PATRICIA KIMELEMETA NaCHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM
SIMU ya Kiongozi Mkuu wa Chama Cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, imechukuliwa na polisi kwa ajili ya uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkali.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini, anadaiwa kutoa taarifa za takwimu za uongo na kuzisambaza katika mitandao ya jamiii.
Zitto alikuwa akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana baada ya kumaliza mahojiano kwenye Kituo cha Polisi cha Kamata katika kitengo kinashughulika na uhalifu wa fedha na mtandao.
Alisema polisi waliamua kuchukua simu hiyo kuangalia mawasiliano yake ikiwamo kudaiwa kusambaza takwimu za uongo kwenye mitandao ya jamii ikiwamo Twitter.
Alisema kwa sababu kitengo hicho kinashughulika na makosa ya mtandao (Cyber Crime), wanapaswa kuchukua simu hiyo waweze kujiridhisha na wanachodhani.
“Nitakua nje ya mawasiliano kwa muda kidogo mpaka polisi watakaponirudishia simu yangu kwa sababu ni haki yao kuchukua mawasiliano yangu na kuyafanyia uchunguzi wanapoona kuna shaka,” alisema Zitto.
Alisema kwa sababu kosa wanalomtuhumu la kudai kuwa alitoa takwimu za uongo na kuzisambaa limejikita kwenye mitandao ya jamii, hali inayowaruhusu kutekeleza majukumu yao.
Zitto alisema kwa sababu hiyo, watu watakaomtafuta kwa kipindi hicho wanapaswa kujua kuwa hana mawasiliano yoyote ya simu mpaka polisi watakapomaliza kazi zao na kumrudishia.
Akizungumzia kuhusu kutenguliwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bukoba Erasto Mfugale na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Vijijini, Mwantumu Dau, alisema ni udhalilishaji.
“Rais anaweza kuwakatisha tamaa watendaji wake kutokana na kitendo chake cha kuwaita hadharani na kuwatumbua hata kama ana mamlaka ya sheria,” alisema.
Zitto ametakiwa kurudi kituoni hapo Novemba 21.