27.6 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Simba, Yanga katika mtihani

Na MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM


VIGOGO wa soka nchini, timu za Simba na Yanga, leo zitashuka katika viwanja tofauti kusaka pointi tatu katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Yanga itakuwa nyumbani ikiikaribisha Singida United katika Uwanja Taifa, Dar es Salaam, huku, Simba wakiwa ugenini dhidi ya Mwadui FC, katika Uwanja wa Mwadui Complex, mjini Shinyanga.

Yanga inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi tisa, baada ya kucheza michezo mitatu bila kupoteza, wakati Singida United inashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi saba,  baada ya kucheza michezo mitano, ikishinda miwili, sare mmoja na kupoteza miwili.

Katika msimu uliopita, timu hizo zilishindwa kutambiana baada ya kutoka sare katika michezo yote miwili.

Tangu Singida United wapande daraja msimu wa mwaka 2017/18, imepoteza mechi moja tu kati ya nne ilizokutana na Yanga msimu uliopita.

Mchezo huo pekee waliopoteza ni ule wa kirafiki ambao Yanga iliibuka na ushindi wa  mabao 3-2 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Yanga itashuka dimbani bila beki wake kisiki, Kelvin Yondani, ambaye ana kadi tatu za njano alizopata katika michezo iliyopita.

Simba inashika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi saba baada ya kucheza michezo minne, ikishinda miwili, sare mmoja na kupoteza mmoja, wakati Mwadui wanashika nafasi ya 18 kwenye msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi mbili, baada ya kucheza michezo minne, ikitoka sare miwili na kupoteza miwili.

Kikosi hicho cha Wekundu wa Msimbazi kitashuka kuikabili Mwadui kikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupokea kichapo cha bao 1-0 kutoka Mbao FC katika mchezo uliopita, katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Simba iliambulia pointi nne msimu uliopita katika michezo miwili dhidi ya Mwadui, ikianza kushinda mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza uliochezwa Dar es Salaam, kabla ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa marudiano uliochezwa Shinyanga.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, alisema wanataka kushinda mchezo huo ili kuendelea kuzichanga vema karata zao katika michezo ya nyumbani.

“Kila siku nawapanga wachezaji wangu wafanye mazoezi kwa nguvu na kufuata kile ambacho nawaelekeza, kwani nimefurahi kupata ushindi kwa mechi zote tatu na ninahitaji kuendeleza ushindani.

“Najua mchezo hautakuwa rahisi, kwani Singida United nao wamejipanga, hivyo watakabiliana nao kwa tahadhari ili kuhakikisha wanatoka na matokeo mazuri,” alisema.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Singida United, Hemedi Morocco, alisema anahitaji kushinda mchezo huo ili kujiongezea pointi tatu.

“Najua tunakutana na Yanga, ambayo haijapoteza mchezo hata mmoja, tunajua ubora wao, lakini tumejipanga kuhakikisha  tunaondoka na ushindi katika mchezo huo.

“Tunataka kuhakikisha tunapambana kushinda ili kumaliza hasira za kupoteza mchezo uliopita, tunajua ni timu yenye wachezaji wazuri, lakini kwetu sisi hatuangalii hilo, bali tunahitaji ushindi,” alisema Morocco.

Mbali na mchezo huo, ligi hiyo itaendelea katika  viwanja vingine, Kagera Sugar itakuwa ugenini kuikabili Mbeya City, katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Azam FC pia itakuwa ugenini katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, kuikabili Alliance.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles