27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

SINTOFAHAMU UCHAGUZI WA MADIWANI

*Chadema yasusia Arumeru Mashariki, *CCM yashinda kat zote Arusha, *NEC yasema dosari hazikuathiri uchaguzi

Na WAANDISHI WETU-DAR/ MIKOANI


 

NI uchaguzi wa vurugu. Ndivyo unaweza kusema baada ya kuripotiwa baadhi ya matukio ya fujo yaliyotekelezwa na watu wasiojulikana huku mawakala wa vyama vya upinzani wakitolewa kwenye baadhi ya vituo vya kupigia kura.

Maeneo yaliyoripotiwa kukumbwa na vurugu wakati wa uchaguzi mengi yako Mkoa wa Arusha ambako Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuliwataka wagombea wake wa udiwani katika kata zote za Wilaya ya Arumeru kujitoa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema Chadema kinajitoa kwenye uchaguzi wa kata Tano za Jimbo la Arumeru Mashariki huku kikieleza macho kwenye kata 38 zilizobaki.

Mbowe alidai uchaguzi huo wa marudio ulikuwa na matukio ya ukatili na mashambulizi waliyofanyiwa baadhi ya viongozi na wanachama wa Chadema.

Aliwataka vijana wa chama hicho kujitetea wanaposhambuliwa na polisi badala ya kusubiri tamko la chama.

Mbowe alizitaja kata zilizojitoa kuwa ni Ngabobo, Leguruki, Makiba, Maroroni na Mbureni.

“Nimewasiliana na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima ameniambia yuko Tunduru, mambo haya viwango vinatofautiana. Katika hatua ya sasa tumejitoa katika kata tano hizi na tutaendelea kuangalia katika kata nyingine 38 zilizobaki, lakini tunafuatilia kwa karibu matukio haya.

“Kuna matukio mengi ya polisi kuumiza watu na sisi tunachelea kuruhusu vijana wetu kutoka kupiga watu kwa sababu hatuna sababu ya kupiga raia wetu wanapokwenda kutekeleza wajibu wao.

“Lakini tunapenda kuwaambia vijana wetu popote walipo wasikunje uso wanapoendelea kupigwa au wanapofanyiwa mashambulizi basi wajitetee, watafute utaratibu wa kujitetea wasisubiri tamko la chama, wajitetee kunusuru maisha yao,” amesema Mbowe.

Mbowe alisema mambo hayo yana mwisho wa uvumilivu kwa sababu vyombo vya dola vinatumika vibaya huku polisi wakishuhudia.

“Kamanda Mkumbo (Charles Mkumbo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa arusha) anajua yote haya, kama hajui hastahili kuwa ofisini lakini vijana wake ndiyo wanaongoza vijana wa ‘green guard,’ wanapiga watu, wanaumiza, wanakata mapanga, wanateka watu wanateka vuongozi.

“Arumeru hakuna uchaguzi kuna upumbavu na upuuzi ni fujo tu na zimasimamiwa na vyombo vya dola. Sisi kwa hali hii inayoendelea Arumeru tunawaagiza viongozi wetu wa chama na madiwani wetu haraka sana wajitoe.

“Mawakala wetu ambao wamekuja vituoni mchana huu waondoke wote waachanae na uchaguzi huu wa kikatili, tuwaachie wao waendelee na viongozi wote Chadema wasiende kwenye majumuisho ya kura hizi ambazo haziakisi maamuzi ya wanachi ama utashi wa wananchi,” alisema Mbowe.

 

Mgombea ageuka wakala

 

Mgombea udiwani wa Kata ya Mamba Wilaya ya Lushoto, Jafari Ngede (Chadema),  alilazimika kuwa wakala mwenyewe baada ya mawakala kutolewa katika vituo 13.

“Mimi Mgombea Udiwani Jafary Ndege, Kata ya Mamba Mawakala wangu wote katika vituo 13 vyote wameondolewa na kupelekwa Polisi mida ya saa 4:00 asubuhi.

“…na imenibidi nikae katika kituo kimoja wapo kama wakala na polisi wamekuja kunitishia hapa kuwa niache kiherehere,” alisema Ndege.

