27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Bageni aomba kufutiwa adhabu ya kunyongwa

Na Kulwa Mzee

-Dar es Salaam

ALIYEKUWA Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kinondoni, SP Christopher Bageni, ameomba Mahakama ya Rufaa imfutie adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Alihukumiwa adhabu hiyo kwa kosa la kuwaua kwa makusudi wafanyabiashara wanne wa madini kutoka Mahenge mkoani Morogoro na dereva teksi katika Msitu wa Pande, Dar es Salaam.

Bageni kupitia wakili wake Gaudioz Ishengoma, aliwasilisha hoja katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania mbele ya jopo la majaji watatu; Stellah Mugasha, Ferdinand Wambali na Rehema Kerefu wanaosikiliza maombi ya marejeo ya hukumu dhidi yake iliyotolewa Septemba 13, 2016 na kusomwa Septemba 16, 2016  na aliyekuwa Msajili wa Mahakama hiyo, John Kahyoza.

Mleta maombi alitiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu hiyo na jopo la majaji watatu; Benard Luanda, Sauda Mjasiri na Senistocles Kaijage.

Akiwasilisha sababu mbili za kuomba marejeo, Ishengoma anadai mteja wake alinyimwa haki ya kusikilizwa wakati wa kutathmini ushahidi ulioko kwenye kumbukumbu za mahakama kwa kuegemea tu kwenye ushahidi wa upande wa mashtaka.

Alidai katika kuchanganua ushahidi, mahakama ilishughulika na ushahidi wa msingi wa upande wa mashtaka na iliangalia kwa juu juu tu ushahidi wa utetezi, hususan wa Bageni au haikuutazama kabisa.

Ishengoma alidai mahakama ilimtia hatiani mrufani kwa hoja ambazo hazikujadiliwa wakati wa usikilizwaji wa rufaa iliyokatwa na Jamhuri, wakipinga Mahakama Kuu kuwaachia huru washtakiwa.

“Mahakama Kuu ilisema washtakiwa wote walikuwepo msituni, lakini mahakama haiwezi kumtia hatiani mtu aliyesaidia mauaji na kumwacha aliyeua,” alidai.

Alidai Mahakama Kuu ilisema kosa la kuua na kosa la kusaidia kuua ni makosa mawili tofauti, hivyo si sahihi kwa mtu aliyeshtakiwa kwa mauaji kutiwa hatiani kwa kosa jingine ambalo tangu mwanzo mshtakiwa alitakiwa kulijua ili aweze kujitetea.

Ilisema makosa hayo si makosa yanayofanana, hivyo mahakama hiyo ilitofautiana na hoja za upande wa Jamhuri, kwamba washtakiwa watiwe hatiani kwa kosa la kusaidia kuua baada ya kushindwa kutiwa hatiani kwa mauaji.

“Jamhuri katika sababu za kukata rufaa, walitaka washtakiwa wote watiwe hatiani kwa sababu walionekana walikuwepo msituni Pande.

“Mahakama badala ya kujikita katika eneo hilo, yenyewe ilijiuliza maswali kwamba walienda Pande kufanya nini, walipelekwa na nani, hoja ambazo hazikuwepo katika sehemu ya mabishano. Mrufani alijikita kujibu sababu za rufaa na sio maswali yaliyoibuliwa na mahakama,” alidai.

Alidai katika utetezi wake, Bageni alisema hakwenda msituni, lakini mahakama ilipochambua ushahidi iliangalia ushahidi wa upande wa Jamhuri na kuacha utetezi wa mshtakiwa na haikusema chochote kuhusu utetezi huo.

Akizungumzia sababu ya pili ya kuomba marejeo, alisema kulikuwa na dosari ya wazi katika kumbukumbu za mahakama.

Ishengoma alidai ushahidi uliochukuliwa na mahakama kwamba Bageni alidanganya kwamba wafanyabiashara walikufa baada ya kushambuliana kwa risasi na polisi haupo mahali popote.

“Ushahidi kwamba Bageni ndiye alikuwa na cheo kikubwa kuliko wengine katika timu iliyokwenda Pande, na kwamba alikuwa na uwezo wa kutoa amri, huo pia haupo kokote,” alidai.

Aliiomba mahakama ifute uamuzi wake wa kumtia hatiani mleta maombi kwa sababu ilimtia hatiani kwa ushahidi ambao haukujadiliwa katika usikilizwaji wa rufaa.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ladislaus Komanya, akijibu hoja za mleta maombi, alidai anapinga maombi yaliyowasilishwa, na kwamba mleta maombi alisikilizwa sana.

Alidai hakuna makosa ya wazi yaliyofanywa na mahakama, hivyo maombi hayana msingi, yatupiliwe mbali.

“Mleta maombi alipata nafasi ya kusikikizwa kikamilifu na alikuwa na mwakilishi mahakamani,” alidai Komanya.

Katika hati ya kiapo iliyoapwa na Wakili Ishengoma, Bageni anadai yeye na wengine wanane ambao hawako katika maombi hayo, walishtakiwa Mahakama Kuu kwa makosa ya mauaji ya watu wanne katika kesi ya jinai namba 26 ya mwaka 2006.

Bageni alikuwa mshtakiwa wa pili na katika hukumu iliyotolewa na Jaji Salum Massati mwaka 2009, wote waliachiwa huru, lakini Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hakuridhishwa na uamuzi huo, hivyo alikata rufaa dhidi yao katika rufaa namba 358 ya mwaka 2013.

Kabla ya usikilizwaji wa rufaa hiyo, DPP aliwaondolea rufaa wajibu rufaa watano na kubaki wajibu rufani wanne ambao waliachiwa huru pia Septemba 16 mwaka huo.

Walioachiwa huru ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam (RCO), Kamishna Msaidizi wa Polisi Abdallah Zombe, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Ahmed Makelle na Rajabu Bakari baada ya mahakama kuona hakuna ushahidi wa wazi ama mazingira kuwatia hatiani.

Katika kesi ya msingi, Bageni alidaiwa kuwaua kwa kukusudia wafanyabiashara Sabinus Chigumbi, maarufu Jongo na ndugu yake, Ephrahim Chigumbi, Mathias Lunkombe na Juma Ndugu, aliyekuwa dereva wa teksi wa Manzese, Januari 14, mwaka 2006 katika Msitu wa Pande, Mbezi Luis.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles