32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

SIMULIZI YA UTAWALA WA MOI KUPOTEZA MADARAKA (1)


NAIROBI, KENYA

ILIKUWA Disemba 29, 2002 kwenye Hoteli ya Nairobi Serena, mjini Nairobi ambako tukio la kihistoria lilishuhudiwa.

Ni pale mgombea urais wa kilichokuwa chama tawala tangu uhuru cha Kanu nchini Kenya, Uhuru Kenyatta alipokubali kushindwa na kumpongeza mgombea wa upinzani kutoka muungano wa National Rainbow Alliance (NARC), Mwai Kibaki.

Miongoni mwa waliosimama kando ya mtoto huyo wa muasisi wa Taifa la Kenya, Jomo Kenyatta walikuwa mawaziri William Ruto na Chris Okemo.

Wengine ni wabunge wateule walioshinda katika uchaguzi wa kipindi hicho, Musa Sirma, Njenga Karume, Patrick Muiruri na bosi wa zamani wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Jos Konzolo.

Ambao hawakuonekana katika tukio hilo ni pamoja na mgombea mwenza wa kijana huyo na aliyewahi kuwa makamu wa rais, Musalia Mudavadi ambaye alikuwa amepoteza kiti chake cha ubunge wa Sabatia kwa mwanasiasa mpya, Moses Akaranga.

MATESO

“Nachukua fursa hii kumshukuru Rais (Daniel arap) Moi kwa kuniunga mkono bila kuchoka na jukumu lake zito la kukabidhi madaraka kwa utulivu na amani,” Kenyatta aliliambia taifa.

Tukio hili lililotokea miaka 16 iliyopita, lilimaanisha mwisho wa kusisimua wa utawala wa miaka 24 wa Moi aliyezitawala siasa za Kenya.

Pia lilifungua milango kwa Kibaki na muungano wa NARC ulioongozwa na Raila Odinga.

Lakini, kisichojulikana na wengi, tukio hilo liliashiria mwanzo wa mateso kwa Moi ambaye utawala wake uliishia mikononi mwa Kibaki, aliyewahi kuwa makamu wake wa rais.

USHINDI WA KISHINDO

Awali siku mbili kabla, yaani Disemba 27, Wakenya walikuwa katika vituo vya kupiga kura katika moja ya chaguzi zilizosubiriwa na kufuatiliwa kwa karibu zaidi katika millennia mpya.

Kufikia alasiri ya siku iliyofuata ya Disemba 28, ilikuwa wazi Kibaki alikuwa akielekea kupata ushindi wa kishindo.

Mapema alasiri ya siku iliyofuata, yaani Disemba 29, Kenyatta alikubali kushindwa.

Na jioni ya siku hiyo, Tume ya Uchaguzi ya Kenya ikamtangaza Kibaki kuwa rais mteule.

Baada ya hapo, viongozi wa upinzani walitoa mwito wa kuapishwa mara moja kwa Kibaki siku iliyofuata ya Disemba 30 na kusababisha uwapo wa moja ya shughuli ya hovyo kabisa ya kirais kushuhudiwa nchini Kenya.

MAKABIDHIANO YA MADARAKA

Kilichojiri hiyo Disemba 30, wakati Kibaki alipoapishwa kama rais wa tatu wa Kenya, hadi leo hii bado ni sehemu ya mjadala mchungu baina ya kambi za Moi na Kibaki.

Kwa mujibu wa katibu wa habari wa muda mrefu wa Moi, Lee Njiru, rais alilazimika kuelekea Bustani ya Uhuru na kukabidhi madaraka kwa Kibaki ili kuepusha mgogoro wa kisiasa ulioonekana ukinukia.

Njiru, ambaye mwaka huu anatimiza miaka 40 ya kumtumikia rais huyo mstaafu, alisema timu ya makabidhiano ya madaraka ya Kibaki kwa makusudi kabisa ilimweka Moi gizani juu ya muda na tarehe ya sherehe za kuapishwa zilipangwa kufanyika kwa malengo yaliyojificha.

NJAMA OVU

“Kulikuwa na njama ovu kutengeneza hisia za uongo kuwa Mzee Moi alikataa kuondoka madarakani,” alisema Njiru wakati wa mahojiano katika makazi yake huko Ngata, Kaunti ya Nakuru hivi karibuni.

Njiru alisema siku hiyo timu ya Kibaki ikifahamu fika ni ya kuapishwa kwake, iliendelea kumwambia Moi kuwa bado hawajawa tayari kwa sherehe ya makabidhiano na hivyo abaki Ikulu kusubiri maagizo.

Alidai Moi alipata siri za kiintelijensia kuwa baadhi ya viongozi wa upinzani kwa makusudi walitaka kutumia kukosekana kwake kama kigezo cha kuivamia Ikulu na kumtimua kwa nguvu.

