Na Mwandishi Wetu
Klabu ya Simba leo Desemba 5, 2023 imekabidhi msaada kwa ajili ya wahanga wa mafuriko na maporomoko yalitokea katika Wilaya ya Hanang mkoani Manyara mwishoni mwa juma lililopita.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’, amemkabidhi msaada huo kwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro ambaye ataepeleka kwa wahusika huko Hanang.
“Kwa niaba ya Rais wa heshima Mohamed Dewji, Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti wapenzi na wanachama wa Simba tunapenda kutoa pole nyingi kwa wahanga wa mafuriko na maporomoko huko Hanang.
“Wengi wa wahanga hawa ni wapenzi wa soka na sisi kama klabu tunaungana nao katika kipindi hiki kigumu,” amesema Try Again.
Akipokea msaada huo, Waziri Dk. Ndumbaro ameushukuru Uongozi wa klabu ya Simba kwa kuona umuhimu wa kuwachangia wenzetu wa Hanang huku akiwaomba wadau wengine kuguswa na kutoa kwa ajili ya wahanga.
“Kwa niaba ya Serikali tunaishukuru Simba kwa mchango huu mkubwa kwa ajili ya ndugu zetu wa Hanang waliopata matatizo huko Hanang, watafarijika sana wakiona msaada huu kutoka kwetu,” amesema Dk. Ndumbaro.
Msaada tuliotoa ni unga, mchele, mafuta ya kupikia, sabuni, maji ya kunywa ambayo tumejaza gari mbili.
Katika zoezi hilo la kukabidhi msaada huo limehidhuriwa na Katibu Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba, Imani Kajula pamoja na Katibu Mtendaji Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha.