NA MAREGESI NYAMAKA
-MUSOMA
WEKUNDU wa Msimbazi, Simba, wamezidi kuwabana pumzi wapinzani wao Yanga katika vita ya kuwania ubingwa baada ya jana kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Biashara United, mchezo uliochezwa Uwanja wa Karume, Musoma.
Baada ya ushindi dhidi ya Biashara United, Simba imefikisha pointi 69, baada ya kucheza michezo 27, ikishinda 22, sare tatu na kupoteza michezo miwili na kuendelea kukomaa katika nafasi ya pili.
Uongozi wa ligi hiyo unashikiliwa na Yanga yenye pointi 74, baada ya kushuka dimbani mara 32, ikishinda michezo 23, sare tano na kupoteza michezo minne.
Hata hivyo, kwa kuangalia rekodi hiyo ya michezo, Simba ina akiba ya michezo mitano mkononi ili kulingana na Yanga.
Dakika 10 za mwanzo timu hizo zilishambuliana kwa zamu, huku kipa wa Simba, Deogratias Munishi, akiokoa hatari mbili zilizoelekezwa langoni mwake.
Dakika ya 27, mkwaju mkali wa Saidi Ndemla wa Simba ulipaa juu ya lango la Biashara United.
Dakika ya 33, mshambuliaji, John Bocco, aliifungia Simba bao la kuongoza baada ya kupokea pasi ya Mzamiru Yassin na kuwazidi kasi mabeki wa Biashara United na kufyatua fataki la mguu wa kushoto na mpira kutinga wavuni.
Dakika ya 40, Bocco aliendelea kusababisha maumivu kwa Biashara United, baada ya kuifungia Simba bao la pili kwa kichwa, akipokea pasi ndefu ya Asante Kwasi.
Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilikamilika kwa Simba kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0 dhidi ya Biashara United.
Kipindi cha pili kilianza kwa kila upande kuzidisha kasi ya mashambulizi kwa lengo la kupata bao.
Dakika ya 52, mwamuzi wa mchezo huo, Ally Simba wa Geita, alimlima kadi ya njano, Taro Donald, baada ya kumchezea madhambi, Mohamed Ibrahim.
Simba ilifanya mabadiliko dakika ya 53, alitoka Bocco na kuingia Emmanuel Okwi.
Dakika ya 67, Biashara ilifanya mabadiliko alitoka, Makanga na kuingia Juma Mpakala.
Dakika ya 70, Haruna Niyonzima, alionyeshwa kadi ya njano baada ya kumchezea madhambi Taro kabla ya dakika moja baadaye kulimwa kadi nyekundu kutokana na kuonyesha mchezo usio wa kiungwana na kupinga uamuzi wa mwamuzi.
Dakika ya 74, Simba ilifanya mabadiliko alitoka Kagere na kuingia Hassan Dilunga, kabla ya dakika ya 76, Biashara United kufanya mabadiliko ambapo alitoka Taro na kuingia Kauswa Benard.
Dakika ya 78, James Kalimba wa Biashara alilimwa kadi ya njano kwa kumchezea madhambi Dilunga.
Kocha wa Simba, Patrick Aussems, alilazimika kufanya mabadiliko mengine dakika ya 85, alimtoka Kwasi baada ya kuumia na kumwingiza, Yusuph Mlipili.
Pamoja na mabadiliko yaliyofanyika kila upande kipindi cha pili, dakika 90 za pambano hilo zilikamilika kwa Simba kutakata kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Biashara.
Baada ya mchezo huo, Aussems, alisema wanarejea Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao dhidi ya JKT Tanzania utakaopigwa kesho kutwa.