UASI

“Walilenga kumuumiza mzee na kudai kuwa tukio hilo lilikuwa uasi wa kishujaa,” alisema Njiru ambaye alikataa kutaja viongozi waliokuwa nyuma ya njama hizo kwa sababu baadhi yao bado wako katika siasa au wanaitumikia Serikali bado.

Ilipofika saa za alasiri ya siku hiyo, Moi aliishiwa uvumilivu na kuagiza timu yake ya wana usalama kumpeleka Uhuru Park kukabidhi madaraka kwa mtangulizi wake.

“Alituambia kwamba bila kujali iwapo timu ya Kibaki iko tayari au la, kwa itifaki au bila itifaki, lazima ahudhurie sherehe hizo ili kuliokoa taifa dhidi ya umwagaji damu uliokuwa ukinukia,” anakumbushia.

VITISHO

Msafara wa Moi ulilazimika kupenya umati uliokuwa ukipiga kelele za vitisho zikiwamo za kuua na kupaza sauti kwa Kiswahili: “Yote yawezekana bila Moi” ili kufikia jukwaa walilokaa viongozi mashuhuri.

Akielekea hapo, umati ulisikika ukimwita Moi mwizi na kumrushia madonge ya udongo wakati akipanda jukwaani kwenda kumsalimia Kibaki.

Mkuu wa Utumishi wa Umma, Sally Kosgei aliondoka katika sherehe hiyo yenye vurugu akiwa hana kiatu.

Wakati wa sherehe hiyo, Moi hakuruhusiwa kuwaaga watu aliowaongoza tangu mwaka 1978.

Kipindi chote cha hotuba ya kuapishwa kwa Kibaki, ambayo kwayo alisema ameirithi nchi iliyoharibiwa na miaka mingi ya utawala mbovu na usio na ufanisi, kamwe hakuweka neno lolote la kumsifu mtangulizi wake aliyekaa kando yake akiwa hana kinyongo cha kustaafu.

“Uzoefu wake wa nyuma wakati watu waliomzunguka Mzee Jomo Kenyatta walipoanza kula njama dhidi yake kumzuia asiwe rais katika miaka ile ya 1970 kulimwandaa kabisa kwa matukio hayo ya Uhuru Park,” alisema Njiru.

Lakini kwa mujibu wa Joseph Munyao, waziri wakati wa muhula wa kwanza wa Kibaki, hali ya fedheha iliyoshuhudiwa siku hiyo ilitokana na kukosekana kwa uratibu baina ya kambi za Kibaki na Moi.

HOFU

“Moi kamwe hakuona kushindwa kukiwa njiani,” alisema Munyao, mbunge wa zamani wa Mbooni na mwanachama mwasisi wa chama cha zamani cha Kibaki, DP.

Aliongeza kuwa “Hatukuwa na tatizo naye. Ni yeye aliyetutia hofu.”

Ushindi wa Kibaki dhidi ya chaguo la Moi ulihitimisha utawala wa miaka 39 wa Kanu na kuleta hali ya shangwe na msisimko katika sehemu kubwa ya nchi.

Kabla ya sherehe ya Uhuru Park, hakukuwa na mtu aliyekuwa na uhakika iwapo Moi angekabidhi madaraka kwa upinzani kama Katiba ilivyotaka, hali ambayo ilisababisha matayarisho holela ya sherehe za kuapishwa kwa mrithi wake, siku tatu tu baada ya uchaguzi.

KUKWEPA UPORAJI

Munyao alisema walilazimika kuendesha shughuli za kukabidhi madaraka katika muda huo mfupi kwa sababu hakukuwa na mtu aliyekuwa na uhakika nini Moi alikuwa anapanga.

“Tunafahamu kile alichotufanyia DP mwaka 1997,” alisema, akirejea matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita ambao Moi alishinda huku kambi ya Kibaki ikilia kuwa ushindi wao uliporwa.

“Tulidhamiria kutorudiwa kwa tukio hilo la uporaji.

“Tulikuwa tumejipanga kumwapisha Kibaki bila kujali kitakachotokea. Lakini si kweli kwamba eti hatukupanga uwepo wa Moi Uhuru Park siku hiyo.” alidai Munyao

Lakini msemaji wa Moi, bado anasisitiza maelezo yake kuhusu kilichotokea siku hiyo.

“Ilipaswa kuwa siku na tukio la kusherehekea demokrasia, lakini iligeuka siku ya aibu na kuumizana,” alisema Njiru (77).

Tangu aondoke madarakani, Moi hajawahi kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu kukabidhi kwake madaraka.

Mtazamo wa msemaji wake pengine ni karibu na ukweli utakaokuja julikana kuhusu matukio yaliyojiri alasiri ile.

 

Makala hii imetafsiriwa kutoka gazeti la Nation la Kenya

 

Itaendelea kesho

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles