23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Simba juu kileleni

1(31)NA JENIFER ULLEMBO, DAR ES SALAAM

TIMU ya Simba imefanikiwa kukwea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya timu ya Mbeya City, katika mchezo uliochezwa jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa matokeo hayo, Simba inakaa kileleni ikiwa na pointi 48, ikifuatiwa na Yanga na Azam zote zikiwa na pointi 47, zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.

Mchezo huo ulianza kwa kasi kwa timu zote kushambuliana kwa zamu, huku Simba ikionekana kuwa na njaa ya kusaka bao la kuongoza ili kuweza kupata nafasi ya kuongoza Ligi hiyo.

Mbeya City ikiwa inaongozwa kwa mara ya kwanza na Mmalawi Kinnah Phiri kwenye mchezo dhidi ya Simba tangu ajiunge nao, ndiyo iliyokuwa ya kwanza  kupeleka shambulizi  kali langoni mwa Simba katika dakika nne za mwanzo, kupitia  kwa mchezaji wake, Ditram Nchimbi, aliyeachia shuti kali lililoishia  kugonga nyavu za pembeni na kutoka nje.

Hata hivyo, dakika 12 baadaye mshambuliaji wa Simba, Hamis Kiiza, alishindwa kuiandikia timu yake bao la kuongoza baada ya shuti lake kuokolewa na kipa wa Mbeya City, Hannington Kalyesebula.

Presha ya mara kwa mara langoni mwa Mbeya City ilichangia kiungo wa timu hiyo, Haruna Moshi kupewa kadi ya njano dakika ya 44, baada  kumfanyia madhambi mchezaji wa Simba, Juuko Murshid.

Timu hizo zilikwenda mapumziko bila yoyote kuona lango la mwenzake, licha ya kuwa zilikuwa zinaonekana kuwa na uchu wa mabao kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, ambapo dakika ya 56 Raphael Alpha wa Mbeya City alipewa kadi ya njano baada ya kumcheza vibaya Justice Majabvi.

Baada ya mashambulizi ya muda mrefu, Danny Lyanga aliwanyanyua mashabiki wa Simba walioanza kukata tamaa vitini, baada ya kuandika bao la kuongoza dakika ya 75, akiunganisha vema pasi ndefu ya Awadhi Juma.

Bao hilo liliamsha ari kwa wachezaji wa Simba, ambao walilishambulia kama nyuki lango la Mbeya City na kufanikiwa kuongeza bao la pili dakika ya 88 kupitia kwa Ibrahim Ajib, aliyepiga shuti lililomgonga  beki wa Mbeya City, Hassan Mwasapili.

Shuti hilo lilimshinda beki huyo na kujikuta akiusindikiza  mpira  wavuni, akiwa katika harakati za kuokoa  na kusababisha Simba  kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Kikosi cha Simba: Vicent Angban, Emery Nimuboma/Hassan Kessey, Mohamed Hussein, Novaty Kufunga, Juuko Murshid, Justice Majabvi, Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude, Hamis Kiiza/Awadhi Juma, Ibrahim Ajib na Brian Majwega/Daniel Lyanga.

Mbeya City: Hannington Kalyesebula, Hassan Mwasapili, Abubakar Shabani, Tumba Sued, Haruna Shamte, Kenny Ally, Raphael Alpha, Haruna Moshi/Themi Felix, Geofrey Mlawa, Joseph Mahundi na Ditram Nchimbi/Ramadhan Chombo, huku mwamuzi akiwa Rajabu Mrope kutoka Ruvuma.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles