27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Simba washikana uchawi, yamshtaki mwamuzi

Simba-vs-Yanga-8NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

KIPIGO ilichokipata timu ya Simba kwenye mchezo dhidi ya mahasimu wao, Yanga juzi kimezua mapya kwa wekundu hao baada ya wachezaji watatu wa safu ya ulinzi kudaiwa kufanya hujuma

Yanga ilivunja uteja dhidi ya Simba kwa kuichapa mabao 2-0 yaliyofungwa na washambuliaji, Amissi Tambwe na Malimi Busungu.

Habari za kutoka ndani ya Simba zilizolifikia gazeti hili zimedai kuwa wachezaji hao wa safu ya ulinzi walishindwa kabisa kuwazuia washambuliaji wa Yanga, waliofunga mabao rahisi jioni hiyo.

“Hali ndiyo iko hivyo, kuna wachezaji sehemu ya ulinzi wanashikwa uchawi ikidaiwa wamehongwa na wapinzani kuachia mabao kirahisi,” kilieleza chanzo hicho.

Chanzo hicho kiliendelea kueleza mara baada ya mambo kuwa hivyo, baada ya mechi wachezaji hao walipigwa mkwara na uongozi na baadhi ya wadau wengine wa Simba kwa kudaiwa kuihujumu timu.

MTANZANIA lilifanya jitihada za kuwapata viongozi wa Simba kuzungumzia suala hilo na alipotafutwa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Haji Manara, alisema huo ni uvumi tu na watatoa taarifa rasmi ya klabu kwa vyombo vya habari.

Hata hivyo, kwenye taarifa hiyo waliyoitoa Simba imekubaliana na matokeo hayo na kuipongeza Yanga na kuwashukuru mashabiki wao kumaliza mchezo salama licha ya mwamuzi Israel Nkongo, kuharibu mchezo kwa makusudi na kuwatukana wachezaji wa Simba.

“Nkongo kwa dhamira ya kusudi jana aliamua kuwatoa wachezaji wetu mchezoni kwa kuanza kugawa kadi pasipo na sababu na kwa rafu zilezile kuwaacha wachezaji wa Yanga kucheza bila kuwaonya,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Kilichoishangaza zaidi Simba ni kitendo cha mwamuzi huyo kushindwa kumtoa kwa kadi nyekundu mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma, aliyempiga kichwa cha makusudi beki Hassan Kessy.

Kutokana na matukio hayo ya mwamuzi, Simba imepeleka malalamiko kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Tanzania Bara (TPLB) ikitaka wayafanyie kazi na kuchukua hatua stahiki.

Hata hivyo, Kocha Mkuu wa Simba, Dylan Kerr, akiuzungumzia mchezo huo alisema walijimaliza wenyewe kwani walifanikiwa kumiliki mpira kipindi cha kwanza lakini walishindwa kutumia nafasi tatu walizotengeneza.

“Kwenye mchezo unaposhindwa kutumia nafasi ulizopata ni rahisi sana kufungwa na ndilo lililotukuta, tulitawala mpira kipindi cha kwanza lakini hatukuwa makini hata mabeki nao waliruhusu mabao kwa kushindwa kuwakaba vema wachezaji wa Yanga,” alisema.

Kerr aliongeza kuwa wanatarajia kujipanga upya na kusuka mipango ya kufanya vizuri katika mchezo ujao dhidi ya Stand United utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam keshokutwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles