30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Simbu: Tanzania kupata medali Olimpiki inawezekana

IMG_1677

Na WINFRIDA NGONYANI-DAR ES SALAAM

ILIKUWA Februari 2, mwaka 1974, katika mbio za mita 1,500 upande wa wanaume kwenye fainali za mashindano ya Jumuiya ya Madola nchini Christchurch, New Zealand ambapo Filbert Bayi alitumia dakika 3 na sekunde 32.16.

Akiongoza kuanzia mwanzo wa mbio hizo hadi mwisho, Mtanzania pekee aliyeweka rekodi duniani, Filbert Bayi, alimaliza mbio hizo ambazo zinaelezwa kuwa ni miongoni mwa mashindano makubwa duniani.

Mwanariadha huyu nyota nchini, aliyezaliwa katika mkoa ulioko maeneo ya Bonde la Ufa (Rift Valley), Arusha maarufu kwa kutoa wanariadha wazuri hapa nchini, anasema hali ya hewa na mfumo wa maisha ya watu wa mkoa huo unachangia kutoa maarifa kwa wakimbiaji wa mbio ndefu.

“Wazazi wangu walikuwa wakulima, wafugaji wa ng’ombe, nilipokuwa mtoto, nilikuwa naangalia mbuzi na ng’ombe, nikiwa kwenye vichaka nachunga mifugo, nawinda, nakimbia na mbwa, nakimbia na wanyama, nafikiri hiyo ndiyo iliyonifanya niwe na stamina katika ukimbiaji.

“Kila asubuhi nilikuwa nakimbia  kwenda shule  na natakiwa kurudi kwa chakula cha mchana, kisha natakiwa kurudi tena kwa masomo ya jioni, hivyo unaweza  kuhisi nilikuwa nakimbia kilomita nane kwa siku,” anasema  Bayi.

Kauli hii ya Bayi inaakisi matokeo ya riadha ya mwanariadha, Alphonce Felix Simbu, kutoka Mkoa wa Singida aliyeshiriki mashindano ya Olimpiki mwaka huu na kuibuka mshindi wa tano.

Simbu mwenye umri wa miaka 24, ameweka historia kwa taifa kwa kushika nafasi ya tano, akitumia muda saa 2:11:15 katika mbio ndefu ‘marathon’ akiwaacha wanariadha 155 walioshiriki mbio hizo, lakini hakuweza kupata medali yoyote.

Kabla ya kuelekea nchini Rio de Jeneiro, Brazil, kushiriki michezo hiyo, Simbu amekuwa akijituma sana katika mazoezi na mke wake, Rehema Daudi, anasema: “Kila siku huwa anafanya mazoezi asubuhi na kwenye maeneo haya ya jirani na nyumbani na hasa maeneo ya milimani na amekuwa akifanya hivyo kila siku,” alisema Rehema.

Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Antony Mtaka, anasema kabla ya kuelekea kwenye michezo ya Olimpiki, Simbu aliweka kambi miezi sita katika Chuo cha Wakala wa Misitu (FITI), kilichopo Siha mkoani Kilimanjaro chini ya kocha wake, Fransic John, baada ya kufikia viwango vinavyotakiwa na Shirikisho la Dunia la mchezo huo (IAAF).

Mfumo huo wa maisha ambao Bayi anasema unachangia kuwawezesha wanariadha kufanya vizuri hivi sasa unatoweka na hivyo wanariadha wanatakiwa kufanya mazoezi kwa mtindo wa kisasa.

Akizungumza na MTANZANIA SPOTIKIKI kuhusu wanamichezo walioshiriki michezo ya Olimpiki iliyomalizika, Bayi anasema tunahitaji uwekezaji wa kutosha iwapo tunataka kufanikiwa katika michezo  kwani  wanamichezo wetu hawakuwa na maandalizi ya kutosha.

Licha ya mwanariadha, Simbu kufanya vizuri kwa kushika nafasi ya tano, Mkenya, Eliud Kipchoge, alishinda mbio hizo na kutwaa medali ya dhahabu.

Bayi ambaye ni Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki nchini (TOC), anasema tunatakiwa kuwekeza kwa wanamichezo kwa kuweka programu za muda mrefu kwa kuandaa wachezaji.

Anasema hatuwezi kufanya vizuri kama wenzetu wa nchi zilizoendelea kama Marekani, Ufaransa, Ujerumani kama hatutapata makocha wenye uwezo na viwango vya kimataifa.

Aidha, Bayi anasema wachezaji wanatakiwa kuandaliwa kwa muda mrefu kabla ya kwenda kushiriki katika mashindano ya kimataifa.

Licha ya mwanariadha huyu kijana kutoka Singida Kijiji cha Mampandu, kufanya vizuri kwa kushika nafasi ya tano, Bayi amedai tunahitaji uwekezaji mkubwa katika riadha kwa kuandaa vijana wakiwa na umri mdogo na kwa muda mrefu.

