26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 14, 2024

Contact us: [email protected]

Simba, Coastal mechi ya kisasi

NA MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM

KIKOSI cha Wekundu wa Msimbazi, Simba leo kitashuka dimbani kusaka pointi tatu dhidi ya Coastal Union, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Simba itaingia uwanjani, ikitoka kuichakaza Alliance FC mabao 5-1, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Timu hiyo inaongoza msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 84, badaa ya kucheza michezo 36, ikishinda michezo 26, sare sita na kupoteza minne.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara, watataka kuendeleza utemi wao na kuongeza hamasa kuelekea mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Namungo, utakaochezwa Agosti 2, mwaka huu Uwanja wa Nelson Mandela, Rukwa.

Coastal wanayokutana nayo,inashika nafasi ya sita, ikiwa na pointi 52, baada ya kucheza michezo 36, ikishinda 14, sare 10  na kupoteza 12.

Wagosi hao wa Kaya wanarejea nyumbani, baada ya kumaliza ziara yao ya michezo sita ya ugenini na kuvuna pointi nne.

Timu hiyo itashuka dimbani kuikabili Simba, ikitoka kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Biashar Unite, mchezo uliochezwa Uwanja Karume, Mara.

Simba inajivunia ushindi wa mabao 2-0 ilioupata katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Februari Mosi, mwaka huu Uwanja wa Taifa.

Kingine kinachoipa Simba sababu ya kujiamini ni ushindi wa mabao 2-1, ilioupata mara ya mwisho ilipokanyaga Mkwakwani, katika mchezo wa duru ya kwanza wa msimu uliopita uliochezwa April 7, mwaka jana.

Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenblock alisema atautumia mchezo huo kukiandaa kikosi chake kwa ajili ya kuikabili Namungo katika mchezo fainali.

Alisema licha ya kuwa tayari wameshatwaa ubingwa, lakini watahakikisha washinda  mchezo huo ili kumaliza ligi hiyo kwa kishindo.

 “Mchezo huu na ule wa Polisi itakuwa kwa ajili ya kujiandaa na fainali, tunataka tukamilishe ratiba ya ligi kwa kishindo kabla ya kuelekeza nguvu zetu kuivaa Namungo,”alisema Sven.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Coastal, Juma Mgunda alisema, atahakikisha wanashinda mchezo huo ili kupiga hatua nyingine kwenye msimamo wa ligi.

“Tumefanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya mchezo huo, tunataka kushinda, japo hatushuki, lakini haturidhiki na nafasi tuliyopo, tunatamani kwenda mbele zaidi ya hapa,” alisema Mgunda.

Michezo mingine iliyopigwa jana, Mbao ilifufua matumaini ya kusalia Ligi Kuu,baada ya kuibuka na ushindi wa maba 3-0 dhidi ya Namungo, mchezo uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Ushindi wa jana uliiwezesha Mbao kufikisha pointi 42 na kukamata nafasi ya 16 katika msimamo wa ligi hiyo, ikitoka nafasi ya 19, miongoni mwa timu 20 zinazoshiriki ligi hiyo.

Tanzania Prisons ilishinda bao 1-0 dhidi ya KMC, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Mwadui ikailaza bao 1-0 Biashara United,wakati Kagera Sugar ikaibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Singida United, Uwanja wa Liti, Singida.

Ligi hiyo itaendelea leo kwenye viwanja vinne, Azam itakuwa ugenini kusaka pointi tatu mbele ya Mbeya City Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Lipuli itakuwa na shughuli pevu dhidi ya Ruvu Shooting, mtanange utakaopigwa Uwanja wa Samora,Iringa.

Polisi Tanzania itaialika JKT Tanzania dimba la Ushirika,Kilimanjaro.

Ndanda ambayo inapambana kujinasua na hatari ya kushuka daraja,itakuwa na kazi nzito ya kusaka pointi tatu ugenini dhidi ya wenyeji wao, Alliance, Uwanja wa Nyamagana, Mwanza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles