MABADILIKO SERA YA MITAJI KUFANYA DSE KUWA SOKO MOTO

0
643
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango

Na Shermarx Ngahemera,

SERIKALI ina mipango mikubwa ya kuruhusu uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje kwa kuruhusu hisa za makampuni ya simu na migodi  kununuliwa na yeyote aliyenacho na popote alipo ili kufanikisha mitaji inayotakikana na hata  katika Toleo la mwanzo (IPO)  kwa uwekezaji mkubwa nchini.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango, anashughulikia  mabadiliko hayo kufuatia uwekezaji katika IPO ya Kampuni ya Vodacom Plc kuchukua muda mrefu usiotegemewa na kukosa maelezo ya kina hadi sasa.

Kampuni za Airtel na Tigo ambazo wanatakiwa kisheria kujiunga kwa sharti ikiwa  itifaki na masharti yakizingatiwa, ziko kwenye mlolongo  wa  kwenda  mbele kujiunga kwa sheria ila  Tigo  ina matatizo wakati Airtel njia nyeupe.

Ufunguzi wa milango ya uwekezaji kwa wote ni mabadiliko makubwa ya kisera na kiutendaji ili kufanikisha haraka mahitaji ya Taifa ya mitaji  na kuongeza nguvu kuelekea uchumi wa viwanda.

Serikali imebadilisha msimamo wake huo wa kiuchumi ili kulifungua Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) litafute mitaji bila kikwazo kutoka ulimwengu mzima na hivyo kudai marekebisho mengi ya sheria na sera za fedha na uchumi nchini.

“Nia ni kupata wawekezaji kutoka Afrika Mashariki, Diaspora (ughaibuni) na masoko ya mitaji duniani kwenye  matoleo ya awali  (IPO) zaidi ya ilivyo sasa ikiwaruhusu wananchi tu,” alisema Waziri  wa Fedha wakati wa kufunga hotuba ya mawasilisho ya bajeti bungeni.

Serikali itafanya mabadiliko katika Sheria ya  Elektroniki, Posta na Mawasiliano (EPOCA) ya mwaka 2010 ili wawekezaji wa  aina yote washiriki katika shughuli za uchumi hapa nchini hususani katika matoleo ya mwanzo ya hisa (IPOs). Mabadiliko  hayo yanategemewa kufanywa kwenye Sheria ya Fedha ya 2017 ili iendane na uuzaji wa hisa za Airtel na Tigo kwa mafanikio.

Serikali imepanga kuwa na bajeti ya Sh trilioni 31.7 kwa mwaka 2017/18, ikiwa ni matumizi makubwa na ina mipango ya kutekeleza azma yake ya kufanya uchumi  unamilikiwa na wananchi na hivyo  migodi na shughuli za madini kuachia asilimia ya hisa zake kwa kiasi cha asilimia 25 kwa umma wa Tanzania walionazo kuwekeza DSE.

Watanzania walioko nje ya nchi sasa wanaweza kushiriki katika ununuzi wa hisa za awali wa kampuni za simu za Airtel Tanzania na Tigo ambazo ziko mbioni kujiorodhesha.

Mahitaji ya fedha za mitaji katika sekta za mawasiliano na madini ni makubwa na hivyo Serikali imeona ni bora ifungue milango kwa wote ili waweze kugharamia shughuli hizo.

Mabadiliko yanalenga kufanya mambo yaende haraka badala ya kusubiri Watanzania wa ndani  pekee ambao wameonesha  kukosa uwezo mkubwa.

Uzoefu kutoka Vodacom Tanzania Plc, IPO, hatima yake haijajulikana miezi miwili baada ya kufunga mauzo ya hisa.

Vodacom ilikuwa inahitaji uwekezaji wa Sh bilioni 476 kutokana na mauzo ya hisa milioni 560 na kila hisa ikiuzwa Sh 850 na kuna kila dalili kuwa mauzo hayakwenda  vizuri hata baada ya kuongezewa muda wa mauzo.

Kuzuia mambo yasiende kombo imebidi Serikali  ifanye  mabadiliko makubwa  kwa kuifungua  nchi na kuachana na masharti  ya uasilia wa mitaji.

Shauku iliyozimwa ya  hisa za Vodacom ni kitendawili kikubwa cha kibiashara kwani kinaleta jakamoyo kwa  masuala mengi ya uwekezaji hasa huo wa shuruti kwa  kampuni ambazo kimsingi zenyewe  hazikuhitaji bali zinatekeleza wajibu wa kisheria.

Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania Plc, Ian Ferrao, alieleza kwa kifupi kuwa  kampuni yake inasubiri tu kuruhusiwa kutoka Mamlaka ya Hisa, Dhamana  na Mitaji (CMSA), kwani wawekezaji  wapya zaidi ya 40,000 walijiunga nao kwenye IPO.

Juni 26, mwaka huu Baraza la Mawaziri  lilifanya kikao Ikulu Dare Saalam na inasemekana  suala hilo lilikuwa katika ajenda.

Dk. Mpango alieleza bungeni kuwa kama kampuni ikitoa  toleo la mwanzo (IPO)  na haikufanikiwa kupata kiasi kinachotakiwa, wizara  ya sekta husika itahitajika  kutoa  maelezo na kutoa mwongozo kwa kampuni  hiyo namna  gani itapata fedha zinazohitajika kufikia hitaji hilo ili kuridhia mahitaji ya kisheria  kabla ya kufikiria hatua ya kwenda  mbele.

Airtel iko mbioni kwa mwendo kasi kujiorodhesha DSE baada ya wamiliki wake, Serikali na Bharti Airtel kukubali kila upande kuachia asilimia 12.5 ya hisa ili umma uzinunue.

Kampuni ya pili ya mawasiliano kwa ukubwa na umaarufu, Mic Tanzania Limited au Tigo, imekamilisha mipango ya kujiorodhesha ila ina kesi ya dawa ya umiliki mahakamani na hivi karibuni iliruka kihunzi cha kwanza baada ya majaji kung’ang’ania kuendelea kusikia kesi  hiyo kinyume na mahitaji ya mdai.

Alipoulizwa kwenye mkutano na waandishi wa habari kuhusu hatima ya usajili wa kampuni kwenye DSE, Mkuu wa Habari za Kiteknolojia wa Tigo, Jerome Albou, alisema suala hilo liko mahakamani na hawezi kusema litakwisha lini kwani kesi inahusu umiliki na hivyo ni vigumu kwao kwenda sokoni wakiwa na matatizo na hivyo watu wasubiri matokeo ya kesi hiyo.

Albou alieleza kuwa kampuni yake mwaka jana ilitumia dola milioni 75  kuboresha miundombinu  yao na mtandao kwa kuanzisha huduma ya 4G kwenye miji 23 nchi nzima kama walivyopanga awali.

Wakati  huo huo, Maxcom Africa maarufu kama MaxMalipo, imepata  ruhusu na kibali cha CMSA  kubadili jina lake  na kutumia PLC  wakati kampuni nyingine za mawasiliano ziko mguu sawa katika hatua mbalimbali za kujiorodhesha  DSE kwa mujibu wa Sheria ya EPOCA ya mwaka 2010 na Marekebisho ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2016.

Sheria inataka kampuni za simu zote kujiorodhesha DSE ili hisa zake kwa asilimia 25 ziuzwe kwenye soko hilo ili wananchi waweze kununua na kumiliki sehemu ya biashara hizo.

Toleo la IPO  linaonesha kukwama kwani hisa hadi leo hazijapelekwa kwenye soko la upili licha ya IPO kufungwa muda mrefu na kuleta sintofahamu kwa wawekezaji wake na kutishia kuvuna haraka faida kwa wale waliokopa kununua hisa hizo na wale waliosogeza hela za taasisi ili watengeneze chochote kwa muda mfupi.

Airtel au  Bharti Airtel inamilikwa na mfanyabiashara wa India, Mittal Ambani  kwa asilimia 60 na Serikali ya Tanzania hisa  asilimia 40. Taarifa  zinasema  wanahisa hao wamekubaliana kuwa kila mmoja  aachie asilimia  12.5 kuuzwa DSE .

Ambali  alikuja mwenyewe nchini  na jina walikubaliana liwe  Airtel Company Plc na limeshasajiliwa na BRELA  na hivyo kukidhi haja ya ushiriki na kinachosubiriwa ni uchapishaji wa Matarajio ya Toleo (IPO Prospectus)  ambayo inatayarishwa Airtel, yatapitishwa kwanza na DSE, halafu CMSA ambayo ndio itakayotoa kibali cha uuzaji  na ununuzi wa hisa hizo sokoni .

Ni taratibu ndefu lakini ni  kwa usalama wa wale wanaowekeza mitaji. Kampuni  husika zinatakiwa kuwa na uwezo wa kuzalisha faida ili wanahisa wapate gawio.

“Yote haya ni kumlinda mteja anayenunua hisa hizo kuhakikishiwa kupata faida ingawa biashara ina hatari  (risks) nyingi  kutokana na mwenendo wa soko husika,” anasema mtoa  habari DSE.

Hali hiyo imetokea kwenye mauzo ya Hisa za Vodacom Plc ambayo pamoja na kusubiriwa kwa hamu kubwa na wawekezaji, matarajio ya kampuni hiyo hayakwenda vizuri hadi muda wa ziada ulipoongezwa.

Vodacom matarajio yake  hayakufikiwa  kirahisi  kwenye Toleo la awali (IPO)  ya Sh bilioni 476  sawa na $ milioni 213.

Hisa lulu za Vodacom

Ingawa picha kamili ilikuwa  bado  kutolewa hesabu na hatima ya mauzo hayo, kulijaa matumaini kwani vikwazo vya awali vilitolewa na wengi kupata uwezo wa kununua hisa hizo za kihistoria katika soko kwa ukubwa wa toleo la mauzo, kiwango  na kiasi kilichosajiliwa kama bei ya awali ya hisa.

Isitoshe si kawaida kwa hisa za awali DSE kuongezewa muda wa mauzo yake kabla ya kuorodheshwa, tayari ishara zilionesha kwamba mambo si bambam.

Kwa mujibu wa waraka wa matarajio (prospectus), Vodacom Tanzania Plc ina thamani ya Sh trilioni 1.9.

Mkurugenzi Mtendaji wa Orbit Securities, ambao ni washauri wa uwekezaji na wasimamizi wakuu wa mauzo ya hisa za Vodacom, Laurean Malauri, alionyesha imani yake kufanikisha uuzaji huo ingawa imekuwa kwa mbinde.

Malauri amekubali kwamba ukubwa wa thamani ya hisa hizo pamoja na kukosekana kwa ukwasi miongoni mwa Watanzania ambao  ndio waliolengwa kwenye mauzo hayo ni changamoto za msingi.

“Serikali ilitoa upendeleo pekee kwa Watanzania tu kunufaika na hisa za kampuni za simu katika matoleo ya msingi (primary market) na kuzuia  wawekezaji kutoka nje ya nchi ambao wanachangia kiwango kikubwa kwenye biashara ya hisa DSE ikiwamo wale kutoka EAC na  SADC,” alibainisha Malauri.

Hivyo, mpango huo mpya ulioghairi azma ya awali ya Serikali ni mwafaka kwani unatoa nafasi wawekezaji wa nje kugharamia maendeleo ya nchi badala ya kuwa wenyewe pekee.

Mabadiliko hayo ya sera za mitaji kama Dk. Mpango alivyosema yatazuia mkwamo, kwani bado kuna zaidi ya kampuni  nyingine 8 za simu na mawasiliano  pamoja na migodi  mingi zinatakiwa kuuza hisa zake DSE. Swali muhimu ni kuwa fedha zitatoka wapi? Tusipende sana kujikaanga kwa mafuta yetu wenyewe.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here