 

MKOA WA SONGWE

Mwandishi wetu Eliud Ndondo anaripoti kutoka Songwe kuwa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba, Methew Kikoti (CCM) na Mbunge wa Momba, David Silinde (Chadema), jana walitunishiana misuli.

Tukio hilo lilitokea jana katika kituo cha kupigia kura cha Shule ya Msingi Kakozi, Kata ya Ndalambo wakati wa uchaguzi mdogo wa udiwani.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, mzozo ulianza baada ya Silinde kumuona Kikoti akitoka kwenye chumba kimoja cha kupigia kura na kuingia chumba cha pili.

 

Ilielezwa kuwa Silinde alimuuliza mwenyekiti huyo kwanini aliingia kwenye chumba cha kupigia kura wakati hairuhusiwi.

Kwamba baada ya swali hilo walianza kurushiana maneno ya kejeli na kashfa.

Majibishano baina ya Silinde na Kikoti yalikuwa hivi;

Silinde: Wewe Kikoti nani kakuruhusu kuingia kwenye chumba cha kupigia kura?

Kikoti: Nimeingia ili kuwaona mawakala wangu hivyo sina kosa lolote.

Silinde: Hujui kuwa ni kosa kuingia kwenye chumba cha kupigia kura wakati wewe siyo mhusika?

Kikoti: Mimi ndiye Mwenyekiti wa Halmashauri, ninapaswa kuangalia zoezi linavyofanyika na siyo vinginevyo.

Silinde: Mimi ndiye niliyechanguliwa na wananchi wa jimbo hili, lakini siruhusiwi kuingia, kwanini wewe uliyechaguliwa na madiwani uingie ndani ya chumba cha uchaguzi?

Kikoti: Waliopaswa kuniuliza maswali hayo ni wasimamizi siyo wewe ambaye ni sawa na mimi.

Silinde: Ndiyo maana mwenyekiti mzima hujui kusoma hata taratibu za uchaguzi huzifahamu.

Kikoti: Uliyesoma ungekuwa na busara hata ya kumuuliza mwenzako na siyo kuropoka maneno yasiyokuwa na maana kwenye uchaguzi.

Pamoja na majibizano hayo, Silinde aliwaagiza mawakala wa chama chake kuhakikisha wanajaza fomu za Kikoti kuingilia mwenendo wa uchaguzi.

Wakati huo huo, mgombea wa CCM, Flovian Sichzyan, alitangazwa mshindi kwa kupata kura 1402 dhidi ya Mgombea wa Chadema, Michael Kuyange, aliyepata kura 1298.

IRINGA

Mkoani Iringa katika Kata ya Kimara, wanachama kadhaa wa Chadema akiwamo Katibu wa Baraza la Wanawake wa chama hicho (Bawacha), Grace Tendega, walikamatwa na Jeshi la Polisi.

Wengine waliokamatwa ni  Diwani wa Kata ya Ikula, Raymond Francis aliyedaiwa kufanya kampeni kinyume cha taratibu, Frank Nyarusi ambaye ni Mwenyekiti wa madiwani wa Chadema Mkoa wa Iringa, na madiwani wengine watatu na viongozi wanne wa Chadema ambao majina hayakupatikana.

Tendega na wenzake walikamatiwa katika Kijiji cha Muhanga waliokuwa wameweka kambi yao.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Diwani wa Kata ya Nyalumbu, David Mfugwa (Chadema), alisema wanachama wenzake hao walikamatwa jana majira ya saa sita mchana na kupelekwa katika Kituo cha Polisi Kilolo kwa madai kwamba gari lao lilikwaruza gari la CCM, aina ya Land Cruiser.

“Inasemekana baada ya dereva wetu kukwaruza gari la CCM, alikimbia akaenda kujificha katika kambi yetu iliyokuwa na viongozi hao. Kwa hiyo, polisi walipofika ili kumkamata deerva huyo, aliwakamata na wengine waliokutwa mahali hapo,” alisema Mfungwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Julius Mjengi, alipozungumza na MTANZANIA kwa simu yake ya kiganjani alisema hana taarifa za kukamatwa kwa viongozi hao na kuahidi kufuatilia.

 

MOROGORO

 

Mkoani Morogoro katika Kata ya Sofi, Wilaya ya Malinyi, watu 11 wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chadema, walimakatwa akiwamo mgombea udiwani wa chama hicho, Riko Venance.

Akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Urlich Matei, alisema watu hao walikamatwa jana asubuhi wakati wakijindaa kufanya vurugu katika vituo vya kupigia kura.

“Kwa hiyo bado tunaendelea kuwahoji na watakapobainika kuwa na makosa basi tutawafikisha katika vyombo vya sheria.

Katibu wa Chadema Mkoa wa Morogoro, Samuel Kitwika, aliliambia MTANZANIA kuwa waliokamatwa walikuwa wakikagua vituo vya kupigia kura na mawakala wao.

“Kwa mfano, Mgombea Riko Venance alikamatwa wakati akitembelea vituo kuona uwepo wa mawakala wake na mwenendo mzima wa uchaguzi,” alisema .

 

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Sudi Mpili, alisema uchaguzi katika Kata ya Kiloka, ulifanyika kwa utulivu na kukamilika saa 10: 28.

 

Alisema, awali kulitokea malalamiko katika baadhi ya vituo ambako mawakala walibadilishwa na kusababisha hali ya kutoelewana kwa vyama vilivyokuwa na wagombea.

 

“Lakini, baadaye kasoro hizo zilitatuliwa kwa mawakala wengine kuapishwa na uchaguzi ukaendelea kama kawaida,” alisema Mpili.

 

MKOA WA MBEYA

 

Mkoani Mbeya katika Kata ya Ibigi, wilayani

Rungwe, uchaguzi huo ulifanyika katika hali ya amani na utulivu

 

Katika kata hiyo, baadhi ya wabunge wa Chadema akiwamo Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu na Mbunge wa Viti Maalum, Sofia Mwakagenda waliweka kambi katika kata hiyo kuangalia mwenendo wa uchaguzi.

 

Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Rungwe, Sam Mwakapala hakupatikana kuzungumzia uchaguzi huo baada ya simu yake kuita bila kujibiwa.

 

Kata ya Ibighi

Katika Kata ya Ibighi wilayani Rungwe, Chadema imefanikiwa kutetea kiti chake babada ya mgombea wake, Goffrey Mwakajoka kupata kura 1436 dhidi ya 1205 za mpinzani wake, Suma Fyandomo wa CCM.

 

KILIMANJARO

 

Wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro katika Kata ya Machame Magharibi  iliripotiwa kuwa uchaguzi ulifanyika katika hali ya utulivu.

 

Hata hivyo taarifa zilisema katika vituo vya kupigia kura kulikuwa na wapiga kura wachache tofauti na ilivyotarajiwa.

 

Matokeo yaliyofikia MTANZANIA jana kutoka Kata ya Machame yalionyesha kuwa mgombea wa CCM, Martine Munisi alishinda kwa kura 1058 dhidi ya Mgombea wa Chadema, Elibariki Lema aliyepata kura 590.

 

Katika Kata ya Weluwelu, Swalehe Msengesi wa CCM alitangazwa mshindi kwa kupata kura 1454 dhidi ya kura 716 alizopata Mgombea wa Chadema, Moses Kalaghe.

 

Kata za Mnadani na Bomang’ombe, Manispaa ya Moshi,  hadi tunakwenda mitamboni matokeo yalikuwa hayajatangazwa ingawa wagombea wa CCM waliripotiwa kuongoza.

 

MKOA WA SINGIDA

 

Taarifa zinasema uchaguzi ulifanyika katika Kata ya Siuyu, Jimbo la Singida Mashariki katika hali ya amani na utulivu.

 

Hadi tunakwenda mitamboni taarifa zilieleza kuwa wagombea wa CCM na Chadema walikuwa wakichuana kwa karibu.

