaani wanunuzi na wauzaji wa makaa ya mawe hayo nchini.

“Hivi basi madai ya kuwa makaa ya mawe yanayozalishwa nchini hayafai yatakomeshwa vilivyo kwa kutumia taaluma na si hisia na janja janja kwenye masuala ya kitaaluma kama hayo,” anasema mchumi Habi Litaunga.

Kuhusu utitiri wa madalali, hata Rais John Magufuli analifahamu na alilikemea  suala hilo kule Mtwara kwenye Kiwanda cha Dangote na kuwaita watu hao kuwa ni ‘wapiga dili’ na kuonekana kuwa ni kero kubwa kwa wazalishaji mali hapa nchini na hivyo aliagiza kiwanda kikubwa kuliko vyote hapa nchini cha Dangote Cement kipewe kitalu cha makaa ya mawe yake ili kiweze kuchimba chenyewe kwa kuzingatia mahitaji yake.

“Dangote apewe eneo lake la kuchimba makaa ya mawe ndani ya wiki mbili, ili hao wapiga dili wasiendelee kumsumbua na madai yao,” alisema Rais Magufuli kiwandani Mtwara.

Naye Makamu Mwenyekiti wa TEF, Deusdadit Balile, aliwaasa wahariri  wahakikishe wanawasilisha kero pamoja na changamoto zilizopo viwandani  kupitia vyombo vyao na kutaka kusikia zaidi kutoka viwanda vingine, ili kuona namna gani serikali ifanye kumaliza kero hizo, hasa ikizingatiwa kuwa viwanda vya saruji ni walipaji wazuri wa kodi na wanachangia vizuri pato la Taifa.

‘Tuna majukumu ya kuifahamisha  serikali katika kuibua changamoto ambazo zinawakabili wawekezaji wa ndani ili ziweze kupatiwa ufumbuzi wa haraka,” alisema Balile.

Ikaonekna kuwa wazalishaji wa ndani wanapaswa kuzalisha bidhaa zenye ubora ambazo zitaweza kuleta ushindani katika soko la ndani ya nchi na hata nje, kwani bidhaa bora hujiuza yenyewe, lakini wasichukulie kuwapo hapo kama ndiyo kinga ya kutotengeneza bidhaa isiyo bora. Mahitaji ya saruji kukidhi miundombinu kama barabara za juu yataka saruji ya viwango vya uhakika na vilevile mtambo wa LNG kule Lindi.

“Wazalishaji wakongwe hawana haja ya kuhofia viwanda vipya, kwani wachukulie ujio wao kuwa ni changamoto na wana jukumu la kuhakikisha wanajiimarisha katika kuzalisha bidhaa bora na ili waweze kuleta ushindani kwa wazalishaji wapya,” alisema Frank Sanga, mhariri kutoka Mwananchi Communications Limited.

Kiwanda cha Mbeya Cement (Lafarge au Tembo Cement) ina tatizo kubwa la umeme na usafiri wa mazao yake, kwani  ujenzi wake uliambatana na usafiri rahisi wa Reli ya Tazara, lakini reli hiyo inaishi kwa kivuli chake kwa sasa. Sera ya TAZARA ya kuipendelea Zambia imepitwa na wakati, kwani hakuna tena tishio kutokea Afrika Kusini, baada ya maelewano nchini humo na serikali ya ANC iko madarakani.

Dangote Cement imekuja karibuni, nayo imetamalaki matatizo ya kila namna kwenye kiwanda cha uwezo wa kuzalisha tani milioni tatu kwa mwaka na mwaka huu wanategemea kufikisha uzalishaji wa tani 800,000, kufuatiwa na mwakani tani milioni moja. Matatizo makubwa ni nishati isiyoaminika, uchanga wa miundombinu ya biashara, usafiri wa barabara ambao ni ghali na umeanza kuwekewa mizengwe ya kisiasa kuwa magari ya Dangote yanaharibu barabara  na yapigwe marafuku n.k.

Mkongwe wa shughuli za saruji nchini, Kiwanda cha Twiga Cement (TPCC) Dar es Salaam, kina matatizo ya gharama na uhakika wa upatikanaji wa nishati ya umeme wa kuzalishia saruji. Kwa ukubwa ni kiwanda cha pili, kikifuatiwa na Simba Cement, halafu Tembo Cement.

Vingine ni viwanda vya Rhino, Lake Cement, Camel.

Kuna viwanda vitatu vya saruji vitajengwa na viko katika hatua mbalimbali za kujengwa Dar es Salaam, Mkuranga na Tanga. Hengya Cement, EAM Cement kule Tanga na Sungura Cement Mkuranga.

Katika uchunguzi uliofanywa kwa wanunuzi na watumiaji wakubwa wa saruji kama NHC, WCH, Tan Roads wote kwa ujumla wamekubali kuwa  hali ya upatikanaji bidhaa ya saruji haina ugumu wala usumbufu, “Ni pesa yako tu.”

Lakini kutokana na kukua kwa mahitaji na shughuli za saruji, itakuwa si kosa kuanzisha mamlaka mahsusi kusimamia bidhaa hiyo muhimu kwa maendeleo ya nchi

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles