Na Mwandishi Wetu
Mpiga mpira wa timu ya Taifa ya kriketi ya wavulana wenye umri chini ya miaka 19 ya Tanzania, Mohamed Simba, ameonyesha umahiri kwa kuingoza timu hiyo kufuzu kushiriki katika michuano ya Daraja la Kwanza ya Afrika kwa kuifunga Sierra Leone katika fainali ya michuano ya Daraja la Pili iliyochezwa jijini Dar es Salaam, Agosti 11,2024
Ushindi wa mikimbio 36 dhidi ya Sierra Leone uliifanya Tanzania kuwa bingwa wa taji la michuano ya Daraja la Pili ya Afrika ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia kwa vijana linaloandaliwa na Baraza la Kimataifa la mchezo huo (ICC)
Tanzania ambayo ni wenyeji wa michuano hiyo waliibuka na ushindi kwa sheria ya Duckworth-Lewis (D/L), ambayo hushuhudia ova zikipunguzwa kulingana na hali ya hewa na mazingira ya uwanja na timu yenye zamu ya kupiga mpira wakati huo ikiwa na jukumu la kuifikia idadi ya mikimbio iliyowekwa katika ova zilizopunguzwa.
Timu ya taifa ya Sierra Leone ilipata fursa ya kuanza kurusha mpira katika mechi hiyo, ambayo haikukamilisha ova 50 kwa kila timu kutokana na mvua iliyoathiri uwanja, na kuidhibiti Tanzania ambayo ilimaliza zamu ya kupiga mpira ikiwa na mikimbio 178 huku ikipoteza wiketi nane (wapigaji nane) katika ova 50.
Chipukizi Simba alikuwa mpiga mpira aliyekuwa na mikimbio mingi katika timu ya Tanzania, akimaliza akiwa na mikimbio 29 katika mipira 37 aliyopiga, na wenzake- Laksh Bakrania ambaye pia ni nahodha wa kikosi (mikimbio 24) na Darpan Jobanputra (mikimbio 21) pia walikuwa na mchezo mzuri.
Warusha mpira wa Sierra Leone, nahodha Raymond Coker, George Sesay, na Mohamed Turay walimaliza zamu zao za kurusha mpira wakiwa na wiketi mbili kila mmoja, wakipambana kuizuia Tanzania isimalize ikiwa na idadi kubwa ya mikimbio.
Ilipofika zamu ya Sierra Leone kupiga mpira, kikosi hicho- kilichotakiwa kupata mikimbio 135 katika ova 29- ilishindwa kuonyesha makali kwani iliishia kupata mikimbio 98 huku ikipoteza wiketi (wapiga mpira) nane katika ova hizo 29.
Mpiga mpira Sahr Lebbie ndiye aliyemaliza zamu hiyo akiwa na mikimbio mingi, akipata 30, na mchezaji mwingine James Bangura alipata mikimbio 16.
Warusha mpira wa Tanzania, Khalidy Amiri na Hamza Ally, walionyesha umahiri wao baada ya kupata wiketi mbili kila mmoja wakati wa zamu ya kikosi hicho kurusha mpira na kuzuia (fielding).
Pamoja na kupoteza mechi yo ya fainali, ilifuzu kushiriki katika michuano ya Daraja la Kwanza ya Afrika kutokana na kukata tiketi ya kucheza fainali hiyo ya Jumapili.
Nigeria, iliyomaliza katika nafasi ya tatu baada ya kuishinda Rwanda kwa wiketi saba katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu, pia imefuzu kushiriki katika michuano ya Daraja la Kwanza ya Afrika.
Tanzania, Sierra Leone, na Nigeria, kwa maana hiyo, zitapambana na Kenya, Namibia, na Uganda katika michuano ya Daraja la Kwanza ya Afrika ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia la mchezo huo linalozikutanisha timu zinazoundwa na vijana wenye umri chini ya miaka 19.
Timu hizo sita zitakuwa zikiwania nafasi moja ya kuiwakilisha Afrika katika michuano ya Kombe la Dunia la Kriketi ya ICC inayohusisha vijana wenye umri chini ya miaka 19 inayotarajiwa kufanyika katika nchi za Namibia na Zimbabwe mwaka 2026.