Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Wanachama na mashabiki wa Klabu ya Simba kutoka katika matawi mbalimbali yaliyopo Wilaya ya Ilala wamesherehekea Siku ya Simba kwa kufanya usafi katika Hospitali ya Wilaya iliyopo Kivule na kutoa kitanda na vifaa vya usafi.
Akizungumza jana Kaimu Mwenyekiti wa Matawi ya Simba Wilaya ya Ilala, Abdallah Mwaijibe, amewapongeza wanachama na mashabiki kwa kujitoa kuisaidia jamii na kutaka matawi mengine kuiga mfano huo.
“Kwenye jamii yetu kuna changamoto nyingi na sisi kama wana Simba tumeguswa na kuchangishana kuja kuleta kidogo tulichokuwa nacho. Nayaasa matawi mengine ya Simba yaige mfano huu tujitoe kwa moyo mmoja,” amesema Mwaijibe.
Naye Mwenyekiti wa Tawi la Simba Kivule, Amos Hangaya, amesema walihamasishana na kuchangishana kisha kununua vifaa mbalimbali kikiwemo kitanda kimoja, vifaa vya usafi pamoja na kuchangia damu.
“Uongozi wa Wilaya ulituchagua Kivule kuwa wenyeji tunapoadhimisha Wiki ya Simba kwahiyo, matawi yote tumeungana na kila tawi limeweza kutoa vifaa kwa ajili ya hospitali pamoja na kufanya usafi na kuchangia damu…michezo siyo tu ushabiki ni pamoja na kuitumikia jamii na kuisaidia. Tunaamini mwakani tufanya kikubwa zaidi,” amesema Hangaya.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Thobias Nyamboto, ameshukuru kwa msaada huo na kuahidi kuwa watautumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Huu ni msaada mkubwa na kwa kweli mmeonyesha nia njema ya kuwahudumia Watanzania wenzenu, tunayaomba makundi mbalimbali yaone ni jambo jema ili nayo yaweze kushiriki katika kusaidia gurudumu la kuleta maendeleo katika sekta ya afya,” amesema Dk. Nyamboto.
Amesema hospitali hiyo kwa mwezi inahudumia wastani wa wagonjwa 100 mpaka 150 na kwa wajawazito kwa siku wanawapokea 30 mpaka 50.
Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa ambaye aliwakilishwa na Katibu wake Alphonce Msinduki, ameyapongeza matawi hayo na kuzitaka timu zingine kuiga mfano huo kwa kusaidia sekta mbalimbali kama ya afya.