 

MKOA WA TANGA

 

Katika Kata ya Majengo wilayani Korogwe, Msimaizi wa Uchaguzi, Jumanne Shauri, alimtangaza Mgombea wa CCM, Mustafa Shengwatu kuwa mshindi baada ya kupata kura 583 dhidi ya kura 22 alizopata Mgombea wa Chadema, Abas Chomboka.

 

Mwandishi wetu kutoka mkoani Tanga anaripoti kuwa katika Kata ya Mamba Jimbo la Bumbuli, mgombea wa CCM alishinda kwa kupata kura 1373 dhidi ya kura 700 alizopata mgombea wa Chadema.

 

MKOA WA MTWARA

 

Mwandishi wetu kutoka Mtwara anaripoti kuwa katika Kata ya Milongodi wilayani Tandahimba mgombea CCM, Manzi Livedo alipata kura 827 dhidi ya kura 819 za mgombea wa CUF, Juma Mgawa huku Selemani Likome wa ACT akiambulia kura 2.

 

Taarifa zilizopatikana kutoka Masasi, Kata ya Chanikanguo zilieleza kuwa mgombea wa CCM alishinda kuwa kupata kura 928, CUF 36 huku mpinzani wake wa ACT Wazalendo kura 10.

 

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Masasi, Mkoa wa Mtwara, Gimbana Ntavyo zaidi ya watu  3316  walijiandikisha lakini hadi majira ya mchana waliokuwa wamejitokeza kupiga kura ni 1727.

 

Taarifa hiyo ilieleza kuwepo kwa changamoto kadhaa  ikiwemo ya mawakala wa vyama vya siasa kutopewa utaratibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kusababisha watake kufanyakazi za wasimamizi walioandaliwa na Tume.

 

Matokeo ya awali yaliyolifikia MTANZANIA kutoka Kituo cha Mailisita yalionyesha mgombea wa Chadema alipata  kura 155, CCM 89, na CUF 03 na ACT haikuambulia kitu.

 

MKOA WA DODOMA

 

Taarifa kutoka Mpwapwa katika Kata Chipogoro zilionyesha  kuwa matokeo ya awali kwenye Kituo cha Zahanati namba 3 , Hosea Fweda wa CCM alipata kura 129 huku Jafari Simba wa Chadema akiwa na kura 103.

Kituo cha Zahanati namba 2, Hosea Fweda wa CCM alipata kura 131 na  Jafari Simba  wa Chadema alipata 91 na kituo cha Zahanati namba moja, mgombea huyo wa CCM alikuwa akiongeza kwa kura 109 dhidi ya 94 za yule wa Chadema.

Wakati huo huo, mwandishi NORA DAMIAN anaripoti akiwa Dar es Salaam kuwa  Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), jana ilieleza kuwa licha ya kuwapo kwa changamoto ndogondogo katika maeneo mengi uchaguzi umefanyika kwa amani.

Akizungumza jana na MTANZANIA, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima alisema kasoro chache zilijitokeza mkoani Arusha na kusababisha kuondolewa kwa baadhi ya mawakala katika kata tatu.

 

“Changamoto haziwezi kukosekana hali iko vizuri ukiondoa kasoro chache zilizojitokeza Arusha, hata kwenye familia kama una watoto lazima watatokea wawili watakosana.

 

“Arusha wabunge waliwaondoa baadhi ya mawakala kwenye kata tatu lakini walikuwa wanaendelea na uchaguzi,” alisema Kailima.

 

Alifafanua kuwa kiutaratibu kila wakala lazima awe na barua ya chama, fomu ya kiapo namba sita barua ya msimamizi ya kumtambulisha kuwa wakala.

 

“Kama Bumbuli (Tanga) kuna watu waliapishwa kama mawakala lakini leo asubuhi (jana) wamekwenda watu wengine,” alisema Kailima.

Mkurugenzi huyo pia alikiri kutokea kwa vurugu katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Mwanza na kutadharisha kuwa watu wasikimbilie kufanya fujo na kama kuna mambo yamekiukwa wafuate taratibu za kisheria.

“Tuanze kujihurumia na kuihurumia nchi yetu, tujiulize tunafanya vurugu kwa faida ya nani? alihoji Kailima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles