29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

SIKU KUMI ZA ‘DAR MPYA’ ZITASABABISHA MAPYA?

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

NA INNOCENT NGANYAGWA,

HIVI karibuni, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alifanya ziara ya siku kumi kusikiliza kero mbalimbali za wananchi anaowaongoza na kuzipatia majibu ya papo kwa hapo kwa alizoweza kufanya hivyo, kutoa matamko na maagizo kwa zinazohitaji mchakato wa utatuzi. Aliambatana na watendaji mbalimbali waliopaswa kujibu baadhi ya kero hizo katika ziara hiyo iliyopewa jina la ‘Dar Mpya: Majibu ya kero za wananchi’.

Nilifuatilia kwa karibu ziara hiyo ili kubaini yanayojiri kwa muktadha wangu wa kufanya majumuisho katika ‘Tafakuri Yangu’ kuhusu mafanikio, changamoto na upungufu kutokana na ziara hiyo iliyokamata hisia za wakazi wa jiji hili na

wananchi kwa ujumla, kwa kufuatiliwa kwa kina na vyombo mbalimbali vya habari kiasi cha kujenga mvuto wa ushabiki kama ilivyo kwenye michezo, hususan kandanda.

Kwa muda jina la Mkuu wa Mkoa Makonda lilitamalaki katika wigo wa habari na tafakuri za watu wa kada mbalimbali kwa nafasi zao. Baadhi ya niliyoyabaini katika majumuisho yangu kwanza kwa mkuu huyo wa mkoa kufanya jambo adimu kutoka ofisini kwenda mwenyewe kukutana na wananchi badala ya kusubiri kuletewa taarifa, pengine ambazo hana uhakika nazo au zisingemwezesha kufahamu kwa haraka yanayowasibu wananchi wake, ambao wana manung’uniko mengi yanayowaacha wakiwa na nafsi zinazousononekea uongozi wake wa jiji.

Kwa hatua aliyochukua ya kutumia siku kumi kuzungukia wilaya tano za jiji hili linalokua kwa kasi, amefanikiwa kusababisha mabadiliko kadhaa, ikiwemo chachu kwa viongozi wenzake walio katika nafasi kama yake, kujiwekea mkakati wa kusikiliza kero za wananchi wanaowatumikia kwa kuwafuata badala ya kusubiri kuletewa ambapo ugumu wa kuwafikia ungesababisha zisipate utatuzi wa haraka.

Tayari wengine wameanza kufuata nyayo zake kama taarifa zinavyodhihirisha, lakini la pili ni hamasa na imani ya wananchi kwa kiongozi wa nafasi yake, kutokana na kujitokeza na kuongea bila hofu kuhusu madhila wanayofanyiwa na baadhi ya viongozi wa ngazi za chini wa Serikali wanaowasimamia kwa masuala  mbalimbali.

Naye hakusita kuchukua au kuagiza hatua stahiki papo kwa hapo, ikiwemo zilizomo ndani ya mamlaka yake, tumeshuhudia baadhi ya viongozi walioamriwa kuwekwa ‘mahali husika’ ili watoe majibu stahiki kutokana na uwajibikaji mbovu au kukengeuka kwa kukiuka misingi ya mamlaka waliyokasimiwa.

Jambo la tatu lililodhihirika hata kwa ofisi yake mwenyewe kuwa kuna baadhi ya kero zinazowasilishwa hazipati majibu ya haraka, kutokana na walichotamka baadhi ya wananchi kwamba walishawasilisha vielelezo vyao ofisini kwake.

Jambo la nne lililodhihirika ni baadhi ya wananchi kutaka viongozi wao ‘watumbuliwe’ kwa kutoa kero wasizokuwa na uhakika wala ushahidi nazo zilizopingwa na wenzao, hii ikidhihirisha kuwa kuna dhana potofu miongoni mwa wananchi kwamba kila kiongozi anastahili kutumbuliwa hata kama anatimiza majukumu yake ipasavyo, pengine ni mambo yaliyo juu ya uwezo wake kimamlaka asiyoweza kutekeleza ndiyo yanayomkwamisha.

Jambo la tano lililodhihirika ni kwa baadhi ya watendaji kuuza sura mbele ya hadhira na Mkuu wa Mkoa, kwa kuwa baadhi ya kero walizotakiwa kuzitolea majibu kwa nafasi zao za kiutendaji walipaswa kuwa wameshazishughulikia ofisini, si kuja kutoa maelezo kwenye mikutano. Inazua swali katika tafakuri yangu, je, kama Mkuu huyo wa Mkoa asingefanya ziara kwa utashi alioamua wangetoa wapi majibu ya viporo walivyokalia hadi vikachacha?

Jambo la sita ni kutokuwepo kwa muunganiko wa utendaji kwa baadhi ya maeneo ya usimamizi, kwa kuwa kuna kero  inazowakabili wananchi ambazo viongozi wanaowasimamia kwenye ngazi za chini baadhi walijitetea kukosa uwezeshwaji wa kuzishughulikia na walipoamua kushirikiana na wananchi kutafuta uwezo wa rasilimali fedha ili kuzitatua, wakatuhumiwa kuchangisha fedha kwa sababu zisizojulikana.

Jambo la saba ni rushwa ambayo imejidhihirisha kuwa bado ni adui wa haki, kwa kuwa baadhi ya malalamiko ya wananchi, yalituhumu kuombwa rushwa na baadhi ya watendaji, hususan katika vyombo vya dola, ingawa wakuu waliokuwa kwenye msafara walitoa matamko ya kuchukua hatua.

Jambo la nane ni kutoweza kusikilizwa kero zote katika kila mkutano, ikimaanisha kuwa lazima kuimarisha misingi ya utaratibu wa kuhudumia wananchi, kwa kuwa sidhani kama Mkuu wa Mkoa atakuwa na nafasi ya kufanya ziara kila mara.

Jambo la tisa ni udhihirisho kuwa kama kiongozi akitumia muda wake kushughulikia yaliyomweka uongozini ili kuwatumikia wananchi, anakuwa ametimiza wajibu, badala ya ‘promo’ za kutuhumiana walio katika uongozi kuhusu mambo ambayo wanapaswa kuyatafutia ufumbuzi wa pamoja, hata yanapokuwa magumu kutatuliwa.

Kumi na mwisho, ingawa si kwa umuhimu, ni subira ya muda gani tunaopaswa kusubiri ili tupate utatuzi wa kero hizo? Hivyo ndivyo tafakuri yangu ilivyotafakari muarobaini wa siku kumi kama utatutatulia kero.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles