DAMIAN MASYENENE, MWANZA
Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba SC, wanatarajiwa kuwa wageni wa klabu ya Gwambina FC ya wilayani Misungwi mkoani Mwanza katika mchezo wa kirafiki wa uzinduzi uwanja wa kisasa wa Gwambina Stadium utakaofanyika Juni 21.
Simba Sc wanatarajia kuwasili wilayani humo Alhamisi Juni 20 ambapo uzinduzi wa uwanja huo utasindikizwa na burudani kadhaa za wasanii na ngoma za asili kutoka sehemu mbalimbali ikiwemo bendi ya Twanga Pepeta ya jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Gwambina FC, Daniel Kirahi, wamechagua kuwaalika Simba kwasababu ina mashabiki wengi na ni mabingwa wa nchi hivyo itawasaidia kunogesha sherehe hizo na kujaza uwanja.
Naye Kocha wa Gwambina FC, Fulgence Novatus, amesema mchezo huo ambao ni sehemu ya michezo Sita ya kirafiki aliyoiandaa utasaidia kubaini vijana atakaounda nao timu ya kiushindani.
Uwanja huo upo katika Mtaa wa Mbela Kijiji cha Domi kilometa tatu kutoka mji wa Misungwi na Kilometa 45 kutoka jijini Mwanza, una majukwaa manne yenye uwezo wa kubeba watazamaji zaidi ya 10,000 walioketi, hosteli zenye vyumba 17 vya wachezaji, nyumba ya kocha mkuu na wasaidizi wake, sehemu ya chakula na eneo la kuegesha magari.