23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Simba, Yanga na aibu ya karne

simba-na-yanga

NA MARTIN MAZUGWA,

HII ni aibu ya karne kwa klabu kongwe za Simba na Yanga, kitendo cha kushindwa kumiliki uwanja hata wa mazoezi ni jambo linalozishusha hadhi klabu hizi zenye mashabiki wengi hapa nchini.

Licha ya ukongwe na kushinda vikombe mbalimbali kama ligi kuu, Tusker na Kagame, timu hizi zimeendelea kuugua ugonjwa wa viwanja na inashangaza kuona zikikodisha viwanja vya mazoezi kila mwaka huku viongozi wakibadilishwa kila muhula na klabu ikibaki vile vile.

Kitendo cha klabu hizi kutumia Uwanja wa Taifa katika michezo mikubwa inayozihusu klabu hizi si dhambi, lakini vitendo vinavyofanywa na mashabiki wa klabu hizi ni aibu, kuna haja ya kutoa elimu kwa wapenzi wao kuhusu kupenda rasilimali za taifa.

Kuna timu mbalimbali zinatumia viwanja vya Serikali lakini kwa heshima mfano katika Ligi Kuu ya Italia klabu kongwe na zenye mashabiki wengi, Inter Milan na AC Milan, zinatumia uwanja mmoja San Siro lakini huwezi ukasikia klabu moja imefungwa ikafanya uharibifu wa uwanja.

Klabu hizi zinapaswa kuacha kuishi kwa mazoea na kukubali kubadilika na kwenda na kasi ya mabadiliko ya mchezo wa soka ambao umekuwa ukikua siku hadi siku huku klabu ndogo zikijiimarisha, yale mambo ya kutumia gharama kubwa kwa mchezo mmoja ili kuridhisha nafsi zetu yamepitwa na wakati.

Yanga ambayo ndio klabu kongwe kuliko zote katika ligi kuu ilianzishwa Februali 11, 1935 ambayo imebeba vikombe 29, vikombe 20 vya ligi kuu, vitano vya Kagame na vinne vya Tusker, ilipaswa kuwa mfano wa kuigwa na timu zilizoanzishwa miaka ya hivi karibuni.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania bara kwa miaka mingi  waliyoshiriki ligi hiyo, ni aibu kukosa uwanja huku timu kama Mwadui na Azam zikiwa na viwanja vyao ambavyo vinaweza kutumika kwa michezo ya ligi kuu na ile ya kimataifa.

Simba ni klabu ya pili kwa ukongwe katika ligi kuu ikiwa imeanzishwa mwaka 1936 mara baada ya Yanga licha ya ukongwe wao mpaka sasa hawana uwanja wenye vigezo vya kucheza soka, hii ni aibu iliyoje.

Wakali hao wa mitaa ya Msimbazi Kariakoo imejikusanyia vikombe 31 vya mashindano mbalimbali ikiwemo 18 vya ligi kuu, vitano vya kombe la Tusker na sita vya kombe la Cecafa.

Wekundu wa Msimbazi ambao wana rekodi ya kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa kwa kufika katika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho mwaka 1993, wameendelea kubaki vile vile miaka nenda rudi pasipo kuwa na uwanja japo wa kubeba mashabiki 2,000.

Kitendo cha Serikali kuzitimua timu hizo kuacha kutumia uwanja wa taifa kutokana na kitendo chao kisichokuwa cha kiungwana cha kuharibu viti vya Uwanja wa Taifa, limekuwa gumzo mjini wakihaha kutafuta uwanja wa kuutumia katika michezo yao.

Miamba hii ya Kariakoo inapaswa kuamka katika usingizi  na kuanza kupanga mipango madhubuti  iwapo kama wanahitaji kupiga hatua kutoka hapo walipo na kufika levo ya timu kama TP Mazembe, Orlando Pirates, Zamaleki, Asante Kotoko na klabu nyingine kubwa barani Afrika, lakini ninaamini muda mfupi ujao, Simba watakuwa na uwanja wao kutokana na hali inayoendelea huko Bunju.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles