33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA KUIKABILI LIPULI NA TAHADHARI

Na MOHAMED KASSARA


-DAR ES SALAAM

Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, ametamba kuwa kikosi hicho kimejipanga vizuri kuhakikisha kinashinda mchezo wao ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Lipuli FC, ili kuvunja mwiko wa timu hiyo kushindwa kuvuna  pointi tatu katika michezo miwili ya ya msimu uliopita.

Simba itashuka dimbani kuikabili Lipuli katika mchezo wa ligi hiyo utakaochezwa Septemba 14 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Timu hiyo ilishindwa kupata ushindi katika michezo miwili dhidi ya Lipuli, ambapo ilianza kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kabla ya kupata matokeo kama hayo katika mchezo wa marudiano uliochezwa kwenye Uwanja wa Samora, Iringa.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Djuma alisema kikosi hicho kimepanga kuhakikisha kinashinda mchezo huo, ili kuvuna pointi zote tisa katika michezo yao ya nyumbani.

Alisema kikosi chake kimepania kuichapa Lipuli ili kufuta rekodi yao mbaya ya kushindwa kupata pointi tatu dhidi ya timu hiyo iliyowatesa msimu uliopita.

“Tunaendelea kujiandaa na mazoezi kwa ajili ya kuhakikisha tunaendeleza wimbi la ushindi, lengo letu ni kutetea ubingwa wetu, hivyo kila mchezo kwetu ni kama fainali, tumepanga kuhakikisha tunapata pointi tisa nyumbani, kabla ya kuanza kwenda kuzisaka za ugenini.

“Lipuli ni timu nzuri, ndiyo maana tunaweka umakini wa kutosha katika maandalizi ya kuelekea mchezo huo, walitusumbua sana msimu uliopita, hatukuweza kushinda mchezo kwao, safari hii tumejipanga kikamilifu kuhakikisha tunavunja mwiko huo, tuna kikosi kipana na imara ambacho kinaweza kutupa pointi tatu katika mchezo huo,” alisema Djuma, raia wa Burundi.

Lipuli inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi sita, baada ya kushinda michezo miwili dhidi ya Tanzania Prisons na Mbeya City.

Kikosi hicho kinachonolewa na Mbelgiji, Patrick Aussems, kilianza msimu kwa kuichapa Prisons bao 1-0 Uwanja wa Taifa, kabla ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City, pia kwenye uwanja huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles