NA WINFRIDA NGONYANI, DAR ES SALAAM
KLABU za Simba na Yanga huenda zikafikishwa mahakamani na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam, baada ya kutajwa kuwa ni miongoni mwa wadaiwa sugu wa kodi ya majengo katika manispaa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Manispaa hiyo kupitia Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Isaya Mngurumi, Simba inadaiwa jumla ya Sh 5,921,75 ya jengo lake lililopo Msimbazi Kariakoo wakati Yanga ikidaiwa Sh 664,152 eneo la Jangwani.
Wadaiwa wengine waliotajwa katika taarifa hiyo ni pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambao wao wanadaiwa Sh 3,798,152, Ilala Sharif Shamba na Klabu ya Gynmkana Dar es Salaam (DGC) wakidaiwa 1,873,697 eneo la Sea View.
Taarifa hiyo iliwataka wadaiwa wote kuhakikisha kuwa ifikapo Juni 30 mwaka huu wawe wamelipa madeni hayo, vinginevyo halmashauri itawafikisha mahakamani wale wote watakaoshindwa kulipa ndani ya muda uliotolewa.
MTANZANIA lilipata fursa ya kuzungumza na Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro, ambaye alisema yeye hahusiki na suala hilo na kudai kuwa ni la kiuongozi zaidi.