*Yaiua Kagera, Kiiza akipiga ‘hat trick’, waionyeshea Yanga alama ya saa
*Azam, Mtibwa Sugar nazo zaendeleza dozi, Coastal Union mambo magumu
NA JUDITH PETER, DAR ES SALAAM
TIMU ya Simba imeonekana kuwa moto wa kuotea mbali kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), baada ya kupata ushindi wa tatu mfululizo kwa kuichapa Kagera Sugar mabao 3-1 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba kabla ya kuingia kwenye mchezo huo iliweza kuzichapa ugenini timu za Tanga, African Sports bao 1-0 na Mgambo JKT 2-0 mechi zote zikifanyika Uwanja wa Mkwakwani.
Wakati Simba ikifanya hayo, matajiri Azam FC na Mtibwa Sugar nazo ziliendeleza ushindi wao kwa asilimia 100, Azam ikiichapa Mwadui bao 1-0 ugenini kwenye Uwanja wa Mwadui na Mtibwa Sugar ikiichabanga Ndanda 2-1 ndani ya Uwanja wa Manungu, Morogoro.
Shujaa wa Simba kwenye mchezo wa jana alikuwa ni mshambuliaji wake mpya kutoka Uganda, Hamis Kiiza ‘Diego’, aliyefunga mabao hayo yote na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza Ligi Kuu msimu huu kufunga hat trick.
Simba ilianza kwa kasi mchezo huo, mshambuliaji wake, Ibrahim Ajibu, alikosa bao akiwa kwenye nafasi nzuri akizidiwa ujanja na mkongwe wa Kagera Sugar, George Kavila aliyeokoa vizuri.
Kiiza alisawazisha makosa kwa kuipa uongozi Simba dakika ya 30 baada ya kufunga bao la kwanza kwa kichwa akiunganisha krosi iliyochongwa na kiungo Awadh Juma, hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Simba ilienda ikiwa mbele kwa bao hilo.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa Simba, ambapo alikuwa ni Kiiza tena aliyetikisa nyavu za Kagera Sugar kwa mara ya pili kwa kichwa dakika ya 46 akiunganisha mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na beki, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, faulo hiyo ilitokana na kiungo wake, Peter Mwalyanzi, kufanyiwa madhambi na mabeki wa Kagera.
Kagera Sugar ilicharuka dakika ya 50 baada ya kuandika bao pekee walilopata kwenye mchezo huo lililofungwa na Mbaraka Yussuf, aliyetumia vema uzembe wa beki wa Simba, Hassan Isihaka aliyeshindwa kumkaba vema na kupiga shuti lililopita katikati ya miguu ya kipa wa Simba, Manyika Peter na kutinga wavuni.
Kiiza aliihakikishia ushindi Simba kwa kufunga bao la tatu dakika ya 90 kwa shuti zuri nje ya eneo la 18 lililomshinda kipa wa Kagera Sugar, Agatony Anthony na mpira kuisha kwa matokeo hayo.
Kituko kilichotokea kwenye mchezo huo ni wachezaji wa Simba pamoja na Mkuu wa Idara ya Habari ya Mawasiliano ya timu hiyo, Haji Manara, kuonyesha ishara ya saa kwa kidole kugusishwa kwenye sehemu inapovaliwa saa mkononi tukio ambalo lilidaiwa kuwa wanawaonyeshea mahasimu zao Yanga ambao wanacheza nao Jumamosi hii.
Kwenye Uwanja wa Mwadui, bao pekee la Azam lilifungwa na nahodha wake, John Bocco kwa shuti akiwa ndani ya eneo la 18 na kumwacha kipa wa Mwadui, Shaban Kado akiuangalia mpira ukitinga wavuni bila kufanya lolote.
Lakini Azam ilicheza pungufu kwa takribani dakika 37 baada ya kupata pigo dakika ya 53 kufuatia beki wake, Aggrey Morris, kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi kwa kumfanyia madhambi mshambuliaji wa Mwadui, Paul Nonga, ndani ya eneo la hatari na kuwa penalti.
Hata hivyo, Mwadui ilishindwa kutumia vema penalti hiyo kusawazisha bao hilo baada ya mshambuliaji, Rashid Mandawa kuikosa kufuatia kipa wa Azam, Aishi Manula kuicheza vema kwa kuipangua.
Mwadui iliyoonekana kucheza vizuri baada ya Azam kupata kadi hiyo ilikosa mabao mengi ya wazi kupitia washambuliaji wake Mandawa na Nonga.
Mtibwa Sugar iliyoibuka na ushindi wa mabao 2-1, yenyewe ilijipatia mabao yake kupitia kwa beki Salim Mbonde na Said Bahanuzi huku la Ndanda likifungwa na Kigi Makasi.
Mechi nyingine iliyofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani, wenyeji Coastal Union waliendeleza mwenendo mbaya kwenye ligi kwa kulazimishwa suluhu na Toto Africans ya Mwanza.
Coastal Union mpaka sasa haijaonja ladha ya ushindi ikifungwa mabao 2-0 na Yanga, ikafungwa tena na Ndanda bao 1-0 kabla ya jana kuambulia suluhu hiyo.
Baada ya matokeo hayo, Yanga imeendelea kukaa kileleni ikiwa na pointi tisa sawa na Simba iliyo nafasi ya pili, Azam inafuatia nafasi ya tatu na Mtibwa nafasi ya nne.
Mkiani zipo JKT Ruvu na African Sports ambazo hazijaambulia pointi yoyote mpaka sasa.