Asha Kigundula-Dar es Salaam
MABINGWA
watetezi Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba ambayo ni wazi ina kiu ya kutaka kutwaa tena taji hilo, leo inashuka
dimbani kuumana na KMC, katika mchezo utakaochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar
es Salaam.
Mchezo huo umepangwa kuanza saa 1 usiku, ukitarajiwa kuwa na upinzani wa hali
ya juu, kwani kila timu inafahamu umuhimu wa pointi tatu ili kutimiza malengo
yake msimu huu.
Simba inayofundisha na Sven Vandenbroeck, imekuwa katika kiwango cha juu katika michezo yake kadhaa ya hivi karibuni, kiasi cha kuwatisha wapinzani wake.
itaingia dimbani ikihitaji pointi tatu muhimu za mchezo huo, ambazo sio nyepesi kutokana na wapinzani wao wakihitaji pointi hizo kutoka kwenye eneo la hatari.
Simba itaingia na kumbukumbu nzuri ya kuitandika KMC mabao 2-0, katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Kikosi cha vinara hao kinashuka uwanjani kikihitaji kupata ushindi kuendeleza harakati zake za kutetea ubingwa wao, ambao unayemelewa pia na Azam, Namungo pamoja Yanga ambazo zinaifukuzia kwa karibu.
Simba imetoka kushinda mchezo wao wa Kombe la Shirikisho(ASFC) na kutinga hatua ya robo fainali, hivyo itakuwa na mzuka wa hali ya juu.
Inakutana na KMC yenye hasira za kufungashiwa virago na Kagera Sugar katika michuano hiyo.
Kikosi cha Sven kimeshuka dimbani mara 24, kikishinda michezo 20, sare mbili na kupoteza mechi mbili.
Kocha wa KMC Haruna Harerimana, ana kazi ya ziada ya kuhakikisha kikosi chake kina pambana kupata matokeo mazuri dhidi ya vinara hao wa Ligi Kuu, hasa kwakua hkwa sasa hakiko kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Katika msimamo wa ligi hiyo, KMC ipo nafasi ya 19 miongoni mwa timu ishirini zinazochuana katika ligi hiyo, baada ya kushuka dimbani mara 24, kikishinda michezo mitano, sare sita na kuchapwa mara 13, hivyo kujikusanyia pointi 21.
Endapo itapata ushindi katika mchezo huo wa leo itatoka katika nafasi hiyo itazishusha Mbao iliyoko nafasi ya 18 na pointi 22 na Mwadui inayokamata nafasi ya 17, ikiwa pia na pointi 22, kwani itakuwa imefikisha pointi 24.
Nahodha wa Simba John Bocco aliliambia gazeti hili kuwa, yeye pamoja na wachezaji wenzake wanahitaji pointi tatu ili kuzidi kujisafisha njia ya kwenda kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
“Tunahitaji matokeo mazuri ya pointi tatu katika mechi yetu na KMC na wachezaji wote apo tayari kuwavaa wapinzani wetu hao,”alisema Bocco.