Kama anavyosema Juma Ikangaa ambaye alitamba katika Olimpiki ya mwaka 1984 huko Marekani ambapo alishika nafasi ya sita akikimbia saa 2:11:10 na ile ya mwaka 1988 huko Soul, Korea akikimbia saa 2:13:06 na kushika nafasi ya sita.

Wanariadha wenye historia ya kufanya vizuri katika mashindano makubwa hapa nchini ni kama Bayi, Seleman Nyambui na Ikangaa ambao rekodi zao zimekuwa nadra sana kufikiwa na wanariadha wetu hapa nchini.

Kiwango alichofikia mwanariadha huyu kijana ni kukimbia muda wa saa 2:19:00 alipokuwa akipeperusha bendera ya Tanzania katika michezo ya Lake Biwa, iliyofanyika Desemba mwaka jana huko nchini Japan.

Hata hivyo, mwanzoni mwa mwaka huu, Simbu alivunja rekodi yake mwenyewe pale aliposhika nafasi ya 3 katika mashindano hayo kwa kutumia saa 2:09:19 hivyo kufuzu moja kwa moja katika michezo ya Rio mwaka huu.

Dalili za Simbu kufanya vizuri zilianza kuonekana tangu akiwa hapa nyumbani, baada ya kujitosa katika mbio za Bagamoyo Marathon siku chache kabla hajaelekea Rio, ambapo alishika nafasi ya kwanza.

Katika mbio hizo za Bagamoyo kwa upande wa wanaume kilomita 21, Simbu kutoka Arusha aliibuka mshindi akitumia saa 1:03:56, ambapo kwa asilimia kubwa mbio hizo ziliongozwa na wanariadha wengi kutoka Arusha.

Katika mbio hizo za Bagamoyo, Simbu alikuwa na Mtanzania Saidi Makula aliyeshika nafasi ya nne, ambaye yeye katika Rio 2016 alishika nafasi ya 43 hiyo ikiwa ni baada ya kufikia viwango kwa kukimbia marathon kwa saa 2:13:25 mjini Casablanca, Morocco Oktoba mwaka jana.

Na ndoto yake ilitimia Aprili 3 mwaka huu aliposhiriki  marathon ya Daengu, Korea baada ya kukimbia kwa saa 2:12:01.
Simbu anasema haikuwa rahisi kwake kushika nafasi hiyo kama watu wanavyofikiria kwani alikuwa akikimbia huku akiwa na wanariadha mashuhuri na wakongwe katika riadha, hivyo kuziona mbio hizo ngumu sana kwake lakini hakukata tamaa.

“Sitakuja kusahau pale nilipofika km 20 nikiwa sambamba na Kipchoge, aisee jamaa huyu anakimbia  mbio za mwendokasi na kama ningejaribu kushindana naye basi ningechemka na kubaki mwishoni, lakini niliona ni bora niende na kasi ile ile niliyokuwa nayo na hatimaye nilifanikiwa kushika nafasi hii,” anasema

Mwanariadha huyu anaongeza kuwa amejifunza mambo mengi ambayo amesema kwa kiasi kikubwa yatamsaidia katika Olimpiki ijayo hapo mwaka 2020 huko Tokyo, Japan hivyo kutoa wito kwa Serikali kuhakikisha inaanza sasa kampeni ya kutafuta medali.

“Hii ni mara yangu ya kwanza kushiriki lakini nimeweza kupambana kufa kupona naamini kuwa kama Serikali itatuandaa mapema na kambi yetu ikiwa ya kisasa tena ikiwezekana nje ya nchi nina uhakika medali itakuja Tanzania,” alisisitiza mwanariadha huyu na kuongeza:

“Vita ya kusaka medali ianze sasa hivi na si kusubiri wakati mashindano yanakaribia, nimegundua kuwa wanamichezo wengi waliokuwa Rio waliandaliwa vizuri sana na nchi zao na ndio maana wamepata medali na kama walizikosa basi walishika nafasi za juu,” anaongeza Simbu.

Wanariadha wengine ambao nao walishiriki katika michezo ya mwaka huu ni pamoja na mwanamke pekee, Sara Ramadhani ambaye alishika nafasi ya 126 yeye akidai kuwa viongozi wake walimtelekeza akiwa kwenye mbio hizo na kujikuta akiwa mwisho huku akikosa maji.

Saidi Makula ambaye na yeye alipambana na kushika nafasi ya 43, anasema mbio hizo ni ngumu hivyo zinahitaji maandalizi ya kutosha na si kama alivyojiandaa yeye.

Wakati Fabiano Joseph aliyeshika nafasi ya 112, anadai kabla ya kwenda nchini humo miezi miwili kabla alipata matatizo ya mguu hivyo aliposhiriki mbio hizo alitonesha mguu wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles